Vaileth Elisa - Ofisa miradi msaidizi - Shirika la Kivulini akiendesha zoezi la utambulisho kwa washiriki.

SHIRIKA la Kivulini (Women’s Rights Organization) lenye makao yake jijini Mwanza limeadhimisha "Siku ya Mtoto wa Kike" kwa kuendesha mafunzo ya siku moja ya Sheria na Sera dhidi ya ukatili kwa wanamabadiliko kutoka kata za Nyida na Itwangi wilayani Shinyanga.


Lengo ni kuwapa washiriki uelewa kuhusu masuala mbalimbali yanayohusiana na vitendo vya ukatili na baadhi ya sheria zinazotumika katika kuwaadhibu watu wanaotenda vitendo hivyo hasa dhidi ya wanawake na watoto na mbinu watakazotumia ili waweze kuisaidia jamii iachane na vitendo vya ukatili.



Sheria zilizotolewa katika mafunzo hayo ni pamoja na Sheria ya ndoa (aina za ndoa, sifa na wajibu wa wanandoa, utaratibu wa talaka, ndoa za utotoni na madhara yake), Sheria ya Ardhi (Haki ya mwanamke kumiliki ardhi), Sheria ya makosa ya kujamiiana na Mirathi na utaratibu wa mirathi.

Washiriki wa maadhimisho hayo yaliyokwenda sambamba na mafunzo walitoka kwenye vijiji vitatu vya Nduguti, Butini na Nyida vilivyopo kwenye kata mbili za Nyida na Itwangi wilayani Shinyanga.


Ofisa mipango kutoka Shirika la Kivulini, Glory Mlaki akiwasilisha mada kwa washiriki wa mafunzo ya Sheria dhidi ya Ukatili kwa wanamabadiliko.

MADA: JINSI NA UKATILI WA KIJINSIA. 

Mwezeshaji wa kwanza, Glory Mlaki ambaye ni Ofisa mipango Shirika la Kivulini, alianza kwa kuwasilisha mada inayohusu Jinsi na Ukatili wa kijinsia ambapo washiriki wote kwa pamoja walishiriki katika kuelezea jinsi wanavyoelewa maana ya jinsi na ukatili wa kijinsia.

Katika mchango wa mawazo ya washiriiki ilibainika baadhi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia vinaendelea kufanyika kutokana na baadhi ya jamii kuendeleza kuamini mila na desturi ambazo baadhi yake zimepitwa na wakati.

Hata hivyo mwezeshaji alisema pamoja na dini kumtambua mwanamume kama kichwa na mkuu wa familia, basi ni vizuri wakatumia vyema fursa hiyo badala ya kuitumia kwa kuwatendea wanawake ama watoto vitendo vya ukatili.

Pia aliwashauri wanaume kujiepusha na tabia ya kutumia vibaya walizonazo  kwa kutoa vipigo kwa wanawake kwa kigezo tu cha kwamba wao ndiyo vichwa ndani ya familia.

Alifafanua kwamba inapotamkwa neno, Ukatili wa kijinsia haina maana ya kuwalenga wanawake au watoto peke yao bali ieleweke kuwa  wapo pia wanaume wanaotendewa vitendo vya ukatili japo baadhi yao huona aibu kulalamika hadharani.

“Kwa hali hii basi ni vizuri jamii ikatafuta suluhu nyingine ya kutatua matatizo ndani ya familia badala ya kutumia njia ya vipigo ambayo ina madhara makubwa kwa anayetendewa hii ni pamoja na akinamama kujiepusha na mazoea ya kuwachapa viboko watoto wao, maana huu nao ni ukatili,”

"Familia inayotaka kubadilika mara nyingi chanzo chake huwa ni mwanamume ambaye ndiye kichwa pale anapokubali kubadilika na hivyo kuwezesha familia kuwa salama, na itawezesha kufikiwa kwa dhana nzima ya Jamii salama, Familia Salama," alieleza Glory.

Aliendelea kufafanua kuwa daima ukatili unafanyika kijinsi, kuna wanawake pia wanafanya ukatili dhidi ya wanaume lakini pia takwimu zinaonesha wanawake ndiyo wanaoongoza kwa kutendewa ukatili na wanaume.

Hata hivyo aliwataka wanamabadiliko hao kutojaribu kujibu vitendo vya ukatili kwa kufanya ukatili badala yake wajitahidi kutoa elimu kwa jamii iweze kuacha kuwafanyia ukatili watu wengine  ama kuwaadhibu watoto wao kwa makosa ya watu wengine.

Ukatili umegawanyika katika makundi makuu manne:

1.    Ukatili wa kingono,
2.    Ukatili wa kisaikolojia
3.    Ukatili wa kimwili.
4.    Ukatili wa kiuchumi.

Aidha washiriki walihimizwa juu ya suala muhimu la kuboresha mahusiano mazuri ndani ya familia na kwamba mafunzo yoyote yanayotolewa juu ya kupiga vita vitendo vya ukatili hayana maana ya kujenga au kuleta dharau ndani ya familia au miongoni mwa wana jamii wenyewe.

SHERIA YA NDOA:

Washiriki walielimishwa kuhusiana na suala la sheria ya ndoa, aina ya ndoa, sifa na wajibu wa wanandoa, utaratibu wa taraka, ndoa za utotoni na madhara yake.

Mwezeshaji alitoa maelezo kuhusiana na ndoa ambazo zinatambulika kwa mujibu wa sheria za nchi na kwamba wanamabadiliko wana wajibu wa kuzielewa kwa ufasaha ili waweze kutatua matatizo yoyote yanayohusiana na migogoro ya ndoa yatakayojitokeza kwenye maeneo yao.

Glory aliwaelimisha washiriki juu ya maana ya dhana ya ndoa kwa kusema, Sheria ya ndoa ya mwaka 1971  katika kifungu cha 160 inaeleza juu ya mahusiano kwamba endapo mwanamke akiishi na mwanaume kwa miaka miwili au zaidi mfululizo na jamii inayowazunguka ikawatambua na kuwapa hadhi ya mume na mke, basi mahusiano hayo yaweza kupata dhana ya kuchukuliwa kama wanandoa.

Aidha washiriki walikiri kuwepo kwa tatizo la ndoa za utotoni huko katika vijiji vyao ambapo wameshauriwa kuzipiga vita na badala yake wahakikishe watu wanaofunga ndoa ni wale waliofikia umri wa utu uzima wenye umri wa miaka 18.

Hata hivyo Glory alisema sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kuna ibara inayotoa ruhusa kwa mtoto wa kike chini ya miaka 18 kuweza kuolewa kwa ridhaa ya mahakama au wazazi.

Kumaliza migogoro ndani ya familia, mfano kuacha kumshitaki mtu aliyempa mimba mtoto wa kike chini ya miaka 18, ambapo matokeo yake wazazi hufika sehemu wakakubaliana kwamba iwapo muhusika atafungwa basi mtoto wa kike atakapojifungua atakosa mtu wa kumtunza.  Kutokana na hali hiyo wawili hao huruhusiwa kuishi kama mume na mke japokuwa ndoa hiyo huwa haina ridhaa ya wanaooana. 

Washiriki walielezwa ni muhimu wao kama wanamabadiliko wakaelewa madhara yanayowapata watoto wadogo wanaoozeshwa au kubeba mimba wakiwa na umri mdogo moja ya madhara wanayoyapata ni ugonjwa hatari wa Fistula.

"Mtoto anayeozeshwa au kupata mimba akiwa na umri mdogo anapoteza haki ya kikatiba ya kupata elimu tofauti na mtoto wa kiume aliyempa mimba hiyo ambaye yeye huendelea na masomo bila tatizo, lakini pia baadae watoto hao hukumbwa na gurudumu la umasikini," alieleza Glory.

Aliongeza kueleza kuwa ni muhimu kwa wanamabadiliko kuyazingatia hayo sambamba na kuwajali watoto wao wa kike kwa vile kuruhusu kuolewa wakiwa na umri mdogo madhara mengine wanayoyapata ni kutendewa vitendo vya ukatili kutokana na kupigwa mara kwa mara na watu wanaowaoa.

NINI KIFANYIKE KATIKA KUKABILIANA NA MIMBA NA NDOA ZA UTOTONI:

 1. Kukaa pamoja na familia kwa upendo na wazazi wa kiume wasione ubaya kuwaeleza watoto wa kike kwamba wanawapenda sambamba na kuwaelimisha juu ya madhara ya vitendo vya ukatili. 

2. Wanamabadiliko wawe mstari wa mbele katika kuielimisha jamii ili iweze kuachana na mila na desturi zilizopita na wakati ili kuweza kumpa mtoto wa kike fursa sawa ya kupata elimu na haki nyingine kama anavyopatiwa mtoto wa kike.

SHERIA YA ARDHI YA MWAKA 1999.

Washiriki walielezwa kuwa sheria ya ardhi imegawanyika katika makundi mawili makuu, kwanza ni sheria ya ardhi ya jumla na sheria ya ardhi ya vijiji.

Pia walifahamishwa maana ya ardhi na kwamba pamoja na uwepo wa sheria hizo bado wanawake wengi hawajapewa fursa ya kumiliki ardhi japo sheria inaruhusu. 

Kuhusu mada iliyozungumzia suala la mirathi na utaratibu wa mirathi washiriki walishauriwa kuwa makini pale wanaposhughulikia masuala ya mirathi katika maeneo yao na kwamba ni muhimu masuala haya yakashughulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi zilizopo badala ya watu baki kujiingiza kwenye kugawa mirathi.

Washiriki walielezwa sheria za mirathi zinazotambulika nchini kwa mujibu wa sheria ambazo ni pamoja na Sheria ya kimila, Sheria ya kidini na ile ya kiserikali.

Hata hivyo walisema sheria ya kidini inayotumika zaidi katika suala la mirathi ni ile inayohusu dini ya kiislamu.  Lakini pia sheria ya kimila bado ina changamoto katika ugawaji wa mirathi kutokana na kubaguliwa kwa baadhi ya watu wakiwemo mwanamke aliyefiwa na mumewe.

Baada ya mwezeshaji kukamilisha kuwasilisha mada ya Mirathi na utaratibu wa mirathi washiriki kwa pamoja walikubaliana kwenda kuihamasisha jamii ili iweze kuwa na utaratibu mzuri wakati inapotokea suala la ugawaji wa miradhi miongoni mwa wanandugu kwa kuwaelimisha wazingatie sheria za nchi zilizopo badala ya kuruhusu watu wasiohusika kuingilia kati na kupoka mali za warithi halali ambapo mara nyingi akinamama ndiyo hujikuta wakidhulumiwa. 


Katika kuhitimisha mafunzo hayo yaliyokwenda sambamba na maadhimisho ya Siku ya mtoto wa Kike duniani washiriki walifanya zoezi la kuchagua viongozi ikiwemo ujazaji wa fomu maalumu ya Usajili ya Mwanamabadiliko ambazo washiriki watakwenda kuzitumia katika vijiji vyao kwa kuwahamasisha watu wengine kujiunga na kundi la WANAMABADILIKO lengo ni kuwezesha kupatikana kwa Jamii Salama na Familia salama.



TUMEKUWEKEA HAPA PICHA ZAIDI ZA WASHIRIKI WA MAFUNZO KUTOKA KATA ZA ITWANGI NA NYIDA.

Washiriki wakiwa makini kufuatilia mada zinazowasilisha katika mafunzo.

Washiriki wakifuatilia mada kuhusu Jinsi na Ukatili wa kijinsia.

Zoezi la utambulisho, mshiriki kutoka kijiji cha Nyida Kizwalo Masesa akijitambulisha kwa wenzake.
 Mmoja wa wawezeshaji kutoka Shirika la Kivulini, Olpha Maduhu akitoa maelezo ya utangulizi kwa washiriki wa mafunzo.


Mshiriki Naomi Paulo kutoka kijiji na Kata ya Nyida  akichangia mada.

Jonathan Mlingo mshiriki kutoka kijiji cha Butini kata ya Itwangi akichangia mada kwenye kikao.

Washiriki wakiwa makini kufuatilia mafunzo.


Akina mama pia hawakuwa nyuma katika uchangiaji wa mada.  Hapa Elizabeth Mayunga kutoka kijiji cha Butini kata ya Itwangi akichangia maoni yake kwenye mada ya Jinsi na Ukatili wa kijinsia.

Hawa nao wanashauriana jambo kuhusu mada zilizowasilishwa.






Mwezeshaji akiandika hoja za washiriki.


Mariamu Petro kutoka kijiji na kata ya Nyida akinukuu mada muhimu.

Wawezeshaji kutoka Shirika la Kivulini wakijadiliana jambo, kutoka kushoto ni Eunice Mayengela,  Olpha Maduhu na Vaileth Elisa.

              Washiriki wakiwa makini katika kuchukua kumbukumbu muhimu za mafunzo.

 Mshiriki akichangia mawazo yake katika mafunzo hayo kuhusiana na mada zilizowasilishwa.





Hapa ni zoezi la kujaza fomu maalumu ya kusajili wanamabadiliko.




 MAZOEZI YA VIUNGO KWA WASHIRIKI NAYO YALIKUWA MIONGONI MWA MAFUNZO.

Hatimaye mafunzo yalifikia mwisho kwa washiriki wote kukubaliana kwenda kuyatekeleza kwa vitendo pale watakapokuwa wamerejea katika vijiji vyao ambapo mkazo uliwekwa katika kuwahamasisha watu wengine kujiunga kwenye kundi la WANAMABADILIKO.


PICHA YA PAMOJA YA WASHIRIKI NA WAWEZESHAJI KUTOKA KIVULINI.



Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top