Mbunge wa Jimbo la Kisesa wilayani Meatu mkoa wa Simiyu, Luhaga Mpina akihutubia maelfu ya wakazi wa mji wa Mwanhuzi wilayani Meatu na wanachama wa CCM katika mkutano wa hadhara uliofanyika  kwa ajili ya kumpongeza mbunge huyo kuteuliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge ya Uchumi, viwanda na biashara.aption
Meatu

MBUNGE wa Jimbo la Kisesa wilayani Meatu mkoa wa Simiyu kwa tiketi ya CCM, Luhaga Mpina amekitisa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) baada ya kupokelewa kwa maandamano makubwa ya maelfu ya wakazi wa jimbo la Meatu linaloongozwa na mbunge wa CHADEMA, Meshack Opulukwa.

Maandamano hayo yaliyoandaliwa na wakazi wa wilaya ya Meatu na wanachama wa CCM wilayani humo yalikuwa ni ya kumpongeza mbunge huyo kutokana na kuchaguliwa kwake kuwa mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya bunge ya Uchumi, viwanda na biashara ambayo yalifuatiwa na mkutano mkubwa wa hadhara mjini Mwanhuzi.

Akizungumza katika mkutano huo, Mpina alisema pamoja na kwamba yeye ni mbunge wa jimbo jirani la Kisesa lakini amekuwa akipatwa na uchungu mkubwa kuona mbunge mwenzake anayetokana na CHADEMA jinsi alivyoshindwa kuwasaidia wakazi wa jimbo lake na kwamba mpaka sasa hajatekeleza chochote katika yale aliyokuwa amewaahidi.

Alisema kazi kubwa ambayo imekuwa ikifanywa na mbunge huyo ni kusimama majukwaani na kutukana watendaji wa serikali wakiwemo madiwani wa CCM na viongozi wakuu wa chama hicho mambo ambayo hayawasaidii lolote wapiga kura wake ambapo pia amediriki kwenda kwenye jimbo la Kisesa kutoa matusi dhidi yake.

“Jamani huyu niwaeleze wazi, Opulukwa (Meshack) siyo saizi yangu kabisa, na nimfahamishe kuwa ndani ya CHADEMA nawaheshimu kidogo, John Shibuda, mwenyekiti wao Freeman Mbowe, Dkt. Wilbroad Slaa na kijana mwenzagu, Zitto Kabwe, hawa kidogo ndiyo wanaweza kunipa shida,” alisema Mpina.

Mpina alisema kutokana na hali hiyo ameona haitokuwa vyema kuwaacha wakazi wa jimbo hilo waendelee kuteseka na kuishi kama watoto wasio na mzazi na hivyo amejitahidi kufuatilia ahadi mbalimbali zilizoahidiwa na CCM wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2010 kwa lengo la kuhakikisha zote zinatekelezwa.

“Ndugu zangu wakazi wa mji wa Mwanhuzi na jimbo la Meatu, nimefurahishwa sana na mapokezi yenu mkubwa haya ya leo, kwa kweli nimeona jinsi gani ambavyo pamoja na kwamba jimbo lenu linaongozwa na mbunge wa upinzani lakini bado mna imani kubwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM),”

“Kwa hali hii nichukue fursa ya kuwaomba katika uchaguzi ujao msirudie makosa mliyoyafanya mwaka 2010 kwa kuchagua mbunge kutoka upinzani, maana kama ni joto ya jiwe tayari mmeionja, mbunge mliyemchagua mmeona wazi hafai kabisa kuwatumikia, hivyo hakikisheni mnapata mbunge mchapa kazi, na CCM itawaletea mgombea mwenye uwezo,” alisema Mpina.

Awali akizungumza katika mkutano huo mwenyekiti wa CCM wilayani Meatu, Juma Mwiburi (mzee wa jumlajumla) alisema wanachama wa CCM na wananchi wengine wa jimbo la Meatu wameamua kumpongeza Mpina kutokana na kazi nzuri anayoifanya hivi sasa ambapo amekuwa akisaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo.

“Mheshimiwa Mpina (Luhaga) leo hii tunayo furaha kubwa ya kukupongeza kwa kazi nzuri unazozifanya ikiwa ni katika utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM, na pia tunakupongeza kwa kuchaguliwa kwako kuwa mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya bunge ya uchumi, viwanda na biashara, sisi kwetu ni fahari kubwa,” alisema Mwiburi.

Hata hivyo mwenyekiti huyo alimuomba mbunge huyo kwamba mbali ya kulitumikia vyema jimbo lake la Kisesa aendelee pia kulitumikia jimbo la Meatu ili kuweza kusaidia utekelezwaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM katika jimbo hilo ambalo mbunge wake anatokana na CHADEMA na kwamba wana CCM hivi sasa wanajipanga kulikomboa.

Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top