Moja ya banda la kuuzia mbao katika eneo la Soko la Kambarage manispaa ya Shinyanga likiwa lote limeteketea kwa moto |
MOTO ambao haikufahamika mara moja chanzo chake
umeteketeza mabanda 13 ya wafanyabiashara wa mbao eneo la Soko la kata ya
Kambarage manispaa ya Shinyanga na kusababisha hasara ya mamilioni ya shilingi.
Moto huo umetokea usiku wa kuamkia Jumamosi,
Aprili 29, mwaka huu baada ya kulipuka katika moja mabanda yaliyopo katika eneo
hilo na kusambaa kwenye mabanda jirani ambapo umeteketeza tani kadhaa za mbao
za wafanyabiashara hao.
Hata hivyo juhudi zilizofanywa na askari wa
kikosi cha Zimamoto na uokozi mjini Shinyanga ziliwezesha moto huo kutoleta
madhara zaidi kutokana na eneo hilo kuwa na mabanda mengi ya wafanyabiashara wa
mbao na mashine za kuchana na kuranda mbao.
Mmoja wa mashuhuda wa moto huo ambaye ni mlinzi katika moja ya mabanda
yaliyopo katika eneo hilo, Faustine Mapuli alisema aligundua kuwepo kwa moto
kwenye moja ya mabanda wakati alipokuwa akikagua lindo lake ambapo alipiga
kelele na kuwaita wenzake walioanza kufanya juhudi za kuuzima kwa kumwagia
michanga.
Askari wa kikosi cha Zimamoto na Uokoaji mkoani Shinyanga wakifanya juhudi za kuzima moto katika mabanda ya kuuzia mbao. |
Hata hivyo alisema walipoona moto bado unazidi
kuendelea kuwaka waliamua kutumia pia maji jambo ambalo lilisababisha moto
ulipuke kwa kasi zaidi na ikawabidi kuwapigia simu waajiri wao ambao ndiyo
wamiliki wa mabanda na wao walipiga simu ofisi ya Zimamoto kuomba msaada wa
gari la kuzimia moto.
Aliendelea kueleza kuwa pamoja na kufika kwa
gari la zimamoto tayari moto ulikuwa umeishasambaa eneo la vibanda vingi na
kuteketeza kabisa mbao nyingi, mashine za kupasua na kurandia zilizokuwemo
katika vibanda hivyo.
Mmoja wa wamiliki wa mabanda hayo, Moses Mizungu alisema baada ya kupata taarifa
za kutokea kwa kwa moto katika eneo hilo mnamo saa sita usiku.
alisema baada ya kupokea taarifa hizo mara moja alipiga simu
katika ofisi za Zimamoto lakini hata hivyo alipofika eneo la tukio alikuta
tayari moto umeteketeza eneo la vibanda vingi ikiwemo mali zake zote zilizokuwa
ndani ya kibanda chake.
Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji kikiendelea na kazi. |
Kwa upande wake kamanda wa Jeshi la Zimamoto na
uokozi mkoani Shinyanga Ndeto Malisimba, ametoa lawama zake kwa walinzi wanaolinda
mabanda hayo ambao walichelewa kutoa taarifa za kuwepo kwa moto hali
iliyochangia moto uteketekeza eneo kubwa.
Malisima alisema iwapo taarifa zingetolewa
mapema huenda hasara iliyosababishwa na moto huo isingekuwa kubwa kiasi
kinachokisiwa hivi sasa kupatikana. Chanzo
cha moto huo bado kinachunguzwa.
Post a Comment