Sehemu ya Jengo la Matibabu ya nje (OPD) |
Madiwani wakiongozwa na mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu, Justine Sheka wakiwa nje ya moja ya majengo ya hospitali mipya ya wilaya. |
WANANCHI wa
Halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga wamewapongeza madiwani wa
halmashauri hiyo kutokana na kusimamia vyema miradi ya maendeleo inayotekelezwa
katika wilaya yao ikiwemo ujenzi wa hospitali ya wilaya.
Wakizungumza
na waandishi wa habari wilayani humo juzi muda mfupi mara baada ya madiwani
kukamilisha ziara ya ukaguzi wa majengo ya hospitali ya wilaya hiyo ambayo
yamekamilika kwa takribani asilimia 85, baadhi ya wananchi walisema kukamilika
kwa hospitali hiyo kutawaondolea kero ya kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma
za matibabu.
Wananchi hao
walisema kwa kipindi kirefu tangu wilaya ya Kishapu ilipoanzishwa hawakuwa na
huduma ya hospitali ya wilaya hali iliyowalazimu kusafiri zaidi ya kilometa 40
kwenda Shinyanga mjini ili kuweza kupata huduma za matibabu ya uhakika.
Mmoja wa
wananchi hao Boniface Maganga alisema kukamilika kwa ujenzi wa hospitali ya
wilaya kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na juhudi na usimamizi wa kutosha wa
madiwani wa halmashauri hiyo ya wilaya na kwamba wameonesha jinsi gani
walivyowawakilisha vizuri wapiga kura wao.
“Binafsi
nimefurahishwa sana kuona hatimae baada ya muda mfupi watu wa Kishapu tutakuwa
na hospitali yetu ya wilaya, tena ya kisasa kutokana na majengo yake yote
kujengwa kisasa, hatutalazimika tena kwenda Shinyanga au hospitali ya Kolandoto
kutafuta matibabu, kwa hili tunawapongeza madiwani wetu kwa kazi nzuri,”
alisema Maganga.
Mkazi wa
Mhunze madukani Salum Bakari alisema kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na
madiwani wao bila kujali itikadi ya vyama vyao vya siasa ni vizuri wananchi
wakawapatia kipindi kingine cha miaka mitano ili wakamilishe shughuli zote za
kimaendeleo walizozianzisha.
“Kwa kweli
madiwani wetu wameweza kufuta kabisa aibu ambayo wilaya yetu miaka ya nyuma
tuliipata baada ya kufichuliwa ufisadi wa wizi wa zaidi ya shilingi bilioni sita, walikaa
chini na kuamua kufanya kazi, kweli kazi imefanyika, na sasa Kishapu ni shapu
kwa maendeleo na siyo kwa ufisadi,” alieleza Bakari.
Kwa upande
wake mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu, Jane Mutagurwa
alisema kazi kubwa ya ujenzi wa hospitali hiyo imekamilika kwa sehemu kubwa
inatarajiwa iwapo mipango ya upatikanaji wa vifaa inaweza kuanza kutoa huduma
kwa wananchi mwanzoni mwa mwezi Julai mwaka huu.
“Mheshimiwa
mwenyekiti sehemu kubwa ya ujenzi wa hospitali yetu ya wilaya imekamilika,
majengo yaliyo tayari ni pamoja na jengo la wagonjwa wa nje (OPD) jengo la
kisasa la kujifungulia akinamama wajawazito, jengo la upasuaji, la kuhifadhia
maiti na wodi mbili za kulaza wagonjwa kwa wanawake na wanaume ambapo ujenzi
wote unatarajia kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.547,”
Hapa ni kwenye jengo la kisasa la kuhifadhia maiti |
“Kwa ujumla
ujenzi kwa asilimia kubwa umekamilika, tunachosubiri hivi sasa ni kupokea vifaa
mbalimbali ikiwemo samani na vitendea kazi katika jengo la upasuaji na
tunatarajia mambo yakienda vizuri hospitali yetu inaweza kuanza kazi mwishoni
mwa mwezi huu au mwanzoni mwa Julai, mwaka huu,” alieleza Mutagurwa.
Post a Comment