Wanachama na viongozi wa CHADEMA wakiwa nje ya Ofisi ya Kanda ya Serengeti mjini Shinyanga wakiimba wimbo maalumu kulaani tukio la kushambuliwa kwa Tundu Lissu. |
WANACHAMA wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) Kanda ya Serengeti inayojumuisha mikoa ya Simiyu, Shinyanga na Mara
wametoa tamko kulaani kitendo cha kushambuliwa kwa kupigwa risasi mbunge wa
Jimbo la Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Katika tamko lao rasmi lililosomwa mbele ya
waandishi wa habari mjini Shinyanga wanachama hao wamesema kitendo
kilichofanyika kina ishara ya kutaka kuleta machafuko na kuchafua hali ya amani
na utulivu iliyodumu kwa miaka kadhaa hapa nchini.
Walisema kitendo cha mtu asiyejulikana
kumshambulia mmoja wa viongozi wao mwandamizi ngazi ya kitaifa na akiwa pia
rais wa Chama cha wanasheria Tanganyika (TLS) kimewashitua wanachama wote wa
CHADEMA na kinastahili kulaaniwa na wapenda amani kote ulimwenguni.
Waliendelea kueleza kuwa mataifa yote
yaliyoingia machafukoni chanzo chake huwa ni kutokea kwa mtu au watu
wasiojulikana ambao huanza kuwaua watu mashuhuri katika taifa husika, na kwamba
mtu asiyejulikana ni nabii wa ghasia na mauaji makubwa kwa taifa.
“Kwa mara ya kwanza katika taifa letu, awamu
hii ya tano maarufu kama awamu ya Magufuli, tofauti na awamu zingine zote
tumepata mtu asiyejulikana anayeteka na kuua viongozi wakisiasa na watu
mashuhuri katika nyanja mbalimbali,”
“Historia
ya mtu asiyejulikana katika mataifa na jamii mbalimbali ni mbaya sana. Nchini Rwanda, kabla ya mauaji ya halaiki
yaliyopoteza uhai wa watu zaidi ya laki nane, alikuwepo mtu asiyejulikana aliua
viongozi mbalimbali akiwemo waziri mkuu wa nchi hiyo, Bi. Agathe Uwilingiyimana
mnamo Aprili 7, 1994 kabla ya vita vya wenyewe kwa wenyewe,”
“Mtu
asiyejulikana hakuishia kuua viongozi na watu mashuhuri tu alienda mbali na
kulipua ndege ya aliyekuwa rais wa Rwanda wakati huo Bw. Juvenal Habyalimana
akiwa pamoja na Rais wa Burundi Cyprian Ntaryamira Aprili 6, 1994, na baada ya
mauaji hayo hatimaye yakaripuka mauaji ya kimbari katika hiyo ya Rwanda,” ilieleza sehemu ya
tamko.
Kutokana na shambulio hilo wanachama hao
wametoa matamka kadhaa wakilitaka Jeshi la Polisi nchini kuyatekeleza na
kuliomba liache kuhadaa watanzania kuwa Tundu Lissu kapigwa risasi na mtu
asiyejulikana wakati mitandaoni kuna hadi picha za gari lililotumika
kumshambulia.
“Tunaomba
waelewe sisi wana CHADEMA hatuwaamini na zaidi tunaona wakifanyacho ni maigizo
tu, tunaamini wanajua mwanzo hadi mwisho ya kinachoendelea,”
“Tunalikumbusha
jeshi la polisi na vyombo vyake vya usalama ya kwamba sisi bado tunapenda amani ijapokuwa inaonekana wao wameichoka
amani. Na kama silaha zao zinasiku
nyingi hazifanyi kazi, tunawaomba waende Somalia wakapambane na Al-Shabab au
Syria wakapambane na Islamic State.”
Pia wanachama hao wameelezea kushangazwa kwao
na kitendo cha kushindwa kuwakamata maadui wa watu na wasiopendezwa na harakati
za Tundu Lissu (Mb) wakati yeye mwenyewe kila mara amekuwa akikamatwa na
kushitakiwa kwa kile kinachodaiwa kufanya makosa kadhaa wa kadhaa.
Tamko hilo limewaomba viongozi wa kidini,
wanasiasa wakosoaji wa serikali na watu mashuhuri wa kada mbalimbali ikiwemo
sanaa wasiogope kutoa maoni yao juu ya taifa lao hata kama watahisi maoni yao
hayatawapendeza watu wasiojulikana.
“Historia
inaonesha watu wanaojifanya hawana upande wowote wa kisiasa ndiyo huwa
waathirika wa mwanzo ghasia zikiibuka katika Taifa. Tusipowapinga na kupambana na watu
wasiojulikana mara zote taifa huingia machafukoni. Na wakati wa machafuko waathirika huwa wengi
zaidi ya hawa watakaodhuriwa na watu wasiojulikana. Hivyo tusiogope, tupambane na mtu
asiyejulikana hadi tumshinde,” tamko liliendelea kueleza.
Chama hicho kimewaomba makamanda wote wa
CHADEMA popote walipo hivi sasa wajipange kisaikolojia, kiafya na kifizikia
katika kuisimamia falsafa ya NGUVU YA UMMA.
“Niwakumbushe
tu hawajawahi kutokea watu mtu asiyejulikana akashinda falsafa yetu ya Nguvu ya
umma. Tunaamini hakuna kitakacho
tusaidia na kutuokoa dhidi ya kuuawa, kuteswa na uonevu mbalimbali zaidi ya
falsafa yetu,”
“Tujikumbushe
popote tulipo kuwa si mwenyekiti Mhe. Freeman Mbowe, si katibu mkuu, Mhe.
Vincet Mashinji atatuokoa bali mkombozi wetu ni falsafa yetu, Nguvu ya umma, ni
wakati wa kujihoji je, uko tayari kwa nguvu ya Umma? Na kama ukiona hautoshi,
nyamaza milele, ukiona unatosha jiandae kisaikolojia hadi kifizikia,” alieleza katibu CHADEMA
kanda ya Serengeti, Renatus Nzemo.
Akizungumza katika mkutano huo wa ndani wa
utoaji tamko rasmi la kulaani kitendo cha kushambuliwa kwa risasi kwa Tundu
Lissu, Mwenyekiti wa kamati ya madiwani wa CHADEMA katika kanda ya Serengeti na
diwani wa kata ya Manispaa ya Shinyanga, Emmanuel Ntobi ameiomba serikali iwapo
jeshi la polisi litashindwa, basi iombe msaada kutoka mashirika ya upelelezi
duniani wakiwemo FBI na Scotland yard.
“Tunaiomba
serikali iwapo itaona wazi Jeshi lake la polisi hapa nchini litashindwa
kuwatambua na kuwakamata watu wasiojulikana, basi wayaombe mashirika makubwa ya
kiupelelezi duniani, FBI kutoka Marekani au Scotland yard la nchini Uingereza
waje nchini wamsake huyu mtu au watu wasiojulikana,” alieleza Ntobi.
Katika hatua nyingine wanachama hao waliendesha
ibada ya maombi kwa ajili ya kumuombea kiongozi wao na mbunge wa Jimbo la
Singida Mashariki, Tundu Lissu ibada zilizoongozwa na Abel Kitalama kutoka
dhehebu la KKKT – Shinyanga, na Hamis Ngunila aliyewakilisha waumini wa
kiislamu.
PICHA ZAIDI ZA WANACHAMA WA CHADEMA WAKATI WA KUTOA TAMKO LA KULAANI KIONGOZI WAO KUSHAMBULIWA KWA RISASI NA MTU ASIYEJULIKANA.
Dua ya pamoja kabla ya utoaji wa tamko. |
Viongozi wakiwa makini wakimsikiliza katibu wa kanda CHADEMA, Renatus Nzemo (wa tatu kutoka kulia). |
Diwani wa kata ya Kitangiri manispaa ya Shinyanga, Hamisi Ngunila akiomba dua kwa niaba ya madhehebu ya kiislamu kumuombea Tundu Lissu aweze kupona mapema. |
Mmoja wa wanachama ambaye ni muumini wa madhehebu ya kikristo kutoka kanisa la KKKT, Abel Kitalama akiwaongoza wanachama wenzake katika maombi ya kumuombea Tundu Lissu. |
Wanachama na viongozi wakiwa katika maombi. |
Post a Comment