Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na abiria hao kwa mwandishi wa habari hizi, mbali ya baadhi yao kutishiwa kuwekwa ndani pia mmoja wa askari mwenye namba D. 8281 Sajenti David wa kikosi cha usalama barabarani mkoani Shinyanga aliyejaribu kukemea kitendo cha polisi wa kituo cha Nzega naye alinusurika kuwekwa ndani.
Hata hivyo kitendo hicho kimelalamikiwa vikali na abiria hao huku wakielezea kushangazwa kwao na hatua ya Jeshi la Polisi mkoani Tabora kutumia vibaya fedha za umma kwa kuamua kuongoza msafara wa kiongozi wa chama cha kisiasa kinyume na miongozo ya kiitifaki ya viongozi wa kitaifa inavyoelekeza.
Wakielezea kuhusu mkasa huo abiria hao walisema siku hiyo ya tukio mnamo saa 11 jioni wakiwa wamekaribia kuingia mjini Nzega dereva wao alipigiwa honi kali za gari la polisi lililokuwa likiongoza msafara wa katibu mkuu wa CCM Taifa, Abdulrahman Kinana lililotokea nyuma yao na kutakiwa aliegeshe pembeni kupisha msafara huo.
Walieleza baada ya dereva kuweka gari pembeni polisi wale walimfokea vikali wakidai alijaribu kuingilia msafara huo hali ambayo ingeweza kusababisha kutokea ajali ambapo hata hivyo dereva pamoja na abiria wake walipinga madai hayo kwamba hayakuwa ya ukweli wowote kwa vile isingekuwa rahisi kuvuruga msafara uliokuwa ukitokea nyuma yao.
“Siyo kweli kabisa kwamba dereva alitaka kuvuruga msafara, maana yeye alikuwa mbele, na hata madai ya kukataa kusimama alipowashiwa taa na gari la polisi hayana ukweli, maana barabara hiyo ilikuwa na vumbi jingi, haikuwa rahisi kwa dereva kuona mwanga wa taa wa gari linalotoka nyuma yake,” alieleza mmoja wa abiria.
Kwa upande wake Sajenti David alikiri kunusurika kuwekwa ndani na mmoja wa askari wa kituo cha polisi cha Nzega, aliyemtaja kuwa ni namba WP. 7333 aliyepata maelekezo kwa njia ya simu ya kiganjani kutoka kwa OCD wake baada ya WP huyo kudai yeye (sajenti David) alihamasisha abiria wafanye fujo kituoni.
“Nilishangazwa na kitendo cha askari mwenzangu kumtungia mashitaka ya uongo dereva wetu, nilijaribu kumuelewesha kwamba dereva huyo hakuwa na kosa lolote na kwamba kitendo wanachokifanya kinapingana na dhana nzima ya utawala bora, hakunielewa badala yake alitaka kuniweka ndani, niligoma na kumweleza hana uwezo huo,” alieleza Sajenti David.
Naye mtumishi mmoja wa serikali (jina tunalo) alieleza kushangazwa na hatua ya polisi kutoa ulinzi kwa kiongozi wa chama cha siasa kinyume na utaratibu wa itifaki za uongozaji wa viongozi wa serikali na kwamba hata WP aliyewakamata hakuwa muungwana kutokana na kutumia vibaya madaraka yake huku akitoa lugha chafu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Susan Kaganda alisema hakuwa na taarifa juu ya tishio la kuwekwa ndani kwa abiria hao kwa kosa la kumtetea dereva aliyedaiwa kutaka kuvuruga msafara wa katibu mkuu wa CCM wa Taifa na kuahidi kufuatilia ili kuweza kupata ukweli wake.
“Sina taarifa juu ya tishio la abiria kutaka kuwekwa ndani, nikiri tu kwamba ni kweli kiitifaki viongozi wa vyama vya kisiasa hatupasi kuwapa ulinzi katika misafara yao, labda katika mikutano ya hadhara ambako huwa tunaweka ulinzi kwa ajili ya usalama wa wananchi,”
“Hata hivyo tulipokea barua kutoka CCM wakiomba tuwapatie ulinzi, tulifanya hivyo kama walivyoomba kwa ajili ya kuongoza msafara wa katibu mkuu wa CCM Taifa aliyeko mkoani Tabora kwa ziara ya kikazi, na kuhusu malalamiko ya matumizi ya lugha chafu ya askari wetu pale Nzega nitalifanyia kazi,” alieleza Kamanda Kaganda.
Post a Comment