Katiba ya TUGHE |
RAIS Dkt. John Magufuli
amepongezwa kwa kazi kubwa anayoifanya hivi sasa hapa nchini ikiwemo kuwafukuza
kazi wafanyakazi wanaotuhumiwa kughushi vyeti vya shule na waliotumia vyeti vya
watu wengine ili kujipatia ajira.
Pongezi hizo zimetolewa na wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Tawi la Kituo cha Afya Kambarage manispaa ya Shinyanga katika uzinduzi rasmi wa Tawi la wafanyakazi katika kituo hicho cha afya.
Hata hivyo pamoja na
pongezi hizo wafanyakazi hao wamemuomba Rais Dkt. Magufuli aangalie upya uamuzi
wake wa kuwafukuza kwa kuruhusu waweze kulipwa mafao yao mbalimbali
wanayostahili akizingatia mchango mkubwa walioutoa katika ujenzi wa taifa
kipindi walichokuwa wakifanya kazi.
Katibu wa TUGHE mkoa, Tabu mambo akitoa maelekezo na maelezo muhimu kabla ya uchaguzi wa viongozi wa Tawi, kushoto ni Mwenyekiti wa kamati ya wanawake TUGHE Mkoa wa Shinyanga, Frola Magubo. |
Wakifafanua wanachama
hao walisema pamoja na kosa la wengi wao kutumia vyeti vya kidato cha nne
visivyokuwa halali au vilivyoghushiwa, lakini bado waliweza kujiendeleza
kitaaluma na kufanya vizuri na hivyo kuweza kufanya kazi zao kwa ufanisi na
weledi mkubwa katika kipindi walichokuwa kazini.
Waliendelea kufafanua
kuwa kati ya waliokumbwa na kashfa ya vyeti vya kidato cha nne ilichangiwa na
serikali yenyewe kipindi cha awamu ya nne ilipowataka watumishi wote wa umma
kuwa na kiwango cha elimu ya kidato cha nne na kushauriwa kujiendeleza hali
iliyosababisha kwa waliokosa muda wa kusoma kununua vyeti mitaani.
“Tunampongeza Rais wetu
Dkt. Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya hivi sasa kuhakikisha utendaji kazi
ndani ya serikali yake unakuwa wa ufanisi bila ya ujanja ujanja wa aina
yoyote au udanganyifu wa kitaaluma, hali itakayowezesha kila mfanyakazi
kuwa na sifa stahiki anazopaswa kuwa nazo,”
“Hata hivyo tunafikiri
ni vizuri Rais sasa atumie ubinadamu aangalie mchango uliotolewa na watumishi
hawa wa umma ambao wengi wana zaidi ya miaka 30 kazini wakiwa wamebakiza
kipindi kifupi cha kustaafu, hivyo kuwafukuza bila kuwalipa chochote ni
kutothamini mchango wao pamoja na mapungufu waliyokuwa nayo,” walieleza.
Aidha walisema pamoja
na udanganyifu wa vyeti vya kidato cha nne wengi wakiwemo walimu, wauguzi,
madaktari na madereva lakini waliweza kufanya vizuri na kuhitimu mafunzo ya
kozi zao walizosomea kwa kutumia vyeti vya kughushi na hata walipoajiriwa
walifanya kazi zao bila matatizo yoyote.
Waliendelea kueleza
hata baadhi ya viongozi wa serikali waliopo madarakani hivi sasa wakiwemo
waliofanya zoezi la uhakiki vyeti, walifundishwa na kuhitimu vizuri masomo yao
vizuri na walimu wanaodaiwa ambao leo hii wamekutwa na kosa la kughushi vyeti.
“Ni kweli ndugu zetu
hawa wana makosa, lakini pia kwa upande wa pili serikali iliyowaajiri ilikuwa
na makosa yake, maana iliridhika na vyeti walivyowasilisha wakati wa usaili
wao, hivyo ni vizuri busara ikatumika katika kuachana nao, iwaonee huruma
iwalipe mafao yao wanayostahili kwa kuzingatia kazi walizofanya ndani ya
serikali,”
“Pia tunamuomba Rais
ahakikishe zoezi hili la uhakiki wa vyeti liwe endelevu ili kuweza kuwabaini
wadanganyifu wote ambao bado wamo ndani ya ajira kwenye sekta ya umma bila
kujali wapo kundi lipi la ajira, bila kufanya hivyo itakuwa sawa na baba
anayebagua watoto ambao wote ni wake,” alieleza Anna Kasala.
Wakati huo huo Tawi
hilo la TUGHE limefanya uchaguzi wa viongozi wake wa tawi watakaoongoza kwa
kipindi cha miaka mitano ijayo ambapo Dkt. Salome Mtani alichaguliwa kuwa
mwenyekiti na katibu wa tawi ni Lazaro Joseph huku Marietha Buzwizu
akichaguliwa kuwakilisha kundi la vijana.
Wajumbe wa tawi
waliochaguliwa ni Yohana Kuzenza, Kanyala Maganga na Grace Gombanila ambapo
Bernadetha Mushi alichaguliwa kuwa mwenyekiti kamati ya wanawake tawini na
katibu wake ni Prisca Zabron huku Frida Mtungilei akichaguliwa kuwa
mwekahazina, wajumbe wake ni Matlida Grey na Anna Kasalla.
Viongozi wapya wa Tawi wakikabidhiwa vitendea kazi, katiba na kanuni ya TUGHE. |
Kwa upande wake
aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi huo, Katibu wa TUGHE mkoa, Tabu Mambo
aliyeongozana na mwenyekiti wa mkoa wa kamati ya wanawake na mjumbe wa mkutano
mkuu wa Taifa wa TUGHE, Frola Magubo aliwataka wajumbe waliochaguliwa
kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wa kuwatumikia wanachama kikamilifu.
Mambo alisema moja ya
majukumu ya Tawi la wafanyakazi sehemu za kazi, ni kutetea na kulinda ajira,
haki za wafanyakazi ikiwa ni pamoja na kujadili masharti ya utumishi kwa
wanachama wake na kuhakikisha afya na usalama wa wafanyakazi vinadumishwa
sehemu ya kazi.
Pia kuwasilisha
mikataba ya hiari katika kamati ya utendaji ya mkoa na kuiarifu kuhusu suala
lolote ambalo linaweza kusababisha mgogoro wa kikazi ikiwemo pia kutoa taarifa
mara kwa mara kwa wanachama kuhusu shughuli za Tawi kwa ujumla.
“Endapo patatotekea
mgogoro wa kikazi mahali pa kazi, Halmashauri ya Tawi itaitisha mkutano wa
wanachama wote na kama ni mahali ambapo muafaka na mwajiri umeshindikana, kura
ya maoni ya kuhusu uwezekano wa kuitisha mgogoro itapigwa,”
“Uamuzi wa kutangaza
mgogoro utahitaji theluthi mbili ya wanachama na utawasilishwa mbele ya mkoa
ili utoe kibali baada ya kushauriana na makao makuu ya chama,” alieleza katibu
Mambo.
Aliwataka wajumbe
waliochaguliwa kuhakikisha wanatetea maslahi ya wafanyakazi katika kudai haki
zao ambapo hata hivyo alisisitiza suala la kutimiza wajibu kabla ya kudai haki
na kwamba matawi ya chama sehemu ya kazi yanaundwa kwa mujibu wa sheria ya
Ajira na Mahusiano kazini ya mwaka 2004.
Katibu wa Tawi, Lazaro Joseph akitoa neno la shukrani baada ya kuchaguliwa ambapo pia alifunga rasmi kikao. |
“Kabla ya kudai haki
zetu kwanza tuhakikishe wafanyakazi wanatimiza wajibu na malengo ya mwajiri,
kisha ndipo tunadai haki, wafanyakazi wanayo haki ya kukutana na kujadili
masuala muhimu juu ya mstakabali wa maslahi yenu kazini,” alieleza Mambo.
Wanachama wa Tawi la TUGHE Kituo cha Afya Kambarage wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wapya wa Tawi lao wakiwemo viongozi wa TUGHE mkoa waliosimamia uchaguzi. |
Post a Comment