Wazazi nchini Zimbabwe ambao hawawezi
kugharimia karo ya shule wanaweza kupeleka mifugo wao kama mbuzi na kondoo kama
malipo, waziri mmoja amesema.
Waziri wa elimu nchini Lazarus Dokora aliliambia
gazeti la Sunday Mail kuwa itabidi shule zilegeze masharti yao ya kudai karo ya
shule kutoka kwa wazazi, na pia kando na mifugo wanaweza kukubali kupewa huduma
na ujuzi kama malipo.
"Ikiwa kuna mwashi au mjenzi katika jamii,
yeye yuapaswa kupewa ile nafasi ya kufanya kazi kama njia ya kulipa karo,"
gazeti lilimnukuu.
Kuna shule ambazo tayari zimekubali kupokea mifugo kama
malipo, Sunday Mail linasema.
Hata hivyo afisa katika wizara hiyo alifafanua
kwamba wazazi ambao wanaweza kulipia watoto wao karo kwa mifugo ni wale wa
mashambani, lakini wazazi walioko mijini wanaweza kulipa kutumia njia nyingine
kama vile kuifanyia shule kazi fulani.
Tangazo hilo lilitolewa baada ya Zimbabwe wiki
jana kupendekeza watu waruhusiwe kutumia mifugo yao kama mbuzi, ng'ombe na
kondoo kama rehani wanapochukua mikopo katika benki.
Katika sheria mpya iliyopelekwa bungeni wiki
hii, wanaohitaji kuchukua mkopo wanaruhusiwa kuandikisha mali inazohamishika
ikiwemo magari na mashine kama dhamana, ripoti ya BBC World Business ilisema.
Mitandao ya kijamii ilichukulia habari ya
"mbuzi-kwa-karo" na kejeli na ucheshi.
Mwandishi Zimbabwe Tsitsi Dangarembga aliuliza
katika mtandao wa kijamii, Twitter, "kama tungeambiwa mwaka wa 1970 kuwa
tunapigania kutumiwa kwa ng'ombe na mbuzi kama pesa, tungekubali kupigania
uhuru?"
Mmoja wa watumizi wa mtandao wa kijamii Twitter
alisema - Ikizingatiwa kuwa sio wanyama wote waliozaliwa sawa - je "naweza
pata kazi kama mkaguzi wa mbuzi?"
Chanzo: BBC
News.
Post a Comment