MFANYABIASHARA MAARUFU JIJINI DAR, YUSUF MANJI NA WENZAKE WATATU WAACHIWA HURU.
Mfanyabiashara Yusuf Manji na wenzake watatu
waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa kukutwa wakiwa na mabunda
35 ya vitambaa vinavyotumika kutengeneza sare za Jeshi la Wananchi wa
Tanzania(JWTZ) zenye thamani ya Sh milioni 192.5 wameachiwa huru baada ya kesi
yao kufutwa na Mahakama ya Kisutu. Kesi hiyo imefutwa baada ya Mkurugenzi wa
Mashtaka(DPP) kusema hana nia ya kuendelea na kesi hiyo.
KWA NINI MANJI ALIKAMATWA? - Soma habari za kukamatwa kwake hapa:
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam
limethibitisha kumshikilia mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji kwa
mahojiano baada ya kukutwa na jora 43 za sare za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ) pamoja na mihuri 39 ya kampuni tofauti tofauti.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kaimu Kamanda
wa Polisi Kanda Maalumu, Lucas Mkondya alisema Manji anashikiliwa na jeshi hilo
tangu Julai mosi baada ya kukutwa na vitu hivyo katika ghala lake la Quality
Motors, lililopo Chang’ombe jijini Dar es Salaam.
“Ni kweli tunamshikilia tangu Jumamosi
tunaendelea kumhoji kwa vitu alivyokutwa navyo ili atuambie alivipataje na
anavyo kwa madhumuni gani wakati yeye sio mwanajeshi na amekaa navyo kwake,”
alieleza Mkondya.
Akizungumzia endapo Manji atafikishwa
mahakamani baada ya mahojiano, Kaimu Kamanda Mkondya alisema baada ya
kukamilisha mahojiano na kupata taarifa kamili, wataangalia kama atapelekwa
mahakamani kutokana na majibu yake. “Tunasubiri tumalize mahojiano tupate na
maelezo yake ili tuone yamekwendaje na kama atafikishwa mahakamani kulingana na
mahojiano yatakavyokwenda,” aliongeza Mkondya.
Hii siyo mara ya kwanza kwa Manji kushikiliwa
na jeshi hilo kwa mahojiano. Februari mwaka huu, Manji aliyekuwa Ofisa Mtendaji
Mkuu wa Quality Group kabla ya kustaafu Julai mwaka jana, alishikiliwa kwa
mahojiano baada ya kudaiwa kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya.
Katika hatua nyingine, Manji na wenzake
wamepeleka maombi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kuomba Jeshi la Polisi
kuwaachia huru kwa kuwa wanashikiliwa isivyo halali kwa tuhuma zinazohusiana na
sare za JWTZ.
Aidha, wameomba mahakama itoe amri kwa jeshi
hilo kuwataka wawapeleke waombaji mahakamani washughulikiwe kwa mujibu wa
sheria. Mbali na Manji, waombaji wengine katika kesi hiyo ni Deogratius Kisinda
na Thobias Fwere ambao wamewasilisha maombi hayo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali (AG), Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) na Mkuu wa Upelelezi Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam (ZCO).
Katika hati ya kiapo iliyoungwa mkono na maombi
hayo, Wakili wa washitakiwa, Hudson Ndusyepo alidai walalamikaji walikamatwa na
kushikiliwa na ZCO kwa nyakati tofauti; Kisinda alikamatwa Juni 30, mwaka huu
saa 10 jioni wakati Manji na Fwere walikamatwa Julai mosi saa 5 katika Jengo la
Quality Center, Barabara ya Nyerere.
Ndusyepo alidai kuwa tangu siku hiyo mpaka
sasa, walalamikaji wanashikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi na kwamba
alifahamishwa na ZCO kuwa walikamatwa kwa tuhuma za kutenda kosa linalohusiana
na sare zilizokutwa kwenye stoo ya Quality Motors Limited. Pia alidai baada ya
kukamatwa kwa walalamikaji hao, aliwaombea dhamana, lakini maombi hayo
yalikataliwa kwa sababu zisizojulikana ambapo walikuwa wakifuatilia dhamana za
waombaji tangu walipokamatwa.
Chanzo: Habari Leo
Post a Comment