Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Agape Aids Control Programe, John Myola akitoa maelezo kuhusu shughuli za shirika lake mbele ya madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba - Singida.

Makao makuu ya Halmashauri ya wilaya ya Iramba mkoani Singida.
SHIRIKA la Agape Aids Control Programe la mkoani Shinyanga limefungua ofisi yake ndogo wilayani Iramba mkoani Singida kwa ajili ya kupanua wigo wa huduma zake kwa jamii.


Ofisi hiyo imefunguliwa katika makao makuu ya wilaya ya Iramba, kata ya Kiomboi ambapo mkurugenzi mtendaji wa Agape, John Myola na timu yake walipata nafasi ya kujitambulisha rasmi katika kikao cha
Baraza la madiwani kilichofanyika Mei 17, mwaka huu mjini Kiomboi.

Katika kutambulisha shughuli zinazoendeshwa na Agape, Myola alisema miongoni mwa miradi inayotekelezwa na shirika ni mradi wa kuzuia mimba na ndoa za utotoni ambao kwa kipindi kifupi umeonesha mafanikio mkoani Shinyanga.

Alisema kupitia mradi huo mkoa wa Shinyanga hivi sasa umekuwa miongoni mwa mikoa nchini inayofanya vizuri katika suala zima la elimu sambamba na kupunguza asilimia ya matukio ya mimba na ndoa za utotoni kutoka asilimia 59 hadi asilimia 34.

“Kutokana na mafanikio ambayo tumeisha yapata, tulikaa na kushauriana kuona jinsi gani tutaongeza wigo wa shughuli zetu katika maeneo mengine nchini ambapo eneo la kwanza tulilochagua ni Halmashauri ya wilaya ya Iramba,”

“Katika tafiti zetu tumeona baadhi ya maeneo ya Halmashauri ya wilaya ya Iramba yanashabihiana na mkoa wa Shinyanga kwa kuwa na changamoto ya matukio ya mimba na ndoa za utotoni hasa katika kata ambazo wakazi wake wanajishughulisha zaidi na shughuli za kiufugaji,” alieleza Myola.

Alisema wameamua kufika mbele ya baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba ili kuomba ridhaa ya madiwani ambao ndiyo wenye watu katika maeneo yao hivyo ndiyo wenye jukumu la kutoa baraka zao na shirika kuweza kufanya kazi pamoja nao.

Kwa upande wake Ofisa mipango wa Agape, Peter Aman alisema mbali ya shirika kushughulikia suala la kupiga mimba na ndoa za utotoni lakini pia hujishughulisha na uboreshaji wa mifumo ya elimu kwa kujenga mahusiano kati ya mwalimu na mwanafunzi, mwalimu na mzazi na mzazi na mwanafunzi.

“Kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita shirika limekuwa na mafanikio ya kuridhisha ambapo limefanikiwa kuanzisha shule inayoitwa Agape Knowledge school, ambayo shuleni watoto waliokatishwa masomo yao kutokana na mimba na ndoa za utotoni hupata nafasi ya kuendelea na masomo yao,,”

“Kwa mwaka jana tulikuwa na mabinti 29 waliohitimu kidato cha nne na wote walifanya vizuri katika mitihani yao ya mwisho, tunaamini mbeleni watakuwa zao zuri la taasisi yetu, lakini pia kwa miaka 10 iliyopita tumeweza kusaidia watoto yatima 1,800,” alieleza Aman.

Aman alizitaja kata sita zilizochaguliwa kuwa za kwanza ambazo shirika litaendesha shughuli zake kuwa ni pamoja na kata ya Kiomboi, Kidalu, Ntulya, Ntwike, Mgongo na Mtekente ambazo zimeteuliwa kutokana na changamoto zilizopo kwenye kata hizo.

Kwa upande wao madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba walilipokea rasmi shirika hilo na kutoa ruhusa ya kufanya kazi zake katika halmashauri hiyo.

Hata hivyo hata hivyo madiwani hao walishauri na kupendekeza kupanuliwa kwa wigo wa shughuli za shirika ili liweze kufanya kazi kwenye kata zote 20 za halmashauri hiyo ambazo takribani zote zina changamoto zinazofanana.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo ya wilaya, Simon Tyosela alisema amefurahishwa na uamuzi wa Agape kuichagua halmashauri hiyo kuwa moja ya eneo lake la kazi na kwamba kwa upande wao watakuwa kutoa ushirikiano wa karibu pale watakapohitajika.

“Waheshimiwa madiwani nyote nyuso zenu zinaonesha hali ya furaha, ni wazi mmewapokea, tunawakaribisha, hata hivyo tunaomba mara baada ya kumaliza kata sita mlizochagua kuanza nazo, basi muongeze na kata nyingine, sisi tunakutakieni kila la kheri chapeni kazi, tutawapa ushirikiano,” alieleza Tyosela.

TUMEKUWEKEA HAPA PICHA ZAIDI ZA UTAMBULISHO WA SHIRIKA LA AGAPE KWENYE KIKAO CHA BARAZA LA MADIWANI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA IRAMBA.

Mratibu wa miradi kutoka Agape, Peter Aman akitoa maelezo mbele ya madiwani ya jinsi shirika lake litakavyotekeleza shughuli zake katika halmashauri ya wilaya ya Iramba.
Mkurugenzi wa Agape, John Myola (kushoto) akifuatilia maelezo ya meneja mradi wake.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba, Simon Tyosela (katikati) akisikiliza maelezo ya shughuli za Agape, kushoto kwake ni mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Iramba, Linno Mwageni na kulia ni makamu mwenyekiti wa halmashauri.
John Myola akisisitiza jambo mbele ya madiwani
Meneja miradi akimwaga sera mbele ya madiwani





Madiwani na wataalamu wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba wakifuatilia maelezo yanayotolewa na watendaji wa Shirika la Agape.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Iramba, Simon Tyosela akionesha kufurahia maelezo yanayotolewa na mkurugenzi wa shirika la Agape.


Mmoja wa madiwani akiuliza swali la ufafanuzi kuhusu shughuli za Agape.
 
Mkurugenzi wa Agape na meneja miradi wakiteta jambo la mratibu wa NGO's katika halmashauri ya wilaya ya Iramba, Romwald Mwendi (katikati)
Mkurugenzi wa Agape na meneja mradi wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya madiwani.
 PICHA ZA ENEO AMBALO OFISI NDOGO YA AGAPE WILAYANI IRAMBA IMEFUNGULIWA.





Huduma ya vinywaji tayari sasa inapatikana katika ofisi za Agape Iramba

                 KWA HABARI KAMILI KUHUSU SHIRIKA LA AGAPE INGIA HAPA:

www.agapeacp.or.tz
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Post a Comment

 
Top