Hoja 22 za kupinga vifungu Muswada wa Sheria ya
Makosa ya Mtandao wa mwaka 2015 zilizotolewa bungeni na Mbunge wa Singida
Mashariki (Chadema), Tundu Lissu zilisababisha kikao cha 14 cha Bunge
kuvunja rekodi ya kutumia muda mrefu baada ya kumalizika saa 6.15 usiku.
Marekebisho
yaliyowasilishwa na Lissu yaliungwa mkono na Mbunge wa Ubungo (Chadema), John
Mnyika ambaye pia alikuwa na marekebisho yake katika muswada huo, hivyo wote
wawili kuichachafya Serikali bila mafanikio baada ya muswada huo kupitishwa kwa
sauti kubwa ya “Ndiyooo” ya wabunge wa CCM.
Kuanzia saa 12.30
jioni, Bunge lilikaa kama kamati kupitisha muswada huo baada ya kumaliza
kuupitisha muswada wa Sheria ya Miamala ya Kielektroniki ambao haukuwa na
mvutano mkali.
Mvutano wa
kisheria kati ya Lissu dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George
Masaju, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa,
naibu wake, January Makamba ulianza saa 12.30 jioni hadi saa 5.30 usiku na
baadaye Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akatumia muda uliosalia kuahirisha Bunge.
Mpaka inafika saa
5.00 usiku wabunge wa upinzani waliokuwapo bungeni walikuwa 12 tu, akiwamo
Lissu na Mnyika na hivyo kufanya idadi ya wabunge wote kuwa 86, wakiwamo wa CCM
na mawaziri.
Kuna wakati Mbunge
wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge alilazimika kusimama kutoa ufafanuzi
wa kina, ikiwa ni pamoja na namna ya kuvitamka kwa ufasaha vifungu vya sheria
ili kukubalika na pande mbili zilizokuwa zinavutana.
Mapendekezo yote
yaliyotolewa na Chenge ambaye amewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
yaliungwa mkono na Lissu pamoja na Masaju na Wizara ya Mawasiliano.
Wakati mnyukano
huo ukiendelea, Pinda alikuwa kimya akisubiri kusoma hotuba yake ya kuahirisha
Bunge.
Pinda alianza
kusoma hotuba hiyo saa 5.30 usiku mpaka saa 6.00 usiku, ikiwa ni baada ya Bunge
kuupitisha muswada huo. Baada ya dakika 15 za kutoa matangazo mbalimbali na
kuwashukuru wabunge, Spika Makinda aliahirisha mkutano huo.
Kuna wakati Lissu
aliwataka wabunge kutochoka kutokana na hoja anazozitoa kusababisha kikao hicho
kuwa kirefu, huku Makinda naye akiwaeleza wabunge kuwa ‘zege halilali’,
akimaanisha kuwa Bunge haliwezi kuahirishwa mpaka muswada huo upitishwe na
Pinda atoe hotuba ya kuahirisha Bunge.
Kati ya
marekebisho 22 yaliyowasilishwa na Lissu, ni matano tu yaliyokubaliwa na
Serikali huku Lissu akikubali vifungu viwili tu vilivyofanyiwa marekebisho na
Serikali, akivisifia kuwa vimeandikwa kama sheria inavyotaka, lakini vingine
akiviita vya ovyo na sheria inayotungwa ni mbaya yenye malengo ya kuwakomoa
baadhi ya watu.
Hoja kubwa
iliyozua mabishano ya kisheria ni muswada huo kutokuwa na tafsiri ya baadhi ya
maneno yakiwamo, ‘matumizi ya mfumo wa kompyuta kinyume cha sheria’, ponografia
ambayo yanatengeneza kosa kwa mujibu wa sheria hiyo.
Vilevile, ulitokea
ubishi katika hoja ya kuingilia mawasiliano kinyume cha sheria ambacho adhabu
yake ni kifungo kisichopungua mwaka mmoja au faini isiyopungua Sh5 milioni,
ikipendekezwa kuwa yaingizwe maneno ‘kwa nia mbaya au kwa makusudi’, ili
kuwalenga wenye nia ovu na kuwaacha wale watakaoingilia mawasiliano kwa bahati
mbaya.
Mbunge huyo wa
Singida Mashariki alikipinga kifungu cha 14 kinachozuia utazamaji wa filamu za
ngono, akitaka kifutwe chote kwa maelezo kuwa kinawazuia watu wazima kutizama
filamu hizo, isipokuwa kwa watoto.
“Filamu hizi
zinaonyeshwa katika majumba ya sinema na hii ni biashara halali. Kifungu hiki
kinasema ukionyesha hiyo filamu ukikutwa unatozwa faini Sh30 milioni au kifungo
cha miaka 10,” alisema Lissu na kufafanua kuwa sheria hiyo inalenga kuwageuza
Watanzania kuwa watawa na mapadri na si kupiga marufuku makosa ya mtandao.
Hoja ya Lissu
ilitolewa ufafanuzi na Profesa Mbarawa, Makamba na Masaju, huku Lissu
akisisitiza kuwa neno ‘ponographia’ halijatolewa ufafanuzi katika sheria,
lakini ilipingwa na kifungu hicho kupitishwa.
Lissu pia alipinga
kifungu cha 19 kinachozungumzia mauaji ya kimbari akitaka kifutwe kwa maelezo
kuwa muswada huo haujaeleza mauaji ya kimbari ni kitu gani.
Source: Mwananchi
Post a Comment