Khamis Mgeja katika moja ya mikutano ya kampeni kipindi cha uchaguzi mkuu - 2015.




MMOJA  wa makada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na aliyewahi kuwa mwenyekiti wa CCM mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja amewaomba watanzania kumsamehe mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA Taifa, Edward Lowassa kwa kushindwa kuwatembelea kutokana na kuwa katika kifungo cha kisiasa.





Akizungumza kwa na wanachama wa CHADEMA wa kata ya Tumbi manispaa ya Tabora, Mgeja alisema baadhi ya watanzania wengi hivi sasa wanamlaumu, Lowassa kwa kushindwa kuwatembelea na kufanya mikutano ya hadhara na kuhisi ameanza kufilisika kisiasa hivi sasa.



Edward Lowassa - Waziri mkuu mstaafu ambaye hivi sasa ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA Taifa

Mgeja alisema ukimya wa Lowassa na viongozi wengine wa vyama vya upinzani nchini unachangiwa kwa kiasi kikubwa na maamuzi ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na CCM chini ya Rais Dkt. John Magufuli kupiga marufuku mikutano yote ya hadhara ya wanasiasa.

Khamis Mgeja akisisitiza jambo katika moja ya vikao vya CHADEMA.

“Binafsi naomba niwatake radhi watanzania wenye mapenzi na imani ya mheshimiwa Lowassa (Edward) ambaye hivi sasa ameshindwa kukutana na wananchi na kuwahutubia kupitia mikutano ya hadhara kwa lengo la kuwahabarisha mambo mbalimbali yanayohusiana na mstakabali wa kisiasa hapa nchini,”



“Zuio la mikutano ya kisiasa lililotolewa na Rais Dkt. Magufuli limesababisha Lowassa ashindwe kwenda kuwashukuru watanzania zaidi ya milioni sita waliokuwa wamempiga kura katika uchaguzi mkuu uliopita, nawaomba watanzania wamsamehe kwa vile ameshindwa kutokana na kifungo hicho cha kisiasa,” alieleza Mgeja.



Alisema pamoja na kifungo hicho ambacho ni kuminya uhuru wa kidemokrasia nchini bado Lowassa ana imani kubwa na watanzania na alipenda kutembea nchi nzima kuwashukuru kwa heshima kubwa waliyoionesha kwake na vyama vya upinzani kupitia umoja wao wa UKAWA.



“Binafsi naamini mheshimiwa Lowassa kamwe hatochoka kuwasemea wananchi kuhusiana na kero zinazowakabili katika maeneo yao na anaamini viongozi wa serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. Magufuli watazisikia na kuzifanyia kazi,”


“Vyama vya upinzani vilivyopo chini ya UKAWA vinapenda kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo mengi hapa nchini kwa lengo la kukutana na wananchi kusikiliza kero zao na kukosoa pale ambapo serikali inaonekana kushindwa kutekeleza wajibu wake, lakini kifungo cha kisiasa kinavizuia kutekeleza haki yao ya kidemokrasia,” alieleza.



Kwa upande mwingine Mgeja alieleza masikitiko yake kuona wakati serikali imevizuia vyama vya siasa kufanya mikutano ya kisiasa chama tawala kinatumia mlango wa nyuma kuendesha siasa katika maeneo mbalimbali kwa kisingizio ni mikutano inayohutubiwa na viongozi wa kiserikali.



“Kinachofanyika hivi sasa ni viongozi wa CCM kuendelea na siasa, wanajificha nyuma ya migongo ya watendaji wa serikali, mfano kuambatana na wakuu wa mikoa, wilaya na wakati mwingine wanaambatana na waziri mkuu au misafari ya Rais mwenyewe, huko wanafanya siasa,”



“Ukweli hali hii inaonesha wazi kwamba kama taifa hivi sasa tumefikia pabaya kwa mstakabali wa nchi yetu, na tusipokuwa makini ipo hatari ya kutokea mgawanyiko miongoni mwa watanzania, nafikiri ni wakati muafaka wa kuliombea taifa letu ili lirudi kwenye hali yake ya zamani,” alieleza Mgeja.

Hata hivyo Mgeja aliwaomba watanzania kuunga mkono mabadiliko chini ya UKAWA kwani yana manufaa makubwa  kwa wananchi bila ya kukata tamaa na wawe wajasiri kudai haki zao za msingi.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top