Wakazi wa kata ya Mwakitolyo wakiwa na nyuso za furaha wakimpongeza mbunge wao kutokana na kutekeleza ahadi zake. |
WAKAZI wa kata ya Mwakitolyo wilayani Shinyanga
wamempongeza mbunge wa Jimbo la Solwa, Ahmed Salum (CCM) kwa jinsi
anavyotekeleza ahadi mbalimbali alizoahidi kipindi cha kampeni za uchaguzi mkuu
wa mwaka 2015 ikiwemo kuwaondolea kero ya miundombinu mibovu ya barabara.
Pongezi za wakazi hao zimetolewa mwishoni mwa
wiki iliyopita katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kitongoji cha
Mahiga ambako mbunge huyo alisikiliza malalamiko ya wachimbaji wadogo wa
dhahabu waliopewa siku saba na mkuu wa mkoa, Zainab Telack wawe wameondoka ili
kumpisha mwekezaji wa kichina.
Wakizungumza katika mkutano huo wakazi hao
walielezea kuridhishwa na kazi zinazotekelezwa na mbunge wao hivi sasa na
kwamba katika kipindi chake cha ubunge amefanya kazi kubwa katika kuwatatulia
kero ya barabar a zilizokuwambovu na kuwezesha zipitike kwa urahisi tofauti na
ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Walisema miaka ya nyuma kata yao ilikuwa
ikigeuka kisiwa nyakati za masika kutokana na kutokuwepo kwa barabara imara
zinazopitika kwa kipindi cha mwaka mzima hali ambayo hivi sasa imebaki kuwa
historia kutokana na kutengenezwa kwa barabara nyingi imara ndani ya kipindi
cha miaka 10 iliyopita.
Mmoja wa viongozi wa chama katika kata ya Mwakitolyo akitoa salaam kwa niaba ya wananchi. |
Mbunge Ahmed (katikati mwenye maiki) akiwahutubia wananchi wa Mwakitolyo. |
“Kwa kweli tuna kila sababu ya kukupongeza
mheshimiwa mbunge, umetufanyia mambo makubwa sisi watu wa Mwakitolyo, leo hii
tunaweza kufanya mawasiliano na maeneo mengine kipindi chote cha mwaka tofauti
na ilivyokuwa miaka ya nyuma, wasafiri wanaotaka kwenda jijini Mwanza au
wilayani Kahama hawalazimiki tena kupitia Shinyanga mjini tena,”
“Pia jimbo letu linaongoza kwa kuwa na magari
mengi ya wagonjwa (Ambulance) ikilinganishwa na maeneo mengine mkoani Shinyanga,
karibu kila zahanati kuna gari la wagonjwa, umeme tunaona juhudi zako, maeneo mengi tayari
kazi ya upelekaji umeme wa REA inaendelea, lakini pia usambazaji wa maji kutoka
Ziwa Victoria unaendelea katika vijiji vingi vya jimbo letu, tunakupongeza,”
alieleza Shija Malisha.
Hata hivyo kwa upande mwingine wananchi hao
walilalamikia tabia ya baadhi ya watendaji wa serikali ikiwemo ofisa mtendaji
wa kata (WEO) ya Mwakitolyo kuwabughudhi kwa vitisho mbalimbali ikiwemo kuunga
mkono agizo la wao kutakiwa kuondoka katika maeneo yao kwa lengo la kumpisha
mwekezaji.
“Tunashukuru kwa uamuzi wa kututaka tusiondoke
katika maeneo yetu mpaka pale Rais Dkt. John
Magufuli atakapotoa ufafanuzi juu ya kauli yake aliyoitoa hapo awali
alipoagiza tusifukuzwe kwenye maeneo yetu, lakini tunaomba kama inawezekana leo
hii uondoke na mtendaji wetu wa kata, huyu ni jipu maana ni moja ya kero hapa
kwetu,”
“Tunasema ni jipu kwa sababu mara nyingi ana
tabia ya kumkumbatia mwekezaji wa kichina,
na ukimuona tu amekwenda kwenye ofisi zake, basi akirudi ni kututaka tuondoke
hapa, na kweli maana sasa hata mkuu wa mkoa naye ameungana naye na alitoa siku
saba tuwe tumeondoka, tunakushukuru kwa kusema tusiondoke,” alieleza Mary
Maganga.
Sehemu ya wachimbaji wadogo wakimpongeza kwa mbali mbunge Ahmed. |
Kwa upande wake mbunge Salum alisema ana
uhakika mpaka ifikapo mwaka 2020 vijiji vyote katika Jimbo la Solwa vitakuwa
vimepata umeme kupitia mradi wa umeme vijijini (REA) na kwamba ni wakati
muafaka kwa wakazi wa wilaya hiyo kujiandaa kutumia fursa hiyo kwa kuanzisha
miradi midogomidogo ya uzalishaji mali.
Alisema kwa mwaka 2017 tayari kazi ya upelekaji
umeme katika vijiji vitatu itakamilika
na baada ya vijiji hivyo kazi hiyo itaendelea kufanyika katika vijiji 50 na
inatarajiwa ifikapo mwishoni mwa mwaka 2020 vijiji vyote vya Jimbo la Solwa
vitakuwa vimepatiwa huduma ya umeme.
“Ndugu zangu ninachowaomba kwa upande wenu
ungeni mkono juhudi hizi kwa kuanzisha miradi midogo midogo ya uzalishaji mali
ili umeme usiwe mapambo bali utumieni kuwaingizia kipato na pia jengeni nyumba
bora. Juu ya suala la maji, ninyi
wenyewe ni mashahidi, kazi inaendelea katika maeneo mengi,”
“Naamini baada ya kipindi kifupi kijacho kero
ya maji kwa watu wa Jimbo la Solwa itakuwa ni historia, lakini pia kuhusu
barabara vimebaki vijiji vichache sana ambavyo havijapata barabara za uhakika,
nawaahidi pia kero hiyo itamalizika kabla ya mwaka 2020. Niwaombe wale mlioko kwenye uchimbaji mdogo
jiungeni kwenye vikundi mpatiwe hatimiliki,” alieleza.
Kwa upande mwingine Salum alimwagiza mwenyekiti
wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Mboje Ngassa kushughulikia malalamiko
yaliyotolewa na wananchi dhidi ya mtendaji wa kata (WEO) wa Mwakitolyo
anayedaiwa kuwabughudhi wananchi ambapo alikemea tabia ya watendaji
kuwabughudhi wananchi ambao ndiyo waajiri wao wakuu.
Post a Comment