BAADHI ya wanachama wa Chama cha Mapinduzi
(CCM) mkoani Shinyanga wamelalamikia maamuzi yaliyotolewa hivi karibuni na Halmashauri
Kuu ya CCM Taifa (NEC) ya kuwapa onyo kali wana CCM waliotuhumiwa kwa vitendo
vya usaliti badala ya kuwafukuza kama ilivyopendekezwa na vikao vya wilaya na
mkoa.
Baadhi ya wanachama ambao ni viongozi wa ngazi za matawi, kata, wilaya na mkoa wa Shinyanga wakimsikiliza Naibu Katibu mkuu wa CCM Bara, Rodrick Mpogolo. |
Malalamiko hayo yametolewa mbele ya Naibu
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Rodrick Mpogolo alipokuwa
akizungumza na wajumbe wa sekretarieti za CCM ngazi ya matawi, kata, wilaya na
mkoa wa Shinyanga akiwa katika ziara ya siku moja mkoani humo.
Akifafanua kuhusu kitendo cha kutofukuzwa kwa
baadhi ya wasaliti wa chama, katibu mwenezi wa CCM wilayani Kahama, Masudi
Melimeli aliyehoji kitendo cha kutofukuzwa uanachama kwa mwenyekiti wa Umoja wa
wanawake wa CCM (UWT) Aoko Nyangusu aliyebainika kwa ushahidi wote kwamba
alifanya usaliti kipindi cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
“Ndugu Naibu katibu mkuu, tunashukuru kwa maelezo
yako mazuri kuhusiana na suala zima la mageuzi yaliyofanyika ndani ya chama
chetu, lakini hata hivyo sisi hapa
Shinyanga tumesikitishwa na kitendo cha halmashauri kuu ya Taifa, kushindwa
kuwachukulia hatua za kuwafukuza ndani ya chama wanachama waliobainika
kutusaliti,
“Kweli chama kimefukuza baadhi ya wasaliti
waliothibitika kutusaliti kipindi cha uchaguzi mkuu, lakini inavyoonekana bado
mmeacha mizizi yao imebaki ndani ya chama, kule Kahama yupo mwenyekiti wa UWT
wilaya, Aoko Nyangusu, huyu vikao vya wilaya na mkoa vilipendekeza afukuzwe
uanachama, lakini tumeshangaa kusikia amepewa onyo kali,” alieleza.
Viongozi na makada wa CCM wakifuatilia hotuba ya Naibu Katibu mkuu wa CCM bara. |
Alisema kuachwa kwa mwenyekiti huyo
kutasababisha wana CCM wengine waendelee kuumia na kuteseka kutokana na vitendo
vyake anavyovifanya ambapo pia alisema huko nyuma aliwahi kupewa onyo kali
pamoja na aliyekuwa mwenyekiti wa CCM, Khamis Mgeja lakini wameshangaa kuona ameachwa
tena.
“Ndugu naibu, ukweli ukitaka kufukuza mwehu
basi lazima umfukuze na makopo kopo yake, hivi sasa amepewa karipio kali bado
ameendelea kutamba kwamba hakuna mtu atakayemuweza, kwa madai anafanya kazi
maalumu, hatujaridhishwa na hali hii japokuwa tunaheshimu maamuzi ya vikao vya
juu na sisi tunamwachia mungu,” alieleza Melimeli.
Akijibu malalamiko hayo, Naibu katibu mkuu wa
CCM, Mpogolo alisema vikao vya juu havijapuuza maazimio au ushauri uliotolewa
na wilaya na mkoa kwani kila ngazi ilipewa mamlaka yake na kwamba maamuzi ya
Halmashauri kuu ya Taifa katika kutathimini na kutafakari maamuzi ya mkoa
iliona watu hawa wapewe adhabu anayostahili ni kupewa onyo kali.
Hata hivyo alisema maamuzi hayo hayazuii
halmashauri kuu ya wilaya ama mkoa kuendelea kufuatilia nyenendo na maadili ya
mwanachama huyo na iwapo itabainika anaendelea na vitendo vya usaliti dhidi ya
chama basi hatua dhidi yake zichukuliwe.
“Naamini kamati ya siasa ya mkoa, katibu wa
chama na kamati yake ya siasa ya wilaya wanao wajibu wa kufuatilia shughuli za
kila siku za chama katika wilaya ya Kahama, kama mwanachama huyo aliyepewa
adhabu ya onyo kali na anaendelea kukiuka maadili ya chama, lazima adhabu
iendelee kuchukuliwa dhidi yake,” alieleza Mpogolo.
Katika hatua nyingine wanachama wa Chama cha
Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga wamepongezwa kwa kazi kubwa waliyoifanya kipindi
cha uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 iliyowezesha wagombea wa chama hicho katika ngazi ya
udiwani, ubunge na urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuibuka na ushindi
mkubwa.
Mpogolo alisema mkoa wa Shinyanga ni miongoni
mwa mikoa iliyomchagua kwa kura nyingi mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Magufuli ambapo kitaifa ulishika nafasi
ya tano kwa mikoa iliyotoa kura nyingi za urais na wa kwanza kwa mikoa ya kanda
ya Ziwa.
“Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 tulishinda
kwa sababu wananchi walituamini, tulinadi ilani ya uchaguzi na kuonesha matendo
mema ndiyo maana wananchi waliamua kuchagua Chama cha Mapinduzi, kazi hii
lazima iendelezwe maana tunapomaliza uchaguzi mmoja hapohapo tunaanza
maandalizi ya uchaguzi ujao,”
“Niwakumbushe kwenye mikoa bora, mkoa wa Shinyanga
upo katika tano bota, mmefanya kazi kubwa kukiletea chama chetu ushindi, kwa
hili niwapongeze wana Shinyanga, maana kwenye uchaguzi mkuu uliopita 2015
tulishinda kwa kiwango kikubwa kwa nafasi za udiwani, ubunge na urais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alieleza Mpogolo.
Kwa upande mwingine Mpogolo aliwaomba wanachama
wa CCM wakubali kuyapokea mabadiliko yaliyofanyika hivi karibuni ndani ya chama
chao na kwamba mabadiliko hayo yamelenga kukiimarisha chama na kukiwezesha kuwa
kipya kama lengo la serikali ya awamu ya tano ya kuifanya Tanzania kuwa mpya.
Alisema halmashauri kuu ya Taifa (NEC)
iliyofanyika mwezi Desemba mwaka jana ilipitisha mabadiliko na mageuzi ndani ya
Chama cha Mapinduzi kwa lengo la kukiimarisha katika ngazi ya mashina na matawi
na kukifanya kiendelee kukubalika na watanzania wengi.
“Jambo kubwa lililonileta hapa kwenu na
kuhimiza suala la uimarishaji chama chetu ngazi ya mashina na matawi, na hii
lazima tuelewe ili uweze kuimarisha mashina na matawi lazima kwanza uanze
kufanya mageuzi kwa mwanachama mmoja mmoja,”
“Chama chetu hakiwezi kuwa na nguvu kama
hakitoi taswira nzuri kwa watu wanaoongozwa, kwa hiyo mageuzi yanayozungumzwa
yanakwenda kuwagusa wana CCM wenyewe, msingi mkubwa ni wana CCM wenyewe
kukubali kubadilika,” alieleza Mpogolo.
Akifafanua alisema wana CCM mmoja mmoja
wakiweza kufanya mageuzi ni wazi CCM itaimarika na kuwa na nguvu kubwa na
itaendelea kutawala nchi hii kwa kipindi kirefu kwa vile hakuna mtu atakayeweza
kukiondoa madarakani.
Hata hivyo aliwakemea wana CCM ambao bado wana
mawazo mawazo ya ki-UKAWA na kuwataka wasahau UKAWA kwa vile hivi sasa
umeishasambaratishwa na hauna nguvu zozote na hivi sasa wafuasi wake wamejawa
na hasira kutokana na kutopata ushindi.
“Raha ya CCM ni ushindi, na ninyi viongozi wa
Shinyanga mnajua mlikuwa na wenzenu kule nyuma, wakaamua kwenda kule kwingine,
je, leo hii wana furaha? hawana, na hawana la kufanya, hii ni kwa vile uamuzi
wao haukuwa wa busara,”
“Nawapongezeni wana CCM wa Shinyanga, CCM
itaendelea kuwa imara na hakuna mtu wa kuiondoa madarakani, CCM ina historia na
mizizi yake na wapo wazee walioianzisha na hivi sasa wametukabidhi sisi,
tunaendelea nayo, tunasonga mbele hakuna wa kurudi nyuma, kama bado kuna mwenye
mawazo hayo, afanye mageuzi aambatane na CCM,” alieleza.
Hata hivyo naibu katibu mkuu huyo aliwaomba
wana CCM kusimama imara na kufanya kazi ya kukijenga chama chao bila ya baadhi
yao kutegeana na kwamba iwapo watafanya hivyo ipo hatari ya chama hicho
kutetereka na kuwaomba kila mmoja atimize wajibu wake katika eneo lake.
Pia alitoa wito kwa watendaji wote wa ngazi ya
wilaya na mkoa kuachana na utamaduni wa kukaa maofisini na badala yake watoke
wawafuate wanachama matawini ambako watakuwa na fursa nzuri ya kukiimarisha
chama sambamba na uimarishaji wa mashina ambako ndiko kwenye wanachama.
Wajumbe wa kamati ya siasa ya mkoa wakimsikiliza kwa makani Naibu katibu mkuu wa CCM bara. |
Kwa upande wao baadhi ya wanachama hao
walionesha hofu yao kutokana na mabadiliko yaliyofanyika ikiwemo kufuta baadhi
ya nafasi muhimu ikiwemo ile ya makatibu wasaidizi na wale wa Uchumi, mipango
na fedha na kwamba hatua hiyo inaweza kusababisha mdodoro wa kiuchumi ndani ya
chama.
"Binafsi sipingani na mabadiliko yaliyofanyika, lakini hofu yangu ni iwapo hayataathiri hali ya uchumi ndani ya chama chetu, hasa pale ilipoamriwa kuondolewa kwa nafasi za makatibu wa uchumi na fedha ngazi ya mikoa na wilaya na makatibu wasaidizi, naamini hatua hii inaweza ikatuathiri kimapato," alieleza Hassan Mwendapole.
Wanachama wa CCM wakitoa maoni na ushauri wao mbele ya Naibu katibu mkuu wa CCM Bara, Rodrick Mpogolo |
Akijibu hoja hiyo, Mpogolo alisema mabadiliko
yanayolengwa ikiwemo kupunguza baadhi ya nafasi za kiuongozi yanakusudia
kuimarisha zaidi ngazi ya matawi na mashina na kwamba hakuna sababu za wana CCM
kuwa na hofu juu ya mabadiliko hayo kwa vile yamefanyika kwa umakini mkubwa.
End.
Post a Comment