HATIMAYE Mahakama ya wilaya ya
Shinyanga imetoa hukumu yake kuhusiana na kesi iliyokuwa imefunguliwa na kundi
moja la wanachama lililojiita Stand United Kampuni likiomba kumilikishwa timu
hiyo kutoka mikononi mwa kundi lingine la wanachama wa Stand United.
Katika hukumu hiyo iliyotolewa na Hakimu mkazi Evodia Kyaruzi, alisema baada ya kupitia maelezo ya pande zote
mbili mahakama hiyo imetupilia mbali pingamizi lililofunguliwa na upande wa
walalamikaji (Stand kampuni) na kuamua timu hiyo iendelee kumilikiwa na
wanachama wenyewe.
Kyaruzi alisema kutokana na hali hiyo
timu hiyo itaendelea kuwa chini ya wanachama wenyewe kwa kutumia jina lake
lilelile la Stand United Football Club na kubariki rasmi uongozi uliokuwa
umechaguliwa na wanachama wenyewe chini ya menyekiti wao, Dkt. Ellyson Maeja na
kwamba wanachama ndiyo watakaokuwa na sauti ya mwisho kuhusiana na uendeshwaji
wake.
Mwenyekiti wa timu ya Stand United F.C Dkt. Ellyson Maeja |
Akizungumza baada ya kutolewa kwa
hukumu hiyo, mwenyekiti wa timu ya Stand United F.C, Dkt. Ellyson Maeja
alielezea kufurahishwa na jinsi mahakama ilivyotenda haki ambapo alisema kazi
kubwa iliyopo mbele yake hivi sasa ni kurejesha umoja na mshikamano miongoni
mwa wanachama.
Alisema hakuna sababu ya wanachama
wa Stand F.C kuendeleza mgogoro
uliokuwepo na badala yake waungane kuwa kitu kimoja ili kuijenga timu yao kwa
kujitolea kwa hali na mali ikiwemo kutafuta wafadhili watakaosaidia ili
iendelee kufanya vizuri katika Ligi Kuu ya Vodacom hapa nchini.
“Nimefurahi kwa jinsi mahakama yetu ilivyotenda haki,
tunamshukuru mwenyezi mungu kuona suala hili leo (jana) limemalizika, ukweli
sisi viongozi tuliochaguliwa na wanachama tulikuwa na wakati mgumu muda mfupi
baada ya kuchaguliwa kwetu, tulipambana na changamoto nyingi ikiwemo kuwekewa
pingamizi hili mahakamani,”
“Kwa hali hii nawaomba wanachama na
wapenzi wote wa Stand United F.C tuungane na kuwa kitu kimoja ili kuiendeleza
timu yetu, ambayo kwa sasa ni ya sita katika msimamo wa ligi, tutafute
wafadhili wa kutusaidia ili tuijenge kwa ajili ya msimu ujao iwe imara iweze
kutwaa taji la ubingwa badala ya timu kubwa za Simba na Yanga zilizozoeleka,”
alieleza Maeja.
Wachezaji wa timu ya Stand United wakishangilia ushindi kati ya mechi zao walizoshinda. |
Maeja aliendelea kueleza kuwa hivi
sasa wanakaribisha wafadhili wenye mapenzi watakaotaka kuisaidia timu hiyo na
kwamba wanachama wako tayari kukubali timu iitwe jina lolote ikiwa chini yao
ili mradi iendelee kufanya vizuri katika medani ya mchezo wa mpira wa miguu
hapa nchini.
Post a Comment