Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Ally Rufunga akifungua rasmi Mamlaka ya Mji mdogo wa Kishapu. |
Hili ndilo jiwe la uzinduzi wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kishapu |
Bendera ya Taifa na ile ya Mji Mdogo zikipepea katika uwanja wa sherehe. |
Kaimu Katibu Ofisa Mtendaji wa Mamlaka ya Mji mdogo Pharles Mahushi akionesha kwa wananchi hati rasmi ya uzinduzi. |
"Hongera sana kijana wangu" Ndivyo anavyoelekea kusema mkuu wa mkoa wa Shinyanga alipokuwa akimpongeza Kaimu Ofisa Mtendaji wa Mamlaka ya Mji mdogo. |
Wananchi wa mji wa Mhunze ambayo ndiyo makao makuu ya Mamlaka ya Mji mdogo wakishuhudia sherehe za uzinduzi katika viwanja vya SHIRECU. |
Hawa nao walikuwepo kwa ajili ya kutoa burudani. |
HATIMAYE Mamlaka ya Mji mdogo wa Kishapu wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga imeanzishwa rasmi baada ya kukaa katika mchakato kwa miaka 10 sasa tangu ilipotangazwa na serikali.
Pamoja na serikali kutangaza kuanzishwa kwa Mamlaka hiyo katika gazeti lake namba 353 mnamo Septemba 17, 2004 sambamba na mamlaka nyingine 90 nchini lakini haikuweza kuanza kufanya kazi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kigezo cha kuanza kujitegemea yenyewe bila kutegemea fedha za halmashauri mama.
Akizindua rasmi mamlaka hiyo, mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Ally Rufunga aliwapongeza wakazi wa mji wa Kishapu kwa kufanikiwa kuanza kwa mamlaka yao ambapo aliwataka kuhakikisha wanauboresha mji wa Mhunze ambao ndiyo makao makuu ya mamlaka hiyo ili ulingane na hadhi uliyopewa.
Rufunga alisema ni vizuri watendaji na wakazi wa mamlaka hiyo wakazingatia suala la usafi wa mazingira kwa kuboresha majengo yote ambayo yamejengwa kwa mfumo wa matembe ili yawe ya kisasa na kwamba wakifanya vizuri ni wazi hawatachelewa kupata mamlaka kamili ya mji.
“Tunakupongezeni kwa kufanikiwa kuanza rasmi kwa mamlaka ya mji mdogo, lakini kuzinduliwa kwa mamlaka hii kuziwabweteshe ni lazima sasa muhakikishe mji wenu unakwenda sambamba na kiwango cha mji mdogo, suala la matembe sasa muachane nalo,”
“Lakini pia wakati mkijipanga kuanza shughuli zenu kamilisheni changamoto zote zilizokuwepo ikiwemo suala la kufahamika rasmi kwa mipaka ya eneo la mji mdogo hii ni pamoja na suala la kuboresha usafi na utunzaji wa mazingira, ni wazi kupitia kuanza mamlaka hii hata hali yenu ya maisha itapanda,” alieleza Rufunga.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja aliwapongeza wakazi wa mji huo ambapo alisema kuanzishwa kwa mamlaka hiyo kunaonesha jinsi gani serikali ya awamu ya nne ya CCM inavyowajali wananchi wake na inavyotekeleza ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2010.
“Ndugu zangu pamoja na kuwapongezeni kwa kupata mamlaka ya mji mdogo, lakini ni lazima tukiri ukweli kwamba mafanikio haya yamepatikana kutokana na sera nzuri za CCM, tuliahidi wakati wa kampeni mwaka 2010 moja ya mambo tutakayotekeleza ni kuboresha na kusogeza karibu huduma za kijamii kwa wananchi,”
“Serikali ya CCM imefanya mambo mengi kwa ajili ya maendeleo kwa wananchi wake japokuwa wapo wanaotubeza kwamba hatujafanya lolote na badala yake wakiendelea kutuporomoshea matusi, lakini ukweli unabaki palepale kwamba tumefanya mengi, ikiwemo hili la uanzishaji wa mamlaka za miji midogo nchini,” alieleza Mgeja.
Awali katika risala yake kwa mgeni rasmi, Kaimu Ofisa mtendaji wa mamlaka hiyo, Pharles Mahushi alisema mamlaka hiyo imeanzishwa ikiwa na wakazi wapatao 19,347 wanaoishi katika vitongoji 56 kwa mujibu wa sensa ya watu ya mwaka 2012 ikiwa na kata mbili za Kishapu na Mwataga.
“Ndugu mgeni rasmi, wananchi wa kata za Kishapu na Mwataga wanayofuraha kubwa kwa siku ya leo ya kuzinduliwa kwa mamlaka hii ambayo mchakato wake umetumia miaka 10 tangu utangazwe na kuzinduliwa kwake,”
“Wananchi wa mamlaka ya mji mdogo wa Kishapu wanatoa shukrani kwako wewe na serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) katika kufanikisha uanzishaji wa mamlaka hii, hii yote ni kudhihirisha nia thabiti ya serikali katika kugatua madaraka ili wananchi wake wajiletee maendeleo,” ilieleza sehemu ya risala kwa mgeni rasmi.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kishapu, Wilson Nkhambaku pamoja na kuanzishwa kwa mamlaka hiyo, serikali wilayani humo itaendelea kusimamia vipaumbele vyake sita ilivyojiwekea kwa lengo la kuwaletea maendeleo wakazi wote wa wilaya ya Kishapu.
Nkhambaku alisema wilaya ya Kishapu ilijipangia vipaumbele sita katika kuhakikisha vinasaidia kusukuma maendeleo na uchumi wa wakazi wake ikiwemo Elimu, Uchumi, Afya, miundombinu ya barabara, utunzaji wa mazingira na ulinzi na usalama.
“Mheshimiwa mgeni rasmi, ninayo furaha kukufahamisha kwamba katika kipindi kifupi cha miaka miwili iliyopita tumefanikiwa kubadili sura ya wilaya yetu ambayo huko nyuma ilichafuka kutokana na vitendo vya ubadhirifu wa fedha za wananchi,”
“Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na kuiwezesha halmashauri yetu kupata hati safi za ukaguzi kwa miaka miwili mfulululizo, lakini pia tumesimamia vyema vipaumbele vyetu tulivyojiwekea hasa katika sekta ya elimu ambako kwa miaka miwili pia tumefanya vizuri sana,” alieleza Nkhambaku.
Post a Comment