ASKOFU EDSON MWOMBEKI AKIWA OFISINI KWAKE.
Askofu Edson Mwombeki katika picha ya pamoja na mbunge wa Jimbo la Shinyanga mjini, Stephen Masele pamoja na mmoja wa vikongwe wanaotunzwa na kanisa la Tanzania Field Evangelism Shinyanga.
ASKOFU wa kanisa la Tanzania Field Evangelism la mjini Shinyanga, Edson Mwombeki amekitahadharisha Chama cha Mapinduzi (CCM) huenda kikajikuta katika wakati mgumu kwenye uchaguzi mkuu ujao kisipokemea tabia ya wabunge wake wanaotoa ahadi kwa wananchi bila ya kuzitekeleza.
 
Askofu Mwombeki alitoa tahadhari hiyo ofisini kwake ambapo alisema CCM inaweza kujikuta ikipoteza majimbo ya Shinyanga mjini na Kishapu iwapo haitawaweka kitako wabunge wake, Stephen Masele na Suleiman Nchambi kwa lengo la kuwahimiza ili watekeleze ahadi zao kwa wananchi.
 
Mbali ya tahadhari hiyo Askofu Mwombeki alisema kanisa lake halitokuwa tayari kumpigia kampeni mbunge ye yote atakayeshindwa kutekeleza ahadi zake na kusimamia vyema ilani ya uchaguzi ya chama chake huku akijipanga kurudi kugombea tena ubunge akitegemea kutumia fedha kuwarubuni wapiga kura.
 
Alisema iwapo CCM itashindwa kuwarekebisha wabunge hao kwa kuhakikisha wanatimiza ahadi walizozitoa kwa wananchi kanisa lake litasimama kidete kuwahimiza wananchi katika majimbo yao wasiwachague tena kwa vile watakuwa wameonesha wazi kugombea kwao awali haikuwa kwa ajili ya maslahi ya wananchi bali kutafuta maslahi yao binafsi.
 
Akimzungumzia mbunge wa jimbo la Shinyanga mjini Askofu huyo alisema mara baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo alitoa ahadi nyingi ambazo kwa sehemu kubwa ameshindwa kuzitekeleza ambapo amediriki hata kulidanganya kanisa kitu ambacho hakina sura nzuri mbele za mungu.
 
Akifafanua alisema mwaka jana mmoja wa wazee vikongwe wanaotunzwa na kanisa lake alifariki dunia akiwa na zaidi ya umri wa miaka 113 huko katika kata ya Ibadakuli ambapo mbunge Masele alitoa ahadi ya kutoa msaada wa jeneza lakini jambo la ajabu hakuweza kutoa msaada huo na hivyo kanisa kulazimika kutafuta jeneza lingine kwa haraka.
 
Askofu Mwombeki aliendelea kufafanua kuwa Masele ambaye pia ni Naibu waziri wa Nishati na madini mapema mwanzoni mwa mwaka uliopita aliwathibitishia wananchi kwamba amefanya juhudi na kuhakikisha kiwanda cha nyama kilichopo Old Shinyanga kingeanza kufanya kazi na hivyo vijana wengi wangepata ajira hata hivyo mpaka sasa kiwanda hicho hakijaanza kazi.
 
“Sisi kama kanisa tunasema wazi hatuwezi kuruhusu utapeli huu uendelee, Masele amewaahidi mambo mengi wananchi wa Shinyanga lakini hakuna hata moja la maana alilotekeleza ukiachilia mbali suala la timu ya Stand United, moja ya ahadi aliyoitoa kwa vijana ni suala la kuwapatia matrekta kila kata, mpaka leo hajatoa trekta hata moja,”
 
“Huu ni mfano tu wa baadhi ya ahadi zake, lakini yapo mambo mengi aliahidi ameshindwa kuyatekeleza na kipindi ndiyo kinamalizika, sasa ni vyema asihangaike kutaka kugombea tena ubunge, maana ni wazi hawa wenzetu ni wabunge wa kujitengenezea marupurupu hawana nia kabisa ya kuwatumikia wananchi,” alieleza Askofu Mwombeki.
 
Kwa upande mwingine alielezea kushangazwa kwake na kitendo cha mbunge huyo kufunga simu zake za kiganjani hali ambayo imeongeza ugumu wa kupatikana kwake na kwamba ni rahisi kuzipata simu ya Rais Jakaya Kikweta au waziri mkuu, Mizengo Pinda kulikoni kutafuta simu ya Masele.
 
Akimzungumzia mbunge Nchambi alisema mbunge huyo ameshindwa kutekeleza kikamilifu baadhi ya ahadi zake ambapo amekuwa akitanguliza mbele mambo mengi ya mzaha ikiwemo kupokonya ardhi za wakazi wa jimbo lake kwa madai ya kutaka kuwajengea vituo vidogo vya abiria kusubiria mabasi katika njia ya Shinyanga kwenda Mwanza.
 
Alisema wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2010, Nchambi alitoa ahadi kwa wananchi wake kwamba katika kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana atajenga vituo vingi vidogo vidogo vya abiria katika barabara ya Shinyanga kwenda Mwanza na hivyo wananchi wengi walijitolea kmpatia ardhi kwa ajili ya ujenzi huo hata hivyo baada ya kushinda ubunge alivitelekeza.
 
“Huyu Nchambi amediriki hata kutaka kupokonya ardhi ya Kanisa letu, hapa tulipo tuna kesi katika Baraza la ardhi kati yetu na yeye, tulifikisha malalamiko yetu kwa Rais Jakaya Kikwete alimwita na kumtaka tuelewane, tukakaa naye akajitoa na kutuomba samahani, ajabu ametuzunguka na kumwingiza dada yake kwenye kesi hiyo, sasa huyu ni mwakilishi wa wananchi kweli?” alihoji.
 
Hata hivyo Nchambi alikanusha madai ya Askofu Mwombeki ambapo alisema yote ambayo anayazungumza mara nyingi  kwenye mikutano ya chama cha CHADEMA yana lengo la kutaka kumgombanisha na kumchafua kwa wapiga kura wake kwa vile yote hayana ukweli bali yamejaa chuki binafsi.
 
“Huyu bwana inavyoelekea kazi ya uaskofu imemshinda, na sasa anataka kujikita ndani ya siasa, sijawahi kupokonya kiwanja cha mtu wala mimi sikifahamu kiwanja anachodai cha kanisa, lakini pia viwanja vile nilivyonavyo kwa ajili ya vituo vidogo vya abiria nimekuwa navyo hata kabla ya kugombea ubunge, asidanganye watu, mbona mabaya yake hayasemi?” alihoji Nchambi.
 
Juhudi za kumpata Masele ziligonga mwamba kutokana na simu zake zote zinazofahamika kutokuwa hewani kipindi chote na hata pale msaidizi wake alipotumiwa maswali kwa njia ya ujumbe mfupi (sms) alihoji tu ni mtu gani aliyetuma ujumbe huo, alipoelezwa kuwa ni mwandishi hakuweza kujibu lolote.

Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top