MCHIMBAJI mdogo wa madini ya almasi katika kijiji cha Maganzo wilayani Kishapu Bernard Edward amekufa baada ya kupigwa risasi na walinzi wa Kampuni binafsi ya ulinzi ya Zeneth inayolinda mgodi wa almasi wa Williamson Diamonds Ltd ulioko Mwadui mkoani humo.



Mbali ya mchimbaji huyo pia wachimbaji wengine wawili wanahofiwa kufa ikihisiwa walidumbukia ndani ya bwawa lenye tope lililomo mgodini humo walipokuwa wakifukuzwa na walinzi wa kampuni hiyo ya ulinzi walipokurupushwa wakati wakijaribu kuiba mchanga wenye madini ya almasi.

Hali hiyo imesababisha wakazi wa kijiji cha Maganzo wakiongozwa na diwani wa kata ya Songwa, Mohamed Shabani kuvamia katika ofisi za Makao Makuu ya Polisi mkoani Shinyanga wakishinikiza kukamatwa kwa walinzi waliosababisha vifo vya wachimbaji hao baada ya tabia hiyo kuonekana kushamiri hivi sasa.

Akizungumza tukio hilo diwani huyo wa CCM alilaumu vikali kitendo cha walinzi wa mgodi huo kuwashambulia kila mara kwa silaha za moto wachimbaji wadogo maarufu kwa jina la “wabeshi” wanaodaiwa kuvamia mgodini kwa lengo la kupora mchanga wa almasi kwa vile kitendo hicho kinapingana na sheria za nchi.

“Hatuungi mkono kitendo cha  wachimbaji kuvamia ndani ya mgodi kwa lengo la kupora mchanga wenye madini ya almasi, tunachopinga ni tabia ya walinzi kujichukulia sheria mkononi kwa kuwapiga risasi, tabia hii sasa inaelekea kuzoeleka kwani zaidi ya vijana 10 wameishashambuliwa kwa risasi wengine wakipoteza maisha au kupata vilema vya maisha,”

“Inasikitisha sana, lakini tumebaini vitendo hivi vinaungwa mkono na viongozi wetu wa serikali ngazi ya mkoa na wilaya, kila tunapowalalamikia wao wanasema hawa vijana waache kuvamia mali za watu vinginevyo wataendelea kufa, majibu haya hayastahili kutolewa na viongozi wenye dhamana ya kuongoza wananchi, walipaswa kutafuta ufumbuzi wa tatizo,” alieleza Shabani.

Shabani alisema wachimbaji wadogo wanalazimika kuvamia eneo hilo la mgodi kutokana na serikali kushindwa kuwatengea maeneo watakayofanya shughuli zao na kwamba eneo lililowahi kutengwa kwa ajili yao lililopo kijiji cha Maganzo limebainika kutokuwa madini ya kutosha ni kame halina maji kwa ajili ya kusafishia madini hayo.

Mke wa marehemu Edward, Mwajuma Nasibu alisema mumewe alifariki juzi akiwa anapatiwa matibabu katika hospitali ya Kolandoto manispaa ya Shinyanga baada ya kupigwa risasi na walinzi wa kampuni ya Zeneth Septemba 24, mwaka huu na kwamba alipofanyiwa upasuaji kwa ajili ya uchunguzi alikutwa na goroli 30 za risasi aina ya Shortgun.

“Siku ya Alhamisi saa 1.00 usiku nilipigiwa simu nikitakiwa kwenda kituo kidogo cha polisi cha Maganzo ambako nilimkuta mume wangu akiwa amejeruhiwa kwa kupigwa risasi walipokuwa mgodini, wakati huo alikuwa akitapika mabonge ya damu,”

“Tulimchukua na kumpeleka katika hospitali ya Kolandoto alikopatiwa matibabu lakini alifariki siku ya pili yake wakati akiendelea kupatiwa matibabu, baada ya kufariki alipelekwa mjini Shinyanga katika hospitali ya serikali kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi ili kubaini kilichosababisha kifo chake na kuelezwa kilitokana na kupigwa risasi,”  alieleza Mwajuma.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Mussa Taibu alikiri kutokea kwa tukio hilo na kwamba mpaka hivi sasa wanamshikilia mlinzi anayetuhumiwa kuwafyatulia risasi wachimbaji hao kwa ajili ya uchunguzi zaidi ambapo hata hivyo alikemea kitendo cha wachimbaji wadogo kuvamia mara kwa mara katika mgodi huo.

“Tuna taarifa za kifo cha mchimbaji huyo, lakini siyo kweli alikutwa na goroli za risasi 30, ni goroli moja tu iliyokutwa mwilini mwake, tunawaomba wenzetu waache tabia ya kuvamia kwenye huo mgodi, maana sheria namba 18 vifungu (a) mpaka (c) ya kanuni za adhabu inaruhusu mtu kuua pale anapojihami au kuzuia kuibwa kwa mali yake,” alieleza Taibu.

Kamanda Taibu alimtaja mlinzi anayeshikiliwa kuwa ni Juma Masanja (38) ambapo pia amekiri mmoja wa wachimbaji hao kufia ndani ya bwawa lenye tope alipokuwa akijaribu kuwakimbia walinzi wa mgodi huo na kwamba mchimbaji wa pili aliwahi kutoroka alipokuwa akikimbizwa na kueleza kuwa uchunguzi zaidi juu ya tukio hilo unaendelea.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top