SERIKALI inakusudia kuzifanyia ukarabati mkubwa barabara muhimu zilizopo katika jimbo la Ushetu wilayani Kahama mkoani Shinyanga ili kuwaondolea wananchi kero ya ukosefu wa mawasiliano ya uhakika ya barabara.


Hali hiyo imebainishwa na Naibu waziri wa ujenzi nchini, ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Ushetu, Elias Kwandikwa wakati akijibu hoja za wananchi baada ya kukagua maeneo korofi ya barabara  katika jimbo lake.

Naibu waziri huyo amesema mbali ya kuondoa kero ya ubovu wa barabara pia serikali ya awamu ya tano imejipanga kuhakikisha wananchi wake wanapatiwa huduma zote muhimu ikiwemo huduma za matibabu, maji safi na salama, na umeme.

“Niwaomba ndugu zangu sasa badilikeni anzeni kutumia fursa ambazo zinaletwa na serikali yenu ya awamu ya tano ambayo imedhamiria kwa dhati kuleta mageuzi ya kweli katika taifa letu, tunaposema suala la huduma tunamaanisha Tanzania mpya,” alieleza Kwandikwa.

Awali baadhi ya wakazi wa kata za Ushetu, Ulewe na Chambo wilayani Kahama akiwemo diwani, Kulwa Emmanuel wa kata ya Ulewe, walimuomba waziri huyo awatatulie kero ya ubovu wa barabara katika maeneo yao inayochangia washindwe kufanya shughuli za kimaendeleo.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Ulewe, Kulwa Emmanuel alisema ujenzi wa daraja katika barabara kuu iliyopo katika kijiji cha Ulewe, kati ya vijiji vya Ulewe, Nyankende na Ubagwe umesaidia mawasiliano ya uhakika kwa wakazi wa kata yake.

Sisi kama kijiji cha Chambo tuna shida kubwa ya barabara ambayo ni kiungo muhimu na maeneo mengine katika mkoa wa Shinyanga, Tabora na Mwanza ambayo kwa sasa imechakaa, ni barabara ya kihistoria, ni vyema ifanyiwe ukarabati mkubwa ili ipanue fursa kwa watu wanaojiajiri,” alieleza Bethod John.

Katika hatua nyingine, Naibu waziri alipata fursa ya kutembelea shule mpya ya msingi Nonwe iliyopo kata ya Ushetu iliyojengwa kwa fedha za maendeleo kutoka halmashauri ya Ushetu ambayo ilitokana na ongezeko kubwa la wanafunzi katika shule mama ya Nonwe baada ya kusajili watoto 800 wa darasa la kwanza.

"Tuliamua kujenga shule hii ili kuwasaidia watoto waliokuwa wakisoma shule ya msingi ya Nonwe ambapo katika mwaka 2016 iliandikisha watoto 800 wa darasa la kwanza, hali iliyotushitua na kuona kuna umuhimu wa kujenga shule mpya mbadala ili kunusuru msongomano wa wanafunzi kwenye shule mama," alieleza Kwandikwa.


TUMEKUWEKEA HAPA PICHA 16 ZAIDI YA ZIARA YA NAIBU WAZIRI WA UJENZI, ELIAS KWANDIKWA KATIKA JIMBO LAKE LA USHETU.



 Naibu waziri wa Ujenzi nchini, Elias Kwandikwa akikagua kipande cha barabara iliyopo yenye urefu wa kilometa 35 kutoka upande wa mkoa wa Shinyanga kwenda Tabora ilitengenezwa wakati wa ukoloni ikiwa ni kiungo muhimu kati ya mikoa hiyo miwili.
Sehemu ya Barabara katika mpaka wa mikoa ya Shinyanga na Tabora.


Naibu waziri Kwandikwa (mwenye miwani) pia alipata fursa ya kukutana na wanafunzi waliokuwa wakiendelea na masomo ambapo kwa sehemu kubwa walisema wanaridhishwa na hali ya shule yao kuwa na mahitaji mengi muhimu ya kufundishia na kujifunzia.

Hapa anasaini kitabu cha wageni baada ya kumaliza kukagua majengo na mandhari ya shule ya msingi Nonwe, mwenye blauzi nyekundu ni mmoja wa walimu wa shule hiyo, Mary Alex na kulia ni katibu wa waziri kutoka wizarani.

HAPA NI KATIKA MKUTANO WA HADHARA ULIOFANYIKA KWENYE KATA YA CHAMBO WILAYANI KAHAMA MKOA WA SHINYANGA.







Mwanahabari kazini.

Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top