BAADHI ya wakazi wa mji wa Shinyanga
wamevilalamikia vyombo vya sheria mkoani humo kutokana na jinsi vinavyopindisha
kwa makusudi ushahidi wa kesi zinazohusiana na matukio ya ubakaji ikiwemo
kulawiti hali inayochangia kuendelea kwa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.
Hatua ya kulalamika kwa wakazi hao inatokana na
Mahakama ya wilaya ya Shinyanga kumuachia huru bila masharti mshitakiwa wa
kesi ya ubakaji Eugen Mwaluko (18) aliyekuwa ameshitakiwa kwa kosa la kumbaka
mtoto mdogo mwenye umri wa miaka tisa anayesoma darasa la tatu ambaye pia anasumbuliwa
na tatizo la ugonjwa wa kupanuka moyo.
Wakizungumza na waandishi wa habari muda
mfupi baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo wakazi hao wameelezea kutoridhishwa na
hukumu hiyo na kwamba imeonesha wazi jinsi fedha ilivyotumika ambapo walidai
kitendo cha ushahidi kutojitosheleza wakati mtoto anaonekana wazi kuharibiwa
sehemu zake za siri na kutambuliwa kwa mshitakiwa ilitosha kuwa ushahidi.
Wakazi hao walisema ongezeko la vitendo vya
kubakwa na kulawitiwa kwa watoto wadogo katika siku za hivi karibuni mkoani
humo inaonesha wazi kunatokana na vyombo vya sheria kutokutoa adhabu kwa
washitakiwa wanaokamatwa huku baadhi ya kesi nyingi zinazofikishwa mahakamani
zikichukua muda mrefu bila sababu za msingi.
Mmoja wa wakazi hao aliyejitambulisha kwa jina
la Njile Maganga mkazi wa Mwasele manispaa ya Shinyanga alisema tabia ya vyombo
vya sheria kuharibu kwa makusudi kesi zinazohusiana na masuala ya kubakwa kwa
watoto ndiyo chanzo cha mkoa wa Shinyanga kuongoza kwa matukio ya ukatili dhidi
ya watoto kwa asilimia 59.
Maganga alisema mbali ya mkoa huo kuongoza kwa
matukio ya ukatili wa kijinsia pia kwa mujibu wa utafiti ulioendeshwa na
Shirika la Kimataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) watoto 16 hubakwa kila siku
mkoani Shinyanga hali inayoonesha wazi ukubwa wa tatizo hilo la ukatili na
unyanyasaji wa jinsia mkoani humo.
“Kwa kweli binafsi nimechanganyikiwa, maana
inavyoelekea mkoa wetu sasa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinaonekana
kuwa vya kawaida, kitu ambacho ni cha hatari kwa mstakabali wa wahanga wa
matukio hayo, tulitegemea vyombo vya sheria vikomeshe hali hii, lakini na
vyenyewe inaonekana kusaidia watuhumiwa,” alieleza Maganga.
Akizungumzia kufutwa kwa kesi hiyo, baba mzazi
wa mtoto Novatus Ernest (42) mkazi wa Lubaga Farm Manispaa ya Shinyanga alisema
ameshangazwa na jinsi hukumu hiyo ilivyotolewa na kwamba imeonesha wazi
mahakama imeshindwa kumtendea haki mtoto wake.
“Kwa ujumla hivi sasa nimechanganyikiwa, maana
pamoja na mwanangu kuharibiwa sehemu zake za siri lakini bado mahakama
imemuachia huru mshitakiwa kwa madai ya kutopatikana kwa ushahidi wa
kutosheleza pamoja na mtoto mwenyewe kumtambua mshitakiwa mahakamani,”
“Hivi sasa ninajipanga kukata rufaa, na
ninaomba iwapo hapa nchini kuna wanaharakati wa kupinga ukatili dhidi ya watoto
wanisaidie, maana haki ya mtoto wangu inachezewa wakati tayari ameishaathiriwa
kisaikolojia na kuharibiwa sehemu zake za siri, ukweli haki haikutendeka,
nimeamini nilichoelezwa na baba wa mshitakiwa kuwa nitaondoka patupu,” alieleza
Novatus.
Hata hivyo kwa upande wake Hakimu mkazi wa
mahakama ya wilaya ya Shinyanga aliyesoma hukumu hiyo, Neema Gasabile
alikanusha madai ya kupindisha haki katika kesi hiyo na kwamba kuachiwa huru
kwa mshitakiwa huyo kunatokana na upande wa mashitaka kushindwa kutoa ushahidi
mahakamani hapo usioacha shaka.
“Ni kweli leo hii (jana) nimemuachia huru
mshitakiwa aliyekuwa akishitakiwa katika kesi ya jinai namba 1 ya mwaka 2015, Eugene
Mwaluko, hii ni baada ya kukosekana ushahidi unaomtia hatiani, hapakuwa na kesi
ya kulawiti bali ilikuwa ni kesi ya kawaida ya ubakaji,”
“Katika kesi hii ushahidi wa mhanga (mbakwaji)
ambao haukuwa wa kiapo kwa vile ni mtoto ulikosa ushahidi wa kuungwa mkono na
hivyo kuacha shaka kwa upande wa mahakama, lakini pia maelezo yaliyoandikwa
katika fomu namba tatu ya matibabu yalipingana na aliyotoa daktari mahakamani hapa,” alieleza
Gasabile.
Alisema baada kupingana kwa maelezo ya daktari
Dkt. Lucas aliyoyatoa mahakamani kupingana na maelezo yake ya awali kwenye fomu
namba tatu (PF.3) alipompima mtoto huyo mahakama ilishindwa kupata ukweli na
hivyo kubaki na shaka kubwa iwapo kweli mshitakiwa alitenda kosa hilo na hivyo
kumuachia huru.
Gasabile alisema hata hivyo mlalamikaji anayo
haki ya kukata rufaa iwapo anaona hajatendewa haki na kwamba daima mahakama
husimama katika kutenda haki na haiwezi kutoa adhabu kwa mshitakiwa iwapo
ushahidi uliotolewa mahamani unatia shaka.
Post a Comment