Makao Makuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Shinyanga mjini. Vijana wakionekana wamefunga lango la ofisi hizo. |
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Shinyanga mjini, Kanali mstaafu, Tajiri Maulidi, akitoa tamko mbele ya waandishi wa habari. |
Hapa wamesimama mbele ya mlango mkuu wa kuingilia katika ofisi za CCM Shinyanga mjini kuzuia mtu ye yote asiingie ndani. |
CHAMA
Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Shinyanga mjini kimelaani vikali kitendo cha
baadhi ya vijana wa Umoja wa vijana (UVCCM) kufunga ofisi za chama hicho
wakishinikiza kuondolewa madarakani kwa baadhi ya watendaji wanaowatuhumu kwa
vitendo vya usaliti. Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake, mwenyekiti wa CCM Shinyanga mjini,
Kanali Mstaafu Tajiri Maulidi alisema Chama cha Mapinduzi kimesikitishwa na
kitendo hicho na kinakusudia kuwachukulia hatua kali za kinidhamu wale wote
watakaobainika kupanga mipango hiyo ili iwe fundisho kwa wengine.
Kanali
Maulidi alisema kitendo cha vijana hao kuzifunga ofisi za chama hicho kwa muda
hiyo juzi kinakwenda kinyume na taratibu za chama kuhusiana na uwasilishaji wa
malalamiko kwa mujibu wa katiba na kanuni zilizopo zinazopaswa kufuatwa na kila
mwana CCM.
Alisema
kufuatia hali hiyo, Kamati ya siasa ya halmashauri kuu ya CCM wilaya ya Shinyanga
mjini imetoa tamko rasmi la kulaani kitendo hicho na imetoa maelekezo kwa
wanachama wote wa CCM kuheshimu katiba na kanuni za chama zilizopo pale
wanapowasilisha tuhuma zozote dhidi ya viongozi wanaowatuhumu.
“Kamati
ya Siasa ya Halmashauri kuu ya CCM wilaya iliyokutana jana (juzi) ilipokea kwa
masikitiko makubwa taarifa ya jaribio la baadhi ya vijana wa UVCCM kuhusu
kufunga ofisi ya wilaya kwa lengo la kuwazuia viongozi kuingia ofisini kutokana
na tuhuma mbalimbali wanazodai,”
“Uongozi
wa wilaya utafuatilia na kuchukua hatua kali kwa mtu ye yote aliyehusika
kupanga na kutekeleza uasi huo, aidha kamati ya siasa wilaya imeelekeza kwa
mwanachama ye yote atakayekuwa na tuhuma kwa kiongozi ye yote afuate taratibu
za kutumia vikao na si vinginevyo,” ilieleza sehemu ya tamko hilo la CCM.
Kanali
Maulidi
alisema ofisi za CCM ni taasisi ya umma na siyo za mtu binafsi hivyo
zinapaswa kuheshimiwa na hata kama kuna watendaji ambao vijana hao
hawawataki basi wangefuata taratibu za kuwasilisha malalamiko yao badala
ya
kuchukua hatua za kuhukumu moja kwa moja.
“Inawezekana
baadhi ya malalamiko yao yakawa na ukweli fulani, lakini wameyawasilisha
kinyume cha utaratibu, mambo yote ya kichama hujadiliwa na kutolewa maamuzi
ndani ya vikao, lakini hata hata hivyo tuna wasiwasi iwapo malalamiko hayo yana baraka zozote
za vikao vya kikatiba vya UVCCM, sasa huu ni uhuni,” alieleza Kanali Maulidi.
Baadhi
ya vijana wa UVCCM juzi walifunga kwa masaa kadhaa ofisi za CCM wilaya ya Shinyanga mjini
wakishinikiza kuondolewa madarakani kwa katibu wa wilaya wa chama hicho,
Charles Sangura, katibu mwenezi, Charles Shigino na katibu wa uchumi na fedha,
Ahmed Mapalala wote wakituhumiwa kukisaliti chama katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Vijana
hao wanawatuhumu viongozi hao kuchangia kwa njia moja ama nyingine kushindwa
kwa wagombea wa CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika nchini
kote Desemba 14, mwaka huu ambapo wagombea wa CHADEMA kupitia umoja wao wa
UKAWA walishinda katika mitaa 30 huku CCM ikipata mitaa 26.
Post a Comment