Mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack akihutubia mamia ya wafanyakazi wa mkoa wa Shinyanga katika sherehe za Mei Mosi - 2017. |
Filo Nchimbi
SERIKALI mkoani Shinyanga imetoa siku 14 kwa
waajiri wote katika sekta binafsi mkoani humo kuhakikisha wanatekeleza
kikamilifu Sheria ya Ajira na mahusiano kazini namba sita ya mwaka 2004
sambamba na kuwaruhusu wafanyakazi wao kujiunga na vyama huru vya wafanyakazi
wanavyovitaka.
Agizo hilo limetolewa na mkuu wa mkoa wa
Shinyanga, Zainab Telack kwenye kilele cha maadhimisho ya sikukuu ya
wafanyakazi duniani (Mei Mosi) zilizofanyika kimkoa katika kiwanja cha michezo
cha Kambarage mjini Shinyanga baada ya kupokea maandamano makubwa ya
wafanyakazi wa mkoa huo.
Wafanyakazi kutoka idara mbalimbali za serikali na sekta binafsi wakiwa katika maandamano ya Mei Mosi - 2017 |
Hatua ya mkuu huyo kutoa agizo hilo inatokana
na kilio kilichotolewa na katika risala ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi
(TUCTA) mkoani humo wakiiomba serikali iingilie kati tatizo la waajiri wengi
katika sekta binafsi ambao kwa makusudi hawataki kutekeleza kikamilifu sheria
ya ajira na mahusiano kazini.
Kutokana na hali hiyo mkuu huyo wa mkoa ametoa
siku 14 kwa kila mwajiri aliyepo katika sekta binafsi kuhakikisha anatekeleza
kikamilifu sheria hiyo kwa kuwapa wafanyakazi wao mikataba ya ajira
inayotambulika kwa mujibu wa sheria ikiwemo kuwaruhusu kujiunga na vyama vya
wafanyakazi wanavyovitaka.
Pia aliwataka waajiri hao kuhakikisha
wanapeleka michango ya wafanyakazi wao katika mifuko ya jamii ili waweze kulipwa
mafao baada ya kustaafu kazi na kwamba mwajiri anayeacha kupeleka michango hiyo
anavunja sheria na anastahili kuchukuliwa hatua za kisheria.
Wafanyakazi wakipita kwa maandamano mbele ya mgeni rasmi katika sherehe za Mei Mosi - 2017. |
“Nimeisikiliza risala yenu kwa umakini mkubwa
sana na kuzisikia changamoto zote zinazowakabili, naahidi kuzipokea na zile zinazohitaji
utatuzi wa ngazi ya kitaifa nitaziwasilisha kwa mamlaka husika ili zifanyiwe
kazi mapema iwezekanavyo, na ambazo zipo katika uwezo wa ngazi ya mkoa, wilaya
na serikali za mitaa, nitazifanyia kazi mwenyewe,”
“Hili la sekta binafsi kutotoa mikataba ya
ajira, kuwazuia wafanyakazi kutojiunga na vyama vya wafanyakazi, kutotoa hati
za malipo ya mishahara, kutolipa michango ya wafanyakazi kwenye mifuko ya
kijamii, kutotoa likizo zote za kisheria, kutozingatia masaa tisa ya muda wa kazi
kutokulipa saa za ziada na kutotoa vitendea kazi, yapo katika uwezo wa mkoa,”
alieleza Telack.
Akikifanua alisema mwajiri ye yote anayewazuia
wafanyakazi wake kujiunga na vyama vya wafanyakazi ni kinyume cha sheria ya
ajira na mahusiano kazini namba sita ya mwaka 2004 kifungu cha 9 (1) (a) na (b)
inayowapa haki watumishi kujiunga na vyama vya wafanyakazi.
“Sasa naagiza waajiri wote wa sekta binafsi
kufuata sheria za kazi na kuondoa mapungufu hayo ndani ya wiki mbili kuanzia
tarehe ya leo, ifikapo Mei 15, mwaka huu katibu tawala wa mkoa uunde timu
maalumu itakayowahusisha makatibu tawala wa wilaya na wawakilishi wa vyama vya
wafanyakazi na ofisi ya kazi mkoa,”
“Timu hii itafanya kazi ya kutembelea na
kukagua katika sekta binafsi zote zilizopo katika mkoa wetu hususani hizo
zilizotajwa hapa leo ndani ya risala ya wafanyakazi ili kuona kama zimetekeleza
agizo langu, na endapo hawatatekeleza kwa vitendo nitachukua hatua kali za
kisheria dhidi yao,” alieleza Telack.
Wawekezaji kutoka kampuni ya kichina ya Jielong pia walikuwa miongoni mwa watu walioshiriki sherehe Mei Mosi mkoani Shinyanga. |
Wafanyakazi, viongozi, waajiri na wananchi mbalimbali waliohudhuria sherehe za Mei Mosi - 2017 wakifuatilia matukio mbalimbali katika kiwanja cha michezo cha Kambarage. |
Kwa upande mwingine mkuu huyo mkoa amelitaka
Shirikisho la vyama vya wafanyakazi (TUCTA) mkoani humo kuendelea kutoa
ushirikiano chanya kwa serikali na wafanyakazi ili wafanye kazi kwa kujituma
pasipo kuendelea kufanya kazi kwa mazoea.
Pia amewataka wawaelimishe wafanyakazi waweze
kutumia muda wao mwingi katika vituo vyao vya kazi kwa lengo la kuongeza
ufanisi katika kuwatumikia wananchi sambamba na kufanya juhudi za kuongeza
idadi ya wanachama ndani ya vyama vyao na wajenge mahusiano mazuri kati yao na
waajiri.
Telack alisema kwa upande wake serikali ngazi
ya taifa, mkoa na wilaya inaendelea na jitihada za kutafuta wawekezaji wakubwa
na wadogo kutoka ndani na nje ya nchi katika sekta ya viwanda vitakavyotumia
malighafi zinazotokana na kilimo na mifugo ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa
ajira kwa wananchi wa mkoa na Taifa kwa ujumla.
Mratibu wa sherehe za Mei Mosi - 2017, Filo Nchimbi kutoka chama cha Wafanyakazi wa mawasiliano na uchukuzi (COTWU "T") akisoma risala ya wafanyakazi mbele ya mgeni rasmi. |
Awali katika risala yao kwa mgeni rasmi,
Shirikisho la vyama vya wafanyakazi mkoani humo lilipongeza utendaji kazi wa
serikali ya awamu ya tano iliyopo madarakani hivi sasa chini ya Rais Dkt. John
Magufuli ikiwemo suala la kupiga vita vitendo vya rushwa, uzembe kazini,
wafanyakazi hewa na waliofanya udanganyifu katika ajira kwa kughushi vyeti vya
shule.
Pia waliupongeza uongozi wa serikali mkoani
Shinyanga kwa hatua yake ya kusimamia suala la uboreshaji wa huduma za afya
ambazo kwa sasa zinawafikia kwa uhakika wananchi walioko maeneo ya vijijini
ambako pia wapo wafanyakazi wa kada mbalimbali za umma na sekta binafsi.
Wafanyakazi pamoja na mgeni rasmi wakishiriki kuimba kwa pamoja wimbo maarufu wa wafanyakazi ufahamikao kama "Solidarty forever" |
“Mheshimiwa mgeni rasmi, kwa heshima na
taadhima tunaungana na watanzania wote kumpongeza kwa dhati Rais wetu wa
serikali ya awamu ya tano, Dkt. John Magufuli kwa juhudi nyingi anazozifanya
katika taifa letu kwa kupambana na mambo mbalimbali kama ufisadi, watumishi
hewa, rushwa, madawa ya kulevya pamoja na vyeti feki,”
“Lakini pia tunaipongeza serikali kwa kuanzisha
mfuko wa fidia kwa wafanyakazi wote (WCF) ambapo wafanyakazi wanapopata ajali
wakiwa kazini wanalipwa fidia kupitia mfuko huo, sanjari na hilo tunaipongeza
serikali mkoani Shinyanga kusogeza
huduma za afya kwa wananchi wa vijijini,” ilieleza sehemu ya risala ya
wafanyakazi.
Pamoja na pongezi hizo risala hiyo ilielezea
changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi mkoani Shinyanga hasa wale
walioajiriwa katika sekta binafsi ambapo waliwataja kwa majina waajiri kadhaa
wanaodaiwa kutotekeleza sheria ya Ajira na Mahusiano kazini namba sita ya mwaka
2004.
“Baadhi ya waajiri wa sekta binafsi hawatoi
hati za malipo ya mshahara kwa wafanyakazi wao (salary slip), hawazingatii
masaa tisa ya kazi na muda unapozidi hawalipwi posho ya muda wa ziada
(overtime), hawalipi michango ya wafanyakazi kwenye mifuko ya jamii na
huwanyima likizo zote za kisheria,”
“Hata hivyo serikali nayo kwa upande wake
imekuwa ikikiuka mikataba ya mikopo ya elimu ya juu kwa kuwakata watumishi
asilimia 15 kinyume cha mkataba ambao unaeleza wazi kiwango cha mtumishi
kukatwa ni asilimia nane, hii ni sambamba na kodi ya mishahara kuendelea kuwa
kubwa, tunaomba serikali itupunguzie makato haya,” ileleza risala ya
wafanyakazi.
Pia palikuwepo na maonesho ya baadhi ya shughuli za wananchi. |
Michezo ya kuvuta kamba na kufukuza kuku ilikuwa sehemu ya burudani zilizokonga nyoyo za wafanyakazi katika sherehe hizo. |
Washereheshaji maarufu (MCs) Mwl. Msimbang"ombe Peter na Mwl. Tandise walikuwa makini katika kazi yao kuhakikisha mambo yote yanakwenda kama yalivyokuwa yamepangwa, |
Post a Comment