Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Justin Sheka.
Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu katika moja ya vikao vyao vya Baraza la madiwani.
Moja ya miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa wilayani Kishapu, ambayo hata hivyo kutokana na uhaba wa fedha imeshindwa kukamilika kwa wakati, hili ni moja ya Jengo katika hospitali ya wilaya ya Kishapu.

Huu ni mradi mkubwa wa ujenzi wa kituo cha kisasa cha mabasi wilayani Kishapu ambacho kitakuwa na zaidi ya vyumba 300 vya kibiashara

OFISI ya waziri mkuu imeombwa kuruhusu haraka matumizi ya fedha kiasi cha shilingi bilioni 2.1 za Halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga ili kuwezesha kutekelezwa kwa miradi kadhaa ya maendeleo katika halmashauri hiyo.
 
Hatua hiyo inafuatia malalamiko ya wakazi wa Kishapu ambao wameanza kuonesha hofu yao ya kuibwa tena kwa fedha hizo ambazo hapo awali ziliibwa na baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo ambapo benki ya National Microfinance (NMB) Tawi la Manonga Shinyanga ilikubali kuzirejesha.
 
Wananchi hao wamedai ni takribani miezi sita sasa tangu walipopewa taarifa kupitia madiwani wao kwamba baada ya juhudi kubwa waliyoifanya serikali na benki ya NMB walikubali kurejeshwa kwa fedha hizo na zilipangwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo lakini mpaka sasa hawajaona kazi yoyote ikifanyika.
 
Akizungumzia hali hiyo mbele ya waandishi wa habari, mwenyekiti wa Halmashauri hiyo ya Kishapu, Justin Sheka mbali ya kukiri kurejeshwa kwa fedha hizo aliitupia lawama ofisi ya Waziri Mkuu ambayo kwa kusema ndiyo iliyozuia matumizi yake mpaka pale itakapotoa kibali chake ili zianze kutumika.
 
“Ni kweli hata sisi hili jambo hivi sasa limetuweka katika wakati mgumu, tulijitahidi kwa kadri ya uwezo wetu na kufanikiwa kurejesha sehemu ya fedha za wananchi wetu zilizokuwa zimeibwa na baadhi ya watendaji wetu wasio waaminifu, benki ya NMB ilikubali kutulipa na tayari zipo kwenye akaunti zetu,”
 
“Fedha hizi tulizipokea Julai 15, mwaka jana ziliingizwa katika akaunti zetu kwa sharti la kutotumika kwanza mpaka pale tutakapokuwa tumeandaa bajeti ya matumizi yake na kupata ruhusa kutoka ofisi ya waziri mkuu ndipo tuanze kuzitumia, lakini leo ni zaidi ya miezi sita ruhusa hiyo haijatolewa,”
 
“Pamoja na kwamba tuliunda ujumbe maalumu kwenda kukutana na waziri mkuu, baada ya mazungumzo marefu tulielezwa turudi tukasubiri barua itakayotoa ruhusa ya kutumika kwa fedha hizo baada ya kutekeleza maelekezo yote tuliyopewa ikiwemo uandaaji wa bajeti ambayo ilipitishwa pia na uongozi wa mkoa wetu,

"Sasa tunashangaa zaidi ya miezi sita sasa hatujaruhusiwa ili tuanze kuzitumia, wananchi wetu wana matatizo mengi, ujenzi wa maabara, maji na hata madawati mashuleni, fedha zipo zimekaa tu bila ya kutumika, inashangaza, lakini pia sisi madiwani tupo katika muda wa mwisho wa kumaliza kipindi chetu hivyo inatuweka katika wakati mgumu sana,” alieleza Sheka.
 
Hata hivyo alisema huenda ucheleweshaji huo unafanywa na watendaji ndani ya ofisi ya waziri mkuu kwa lengo la kusubiri kumalizika kwa muda wa madiwani waliopo madarakani hivi sasa ili fedha hizo ziweze kutumika katika kipindi ambacho shughuli zote za halmashauri hutekelezwa chini ya watendaji wa halmashauri.
 
“Kwa kweli binafsi nina wasiwasi mkubwa kucheleweshwa huku hakuna lengo zuri hasa kwa sisi madiwani tuliopo madarakani hivi sasa, lakini uamuzi huu unaweza kuwa na madhara makubwa kwa madiwani wa CCM katika uchaguzi mkuu ujao, maana watapigwa chini baada ya wananchi kutokuona matumizi ya fedha hizo,” alieleza Sheka.
 
Kutokana na hali hiyo mwenyekiti huyo ameiomba ofisi ya waziri mkuu iharakishe kutoa ruhusa ili fedha hizo zianze kutumika katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyokuwa imepangwa ikiwemo ununuzi wa mitambo mikubwa ya kutengenezea barabara na kuchimbia visima vya maji na ujenzi wa maabara vinginevyo wananchi hawatawaelewa wawakilishi wao.
 
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top