Wajumbe wa kituo cha Taarifa na Maarifa (Mtandao wa Nyuki) kutoka kata ya Mwadui-Lohumbo wakiimba ngonjera yenye ujumbe wa changamoto mbalimbali zinazowakabili kwenye kata yao. |
Ofisa kutoka TGNP Makao Makuu, Nyanjura Kalundo akitoa maelezo kwenye kikao maalumu cha uwasilishaji wa taarifa na kuelezea changamoto zinazowakabili wakazi wa kata ya Mwadui - Lohumbo. |
Wajumbe wakifuatilia kwa makini kikao kinavyoendelea. |
WANAFUNZI wa kike katika shule za msingi na sekondari
wilayani Kishapu hupoteza siku 40 za masomo kwa kila mwaka kutokana na shule
nyingi wilayani humo kutokuwa na vyumba maalumu vya kujihifadhi pale wanapokuwa
katika siku zao.
Hali hiyo imebainishwa na wajumbe wa kituo
cha Taarifa na Maarifa kutoka kata ya Mwadui-Lohumbo wilayani Kishapu
mkoani Shinyanga kwenye kikao maalumu kilichoandaliwa na Mtandao wa Jinsia nchini - TGNP makao makuu Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili changamoto
mbalimbali zinazowakabili wakazi wa kata Mwadui-Lohumbo.
Wakisoma risala yao mbele ya mgeni rasmi, Kaimu
mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga,
George Kessy wanakituo hao walisema watoto wa kike hushindwa kuhudhuria masomo
wanapokuwa kwenye siku zao kwa hofu ya kuaibika kutokana na ukosefu wa chumba
kitakachowawezesha kujirekebisha na kujiweka katika hali ya usafi.
Walisema hali hiyo huchangia washindwe kufuatilia vyema
masomo yao na kusababisha kupata matokeo yasiyo mazuri katika mitihani yao ya
mihula na hata ile ya majaribio ambapo waliomba halmashauri ya wilaya iangalie
uwezekano wa kujenga vyumba maalumu mashuleni vitakavyotumiwa na watoto wa kike
wanapokuwa katika siku zao.
Akijibu changamoto hiyo, Ofisaelimu msingi wilayani
Kishapu, Richard Mutatina alikiri kuwepo na changamoto hiyo ambapo alisema
tayari halmashauri yake imeanza kuchukua hatua za kujenga vyumba maalumu
mashuleni kwa kushirikisha nguvu za wananchi ili kuweza kuwasaidia watoto wa
kike.
“Ni kweli watoto wengi wa kike hushindwa kuhudhuria
masomo pale wanapoingia katika siku zao, hali hii inachangiwa na kukosa eneo
maalumu la wao kujihifadhi wanapokuwa shuleni, na mara nyingi huona aibu,
takwimu zinaonesha kwa mwaka hupoteza siku 40 za masomo kutokana na kuwa katika
siku zao,”
“Hata hivyo tayari halmashauri yetu imeanza kulifanyia
kazi tatizo hili na kuangaliwa uwezekano wa kujenga chumba kimoja katika kila
shule kwa ajili ya kuwasaidia watoto hawa, tunatarajia kushirikisha pia nguvu
za wananchi ili kufanikisha ujenzi huu,” alieleza Mutatina.
Akijibu hoja ya uhaba wa vyumba vya madarasa na
ukosefu wa shule za msingi katika vijiji vya Nyenze na Mwanholo, Mutatina
alikiri kuwepo na upungufu mkubwa katika vyumba vya madarasa na madawati hali
iliyochangiwa na wazazi wengi kuitikia wito wa kupeleka watoto wao shuleni.
“Suala la upungufu wa vyumba vya madarasa na madawati
kwa sasa halipo katika kata ya Mwadui-Lohumbo pekee, ni wilaya nzima na huenda
pia ni katika maeneo mengi nchini, hii inatokana na mpango ulioanzishwa na
serikali wa elimu bure, wazazi wengi wamehamasika kupeleka watoto wao shule,”
alieleza Mutatina.
Akifafanua alisema mpaka hivi sasa wilaya ya Kishapu
ina upungufu wa vyumba vya madarasa 792 ikiwemo pia ukosefu wa nyumba za
walimu, tayari kiasi cha shilingi milioni 279.5 zimetengwa kwa mwaka huu wa
fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 33.
Pia alisema halmashauri imetenga kiasi cha shilingi
435,375,000 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa nyumba 19 za walimu ambazo
zitapunguza kwa kiasi fulani upungufu wa nyumba hizo katika baadhi ya shule za
msingi na sekondari.
“Idadi ya wanafunzi walioandikishwa ni wengi sana,
tuna wanafunzi wapya 15,000 wa darasa la kwanza, kwa upande wa madarasa ya
awali wapo wanafunzi zaidi ya 10,000 hii imechangia kujitokeza upungufu mkubwa
wa madawati, tayari tumetenga shilingi 280,000,000 kwa ajili ya kukabiliana na
upungufu wa madawati,” alieleza Mutatina.
Post a Comment