Ofisa Mthamini katika Halmashauri ya wilaya ya Kishapu, Reuben Lauwo akijibu hoja mbalimbali zilizotolewa na Kituo cha Taarifa na Maarifa (Mtandao wa Nyuki) kutoka kata ya Mwadui-Lohumbo

Wawakilishi wa kituo cha Taarifa na Maarifa kata ya Mwadui-Lohumbo wakisoma risala yao mbele ya mgeni rasmi.
 
Kaimu mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu, George Kessy akifungua kikao.

MMOJA  wa wataalamu katika halmashauri ya wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga amejikuta akipandwa na jazba na kususia kikao kilichokuwa kinajadili changamoto zinazowakabili wakazi wa kata ya Mwadui-Lohumbo wilayani humo.

Hali hiyo ilijitokeza katika kikao maalumu kilichofanyika mjini Mhunze wilayani Kishapu kilichoandaliwa na Mtandao wa Jinsia nchini – TGNP ambapo kituo cha Taarifa na Maarifa (mtandao wa nyuki) kutoka kata ya Mwadui-Lohumbo kiliwasilisha changamoto mbalimbali zinazowakabili wakazi wa kata hiyo.

Uamuzi wa mtaalamu huyo, Reuben Lauwo ambaye ni Ofisa mthamini wa wilaya ulitokana na wajumbe wa kikao hicho kumshinikiza ataje kiwango halisi cha fedha ambazo mwekezaji kampuni ya El-Hilal Mining anatakiwa kuwalipa kwa kila ekari moja wakulima wa kata ya Mwadui-Lohumbo waliochukuliwa mashamba yao.

“Mheshimiwa mwenyekiti ni kweli paliundwa tume maalumu kushughulikia mgogoro huu ambao ni wa muda mrefu, na kwenye kikao kilichowakutanisha baadhi ya wananchi, mwekezaji na watendaji wa serikali kuna kiwango mwekezaji alikubali kulipa, lakini kitaalamu mimi sipaswi kukitaja hapa,”

“Naheshimu maadili na misingi ya kazi yangu, hivyo siwezi kugeuka na kutaja kiwango hicho hali inayoweza kunisababishia matatizo hapo baadae, tusiligeuze jambo hili kuwa la kisiasa, tuheshimu sheria na taratibu za nchi zilizopo, siwezi kusema kiwango kilichotamkwa hata kama mtanilazimisha,” alieleza Lauwo.

Mtaalamu huyo aliamua kutoka ndani ya kikao baada ya kutokea hali ya kurushiana maneno kati yake na diwani wa kata ya Songwa, Abdul Mohamed ambaye alidai haoni sababu za mtaalamu huyo kushindwa kuwatamkia wananchi kiwango cha fedha kinachopaswa kulipwa kwa wakulima kwa vile mwekezaji alikitamka hadharani katika kikao kilichoshirikisha wadau wengi.
 
Diwani wa kata ya Songwa, Abul Mohamed (kulia) akifuatilia kwa makini hoja zinazowasilishwa na kituo cha Taarifa na Maarifa (Mtandao wa Nyuki) kata ya Mwadui-Lohumbo wilayani Kishapu, kushoto ni Ofisa mipango wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu.


Wajumbe wa kamati ndogo ndogo wakiwasilisha changamoto zinazowakabili katika kata ya Mwadui-Lohumbo


Awali wakiwasilisha changamoto mbalimbali zinazowakabili wakazi wa kata ya Mwadui – Lohumbo wajumbe wa kituo cha Taarifa na Maarifa katika sekta ya madini walisema pamoja na mwekezaji kampuni ya El-Hilal kuahidi kuwalipa fidia baada ya mashamba yao kuchukuliwa lakini ameshindwa kutekeleza ahadi hiyo mpaka hivi sasa.

Walisema mbali ya El-Hilal Mining pia lipo tatizo kwa mwekezaji mwingine kampuni ya Williamson Diamonds Ltd iliyopo Mwadui ambaye ameshindwa kujenga mahusiano mazuri kati yake na wanajamii wanaoishi katika vijiji vinane vinavyouzunguka mgodi huo wa almasi.

“Mheshimiwa mgeni rasmi, moja ya mambo ambayo mwekezaji kampuni ya Williamson Diamond Ltd. ameshindwa kutekeleza ni suala la utoaji ajira kwa vijana wetu, badala yake anaajiri vijana kutoka nje ya vijiji vyetu, hali hii ndiyo inayochangia baadhi kuvamia mgodini kuiba mchanga wenye madini ya almasi ili wapate fedha za kujikimu,”

“Tunachoomba ajenge mahusiano mazuri na wanajamii wanaoishi katika vijiji vinane vinavyouzunguka mgodi, tunaamini akiwa na mahusiano mazuri na kuwapatia ajira vijana wetu suala la mgodi kuvamiwa na watu wanaojiita “wabeshi” litamalizika, maana hata sisi tutakuwa walinzi awa mgodi,” alieleza Sarah Masinga mwenyekiti wa kituo.

Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa maendeleo katika halmashauri ya wilaya ya Kishapu, Reuben Kessy alisema alisema lengo la serikali kukaribisha wawekezaji ni kutaka kuinua uchumi wa taifa pamoja na wananchi wake kwa ujumla ambao husaidiwa  miradi mbalimbali ya kijamii.

“Kuna changamoto nyingi katika maeneo ya migodi hapa nchini, lakini niwaombe wananchi wajitahidi kujenga mahusiano mazuri na wawekezaji waliopo, kwa hili la Mwadui-Lohumbo nashauri zifanyike taratibu za kukaa pamoja kati ya pande mbili na kuweka mambo sawa, ikishindika basi halmashauri tushirikishwe,” alieleza Kessy.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top