MTANDAO wa Jinsia nchini (TGNP) umepongezwa kwa
kazi nzuri ya ya kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kupiga vita vitendo vya
ukatili wa kijinsia na jinsi ya kudai haki zao za msingi wanazostahili kupatiwa
ma serikali.
Pongezi hizo zimetolewa na kaimu mkurugenzi wa
Halmashauri ya wilaya ya Kishapu, George Kessy alipokuwa akifungua kikao maalum
cha utoaji taarifa na kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili wakazi wa
kata ya Mwadui-Lohumbo wilayani Kishapu kilichoandaliwa na Mtandao wa Jinsia nchini
(TGNP).
Kessy alisema juhudi zinazofanywa na Mtandao wa
Jinsia nchini zimewezesha wananchi wengi waishio vijijini kuelewa haki zao za
msingi sambamba na kupiga vita vitendo vya ukatili wa kijinsia ambapo pia
wameanza kushiriki katika shughuli za kijamii kwa hiari yao bila ya
kushurutishwa.
Baadhi ya wana kituo cha Taarifa na Maarifa pamoja na wataalamu wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu wakifuatilia kikao. |
“Nichukue fursa hii kuwapongeza wenzetu wa
Mtandao wa Jinsia - TGNP kwa kazi nzuri wanazozifanya kwa jamii ya watu wa
Kishapu katika kuwaelimisha juu ya masuala muhimu ikiwemo kutambua haki zao na
jinsi ya kuzidai kutoka kwa mamlaka husika,”
“Kazi nzuri mnazozifanya za kuwaelimisha
wananchi tayari zimeanza kuonesha matokeo chanya, hasa katika suala la wananchi
kushiriki katika mikutano ya hadhara inayojadili masuala mbalimbali ya
maendeleo katika maeneo yao, haya ni mafanikio ikilinganishwa na hapo awali,
tunakupongezeni sana,” alieleza Kessy.
Wana kituo wakionesha moja ya igizo kuhusu changamoto zilizopo kwenye zahanati zao kwenye kata ya Mwadui-Lohumbo wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga. |
Alisema kutokana na wananchi kuibua changamoto
zilizoko katika maeneo yao, serikali kwa upande wake hivi sasa imeanza kuchukua
hatua za kutatua changamoto hizo katika sekta za afya, maji, madini na kilimo
na kwamba hali hiyo huenda ingechukua muda kushughulikiwa iwapo wananchi
wasingapaza sauti zao.
Akijibu hoja ya uhaba wa vyumba vya madarasa
katika shule za msingi, Kessy alisema tayari serikali imeanza kuchukua hatua za
kukamilisha majengo yaliyoanza kujengwa kwa kushirikiana na wananchi na kwamba
halmashauri ya Kishapu imetenga kiasi cha shilingi 279,542,514 kwa ajili ya
ujenzi wa vyumba 33.
“Naamini tukishirikiana na wananchi katika
suala hili tutaweza kupunguza tatizo, kwa sasa tunawahimiza wao wajenge maboma
na halmashauri itafanya kazi ya kumalizia kwa kuyaezeka, hii ni kwa mujibu wa sera ya nchi inayowataka
wananchi kushirikiana na serikali yao katika utekelezaji wa miradi mbalimbali
ya maendeleo,” alieleza Kessy.
Post a Comment