Mbunge wa viti maalumu kwa tiketi ya CHADEMA, Rachel Mashishanga akiwahutubia wakazi wa kata ya Ndala katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na chama hicho kuwashukuru wakazi hao kwa kuwachagua wagombea wa CHADEMA katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
 
Mbunge Mashishanga akipokea kadi kutoka kwa mwanachama wa CCM, Mohamed Abdalah baada ya kuamua kujiunga na CHADEMA kutokana na kuvutiwa na hotuba nzuri ya Mbunge Mashishanga.
 
Sehemu ya umati wa wakazi wa Ndala waliohudhuria mkutano huo wakimsikiliza mbunge Mashishanga.
 
Diwani wa kata ya Ndala, Sungura George Kigosi akiwasalimia wananchi.
 
Baadhi ya wajumbe wa kamati za serikali za mitaa kwa tiketi ya CHADEMA kata ya Ndala wakiwasalimia wananchi.
CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Shinyanga kimetoa wito kwa wakazi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi katika kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura wakati kazi hiyo itakapoanza ili wapate fursa ya kupiga kura ya kuikataa katiba iliyopendekezwa na wabunge wa CCM.
Wito huo umetolewa na mbunge wa viti maalumu kwa tiketi ya CHADEMA, Rachel Mashishanga alipokuwa akiwahutubia wakazi wa kata ya Ndala manispaa ya Shinyanga katika mkutano wa hadhara ulioitishwa kwa ajili ya kuwashukuru wakazi wananchi kwa kukiwezesha CHADEMA kuwa chama tawala katika kata hiyo.
 
Mashishanga alisema ni muhimu kwa kila mkazi wa Shinyanga aliyekerwa na kitendo cha wabunge wa CCM kutupilia mbali maoni yao yaliyokusanywa na Tume ya Jaji Joseph Warioba juu ya katiba mpya wanayoitaka na badala yake kuingiza mambo ambayo yatachangia kwa kiasi kikubwa kuendelea kwa vitendo vya kifisadi hapa nchini.
 
Alisema si vizuri kukaa wakilalamika na kupiga kelele kuilalamikia serikali iliyopo madarakani hivi sasa na badala yake wahakikishe wanatoa fundisho jingine kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya kuwaadhibu katika uchaguzi wa serikali za mitaa katika maeneo mengi ya miji nchini ni kuikataa katiba iliyopendekezwa kupitia sanduku la kura.
 
“Ndugu zangu pamoja na kutoa shukrani zetu za dhati kwa uamuzi mgumu mlioufanya wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kuwapiga chini wagombea wa CCM na kuwachagua wale wa CHADEMA, lakini niwaombe jambo moja muhimu nalo si jingine bali ni la kujiandikisha kwa wingi kwenye daftari la kudumu la wapiga kura,”
 
“Mtakapojiandikisha mtakuwa mmepata fursa ya kuikataa katiba iliyotupilia mbali maoni yenu, maana mambo yote muhimu mliyopendekeza kwa mstakabali wa taifa lenu, wenzetu wa CCM wameyatupilia mbali na kuweka yale yanayojari maslahi yao binafsi, hivyo dawa ni kupiga kura za hapana kwa wingi,” alieleza Mashishanga.
 
Katika hatua nyingine alitoa wito kwa wenyeviti wote wa mitaa waliochaguliwa kwa tiketi ya CHADEMA kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa wananchi waliowachagua bila ya kuwawekea vikwazo vyovyote ikiwemo tabia iliyokuwa ikifanywa na wenyeviti wa CCM ya kuwatoza fedha wananchi pale walipohitaji huduma ya kupigiwa mhuri hati mbalimbali.
 
“Natoa wito kwa wenyeviti wote wa mitaa wanaotokana na CHADEMA hakikisheni mnatekeleza majukumu yenu kwa kuwatumikia wananchi bila visingizio vyovyote vile, tusisikie mnaomba fedha, tukipata habari hatutosita kuwaondoa madarakani mara moja, eleweni waajiri wenu ni hawa wananchi, sasa timizeni wajibu wenu kwao,”
 
“Lazima muonesha tofauti kati ya wenyeviti wa CCM na wale wa CHADEMA, na ndugu zangu wananchi msipate hofu yoyote kuwafichua wenyeviti wenu mtakaowaona hawatimizi wajibu wao kikamilifu, tupeni taarifa tuwachukulie hatua, lakini mkiona na sisi tunafanya longolongo, itisheni mkutano mkuu wa kata wapigeni chini mara moja, CHADEMA hatulei uzembe.” alisisitiza Mashishanga.
 
Katika hatua nyingine mmoja wa wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mohamed Abdalah aliyekuwa amehudhuria katika mkutano huo wa hadhara aliamua kujitoa CCM na kujiunga papo hapo na CHADEMA hali iliyoamsha shamra shamra kwa wananchi waliokuwa kwenye mkutano huo, ambapo mbunge Mashishanga alimpongeza kwa uamuzi wake wa busara.
 
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top