SERIKALI imeshauriwa kutekeleza kwa uangalifu mkubwa adhima yake ya kupambana na waganga wa jadi wanaojihusisha na upigaji ramli zinazodaiwa ni chanzo cha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albinism) kwa vile hatua hiyo inaweza kusababisha madhara makubwa kwa taifa.
 
Ushauri huo umetolewa na mmoja wa wazee maarufu mjini Shinyanga, Iddi Juma ambapo amesema serikali haipaswi kukurupuka katika kushughulikia suala la waganga wa jadi kwa vile baadhi yao wana umuhimu mkubwa kwa jamii na wamekuwepo nchini tangu enzi na enzi.
 
Juma alisema kuwadharau waganga wa jadi ni kutaka kusababisha matatizo yasiyo ya lazima yanayoweza kutokea nchini kwa vile wengi wao wana uwezo mkubwa wa kutibu baadhi ya magonjwa yaliyoshindikana kwa kutumia miti shamba na hata baadhi ya viongozi wakubwa serikalini na wanasiasa huwategemea waganga hao katika mambo yao mengi.
 
“Nimesikia serikali imetangaza hivi karibuni itaendesha kampeni ya kupambana na waganga wa jadi wanaopiga ramli chonganishi kwa kuwakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria, sipingani na kampeni hii, ombi langu kwa serikali iwe makini inapotekeleza kazi hii vinginevyo inaweza kutuletea madhara makubwa,”
 
“Waganga wa jadi ni watu muhimu katika jamii yetu, kuna magonjwa yanayoshindikana katika tiba za kitaalamu lakini wao wamekuwa wakiyatibu, magonjwa mengine bwana hayana tiba katika hospitali zetu, lakini ni rahisi mno kupata tiba yake kwa waganga wa jadi, kukurupuka na kuwakamata ni kujiletea matatizo,” 

"Hivi kweli kuna tiba yoyote ya majini au mapepo machafu katika hospitali zetu nchini? wanaopatwa na matatizo haya mara nyingi tunaona wanakimbizwa kwa waganga wa jadi, ndiyo wataalamu wa kuyatibu, na huko ni lazima mganga afanye mambo yake ili kubaini yametokea wapi, sasa tukiwakamata wenye matatizo haya watatibiwa wapi?" alihoji Juma.
 
Mzee huyo alisema yeye binafsi anao ushahidi baadhi ya viongozi wa kisiasa na wa kiserikali ambao wanategemea sana nguvu ya waganga wa jadi, na kwamba kutokana na hali hiyo ni wazi wale watakaokamatwa na kuchukuliwa hatua watakuwa ni wasiokuwa na mahusiano na viongozi wowote ndani ya serikali ama wanasiasa.
 
Alisema yapo mambo yanayoweza kufanywa na waganga hao kutokana na kutoridhishwa na hatua zitakazochukuliwa na serikali dhidi yao na hivyo kusababisha mtafaruku mkubwa nchini ambapo amesisitiza umuhimu wa kutumika kwa busara kubwa katika kuwabaini wanaojihusisha na upigaji ramli chonganishi badala ya kukurupuka kukamata ovyo.
 
“Hawa watu wasidharauliwe, maana wametajwa hata ndani ya vitabu vya mwenyezi mungu, kwa sisi waislamu ipo aya inayoelezea jinsi mambo ya kichawi yalivyofundishwa na malaika wawili, lakini mungu ametukataza kabisa binadamu tusijihusishe nayo kwani ni fitina juu yetu, hivyo ni muhimu tukawa makini katika kuwashughulikia,” alieleza Juma.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top