Risala kwa Mgeni rasmi. |
Baadhi ya watendaji wa Idara ya Uhamiaji wakifuatilia kwa umakini mkubwa kikao kilivyokuwa kikiendelea. |
Mr. Suleiman Kamea - Ofisa Uhamiaji Katavi akifuatilia kwa umakini kikao. |
Ofisa Uhamiaji mkoani Shinyanga, Annamaria Yondani akiwakaribisha wajumbe katika kikao. |
KATIKA kukabiliana na wimbi la wahamiaji haramu nchini, serikali imeombwa kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali zinazoikabili idara ya uhamiaji nchini ambazo ni kikwazo katika utekelezaji wa kazi zake sambamba na kuwapatia elimu zaidi maofisa wake.
Ombi hilo limetolewa mjini Shinyanga katika mkutano wa Kamati ya maofisa uhamiaji katika kanda ya Magharibi (WIISC) na maofisa wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kutoka mikoa ya Katavi, Mara, Kagera, Kigoma, Rukwa, Singida, Tabora, Geita, Simiyu na Shinyanga.
Akisoma risala yao mbele ya mgeni rasmi, mwenyekiti wa WIISC, Remigius Pesambili ambaye ni ofisa uhamiaji mkoa wa Mwanza alisema pamoja na idara ya uhamiaji kuwa ni idara nyeti katika kuhakikisha hakuna wahamiaji haramu wanaoingia hapa nchini lakini bado idara hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali.
Pesambili alisema baadhi ya changamoto zinazoikabili idara hiyo ni pamoja na ukosefu wa huduma za mawasiliano kwa njia ya mtandao wa internet katika baadhi ya vituo na hivyo kuchelewesha utumwaji wa data mbalimbali za wasafiri kwenda makao makuu zinazokusanywa vituoni kila siku.
Ukosefu wa huduma ya umeme wa uhakika katika vituo vya Rusumo mkoani Kagera na Manyovu na Mabamba (Kigoma) hali ambayo huchangia kukwama kutekelezwa kikamilifu kwa utendaji wa mfumo wa kusajili wasafiri (Personal Identification and Registration System (PIRS).
“Pamoja na mafanikio yaliyopo katika kupambana na wahamiaji haramu hapa nchini ambapo mikoa kwa upande wake hushirikiana na Kamati za Ulinzi na Usalama katika kuendesha opresheni za pamoja, kupanga doria, kutoa elimu kwa viongozi wa vijiji na kata, bado kuna changamoto kadhaa zinazotukabili,”
“Ukosefu wa umeme wa uhakika katika vituo vya Manyovu, Mabamba mkoani Kigoma na Rusumo katika mkoa wa Kagera ni moja ya changamoto kwetu hasa katika usajiri wa wasafiri, lakini pia changamoto nyingine ni huduma ya mawasiliano ya internet katika baadhi ya vituo huchelewesha utumaji wa taarifa,” alieleza Pesambili.
Hata hivyo mwenyekiti huyo alisema iwapo serikali itaendelea kuwapatia elimu zaidi baadhi ya maofisa wake wataweza kukabiliana na baadhi ya changamoto zilizopo hivi sasa na kuweza kufikia lengo la utoaji wa huduma bora hasa katika kuangalia suala la utokaji na uingiaji wa raia kutoka nchi jirani.
“Tatizo la wahamiaji haramu duniani limekuja na changamoto nyingi ikipelekea kuhatarisha usalama wa nchi zetu, uharibifu wa mazingira, uvuvi haramu, usafirishaji wa madawa ya kulevya, wizi wa magari, uwindaji haramu katika mbuga za wanyama na utakatishaji wa fedha haramu, ni muhimu tukaunganisha nguvu zetu kudhibiti hali hii,” alieleza Pesambili.
Kwa upande wake mgeni rasmi mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Ally Rufunga katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu tawala msaidizi sekretarieti ya mkoa Projuctus Rutabanzibwa, aliwapongeza watumishi wote wa idara ya uhamiaji katika mikoa ya magharibi kwa jinsi wanavyokabiliana na wimbi la wahamiaji haramu.
“Nichukue fursa hii kukupongezeni kwa juhudi mnazozionesha katika utendaji kazi wenu wa kila siku, binafsi nimefurahishwa na jinsi idara hii inavyoshirikiana na kamati za ulinzi na usalama katika utekelezaji wa majukumu yake kwa lengo la kufikia mafanikio ya kweli,”
“Niwaombe kwamba muendelee kushirikiana na Jeshi la Polisi, mamlaka ya mapato (TRA), Idara ya uvuvi na afya ambazo ni msingi katika ulinzi wa mipaka yetu, uhusiano huu kama mtautumia vizuri utatusaidia katika kupambana na wahamiaji haramu, uvuvi haramu na uhalifu wa aina mbalimbali,” ilieleza sehemu ya hotuba ya mkuu wa mkoa.
Post a Comment