Wazazi na walezi kutoka vijiji vitano vya kata ya Usanda walioshiriki kikao cha kutambulisha mradi wakifuatilia mada zilizowasilishwa kwenye kikao hicho.

Washiriki wa kikao cha kutambulisha mradi wa utoaji elimu ya afya ya uzazi na haki ya mtoto wakimsikiliza Mkurugenzi wa Shirika la Agape - Shinyanga, John Myola mwenye (shati jeupe)

Mmoja wa wataalamu katika kata ya Usanda wilayani Shinyanga akichangia mada juu ya majukumu ya wazazi kwa watoto.


UKOSEFU wa elimu ya afya ya uzazi kwa watoto wa kike wenye umri kati ya miaka 10 hadi 18 umetajwa kuchangia matukio ya mimba na ndoa za umri mdogo mkoani Shinyanga.


Hali hiyo imebainishwa katika uzinduzi wa utekelezaji wa Mradi wa elimu ya afya ya uzazi na haki ya mtoto utakaotekelezwa kwa miaka miwili na nusu na Shirika la Agape mkoani Shinyanga chini ya ufadhili wa shirika la kimataifa la Save the Children (SCI) kwenye kata ya Usanda wilayani Shinyanga.

Akitoa taarifa kwa wawakilishi kutoka makundi mbalimbali ya kijamii ikiwemo walimu wa shule za msingi, Mkurugenzi wa Shirika la Agape, John Myola alisema ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi miongoni mwa jamii bado ni tatizo katika maeneo mengi ya mkoa wa Shinyanga.

Myola alisema hali hiyo imechangia tafiti nyingi zilizoendeshwa na mashirika mbalimbali ya kimataifa ikiwemo UNFPA na UNICEF kuonesha mkoa wa Shinyanga unaongoza kwa mimba na ndoa za utotoni ikilinganishwa na maeneo mengine nchini.

“Elimu ya afya ya uzazi na haki ya mtoto bado ni tatizo kubwa miongoni mwa jamii ya wakazi wa mkoa wa Shinyanga, hivyo kuna kila sababu wananchi  waanze kuchukua hatua madhubuti za kupambana na changamoto zinazosababishwa na ukosefu wa elimu hii zinazochangia kurudisha nyuma maendeleo yetu,”

“Ni jukumu letu hivi sasa kujikita katika kuhakikisha tunawafundisha watoto wetu waweze kuielewa vyema elimu hii itakayowasaidia kujitambua katika makuzi yao, na itawasaidia kujiepusha na vitendo vinavyosababisha wabebe mimba wakiwa na umri mdogo,” alieleza Myola.

Kwa upande wake Ofisa miradi kutoka Shirika la Save the Children, John Maliyapambe alisema elimu ya afya uzazi ikiwemo masuala ya ujinsia itamwezesha mtoto wa kike kufika malengo yake katika suala zima la kupata elimu kama ilivyo kwa mtoto wa kiume.

Maliyapambe alisema watoto wengi wa kike hujikuta wakiingia katika matatizo ikiwemo kubeba mimba za umri mdogo au kuozeshwa kwa nguvu kutokana na wao wenyewe ama wazazi wao kutokuwa na uelewa wa kutosha juu ya elimu ya afya ya uzazi.

“Mradi huu umelenga kumsaidia mtoto wa kike aweze kufikia malengo yake ya baadae badala ya kukatishwa kutokana na kubeba mimba au kuolewa akiwa na umri mdogo, hii ni pamoja na kuielimisha jamii iweze kumlinda mtoto wa kike katika kipindi cha makuzi yake,”

“Mtoto wa kike alindwe asipatwe na madhara yoyote yanayotokana na ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, na hii itafanikiwa kutokana na ushirikiano wa kada mbalimbali zinazoshughulikia masuala ya watoto ikiwemo jamii yenyewe.  watoto wa kike wakiwa na uelewa juu ya elimu ya afya ya uzazi itawasadia katika makuzi yao,” alieleza Maliyapambe.

Washiriki wakiendelea na kikao


John Mliyapambe akitoa mada yake kuhusiana na umuhimu wa utoaji wa elimu ya afya ya uzazi na haki ya mtoto kwa jamii.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, mratibu wa miradi kutoka Agape, Lucy Maganga, alisema mradi utazihusisha shule tano za msingi katika kata ya Usanda na kushirikisha wapatao 1,000 watakaopatiwa mafunzo juu ya afya ya uzazi.

Ofisa miradi, tathimini na ufuatiliaji kutoka Shirika la Agape akitoa ufafanuzi juu ya utekelezaji wa mradi wa utoaji elimu ya afya ya uzazi na haki ya mtoto.
“Walengwa wetu ni watoto wenye umri wa kuanzia miaka 10 hadi 18 walioko shuleni ambako tumepanga kufikia watoto wapatao 1000 na kwa walioko nje ya shule tutafikia watoto 100 pamoja na watu wazima 2,500, tunaomba ushirikiano wa jamii ili mradi huu uweze kufanikiwa,”

“Tukumbuke mradi huu umeilenga jamii yenyewe, ukifanikiwa utatupa mafanikio makubwa na tutakuwa tumewakomboa watoto wetu wa kike, na niombe kuanzia sasa wazazi na jamii kwa ujumla tujenge tabia ya kukaa na watoto wetu na kuwafundisha mambo muhimu yanayohusiana na makuzi yao,” alieleza Maganga.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top