Sehemu ya magunia ya mahindi yaliyohifadhiwa kwenye ghala la NRFA kanda ya Shinyanga ambayo wabunge yanaonesha dalili za kuanza kubanguliwa na wadudu waharibifu. |
SERIKALI
imeshauriwa kuangalia uwezekano wa kuanza kuuza mahindi yaliyohifadhiwa katika
maghala ya wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula nchini (NRFA) ambayo baadhi yake
yapo katika hatari ya kuanza kuharibiwa na wadudu waharibifu wa mazao.
Ushauri
huo umetolewa mjini Shinyanga na wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Maji, Kilimo na Mifugo iliyokuwa ikitembelea miradi mbalimbali iliyopo chini ya
kamati hiyo inayotekelezwa mkoani Shinyanga.
Mbali
ya hofu ya kuharibika kwa mahindi hayo ambayo kumbukumbu zinaonesha
yalinunuliwa katika msimu wa 2014/2015 pia wabunge walishangazwa na kitendo cha
serikali kuendelea kuyahifadhi wakati maeneo mengi nchini wananchi wanahitaji
chakula cha kununua kwa bei nafuu kutokana na bei hivi sasa kuwa juu.
Wakiwa
katika ghala la akiba ya chakula (NRFA) mjini Shinyanga wabunge wa kamati hiyo
wakiongozwa na mwenyekiti wao, Mary Nagu walishuhudia sehemu ya magunia ya mahindi
yaliyomo ndani ya ghala hilo yakiwa na wadudu na baadhi yake yakitoa ungaunga
kuashiria kuanza kushambuliwa na wadudu.
Wabunge
walionesha mshangao kutoka na hali waliyojionea ambapo walishangazwa na kitendo
cha serikali kuendelea kuhifadhi idadi kubwa ya chakula katika maghala yake
huku maeneo mengi nchini ikiwemo wilaya 55 zikiwa na uhaba mkubwa wa chakula na
wananchi wakiuziwa debe moja la mahindi kati ya shilingi 20,000 hadi 25,000.
“Mheshimiwa
mwenyekiti hii hali inatushangaza, ni ajabu kuona chakula kipo cha kutosha
lakini huko nje wananchi wanahangaika na hivi sasa wanauziwa mahindi kwa bei
kubwa, lakini cha ajabu haya yaliyopo hapa tumejionea wenyewe yameanza
kubunguliwa na wadudu, ipo hatari yataharibika,”
“Katika
taarifa ya NRFA wamesema moja ya changamoto waliyonayo ni uhaba wa fedha, hiki
ni kichekesho, kwa nini wasiuze mahindi waliyonayo zaidi ya tani 8,000 wakati hali ya
soko ni nzuri, ni bora wayauze ili wapate fedha na wanunue mengine mapya,”
alieleza Mohamedi Mgimwa mbunge wa Mufindi Kaskazini.
Kwa
upande wake mbunge wa jimbo la Uzini, Salum Rehani alisema iwapo serikali
haitochukua hatua ya kuruhusu kuuzwa kwa mahindi hayo ipo hatari yakakosa soko
baada ya wananchi kuanza kuvuna mavuno mapya hivi karibuni na kwamba
wanachohitaji wananchi ni chakula cha bei nafuu na siyo cha bure.
Hata
hivyo kwa upande wake Kaimu Ofisa mtendaji mkuu wa NRFA, Deusdedit Mpazi
alikanusha madai ya mahindi kuwa katika hatari ya kuharibika kwa vile mara kwa
mara hufanyika ukaguzi wa kuangalia iwapo hayajaingiliwa wadudu waharibifu.
“Mheshimiwa
mwenyekiti si kweli kwamba mahindi haya yapo katika hatari ya kuharibika, hawa
wadudu mnaowaona hapa hawana madhara makubwa, ni wadudu visumbufu tu, na hivi
karibuni tunatarajia kuanza zoezi la kupulizia dawa, hivyo hayawezi kuharibika
kama mnavyohofia,” alieleza Mpazi.
Akizungumzia
suala la mahindi hayo kutopelekwa kwa wananchi ili yauzwe kwa bei nafuu, Naibu
waziri wa Kilimo, mifugo na uvuvi, Ole Nasha alisema hofu ya serikali ni kuona
mahindi hayo yatakapopelekwa kwa wananchi kuangukia kwenye mikono ya walanguzi
na kuuzwa kwa bei ya juu.
“Hatukurupuki
kusambaza mahindi haya ovyo, tuko makini ili kuhakikisha pale yatakapopelekwa
kwa wananchi yanawafikia walengwa husika, lakini pia tunasubiri kipindi halisi
cha mavuno ili tuweze kuona kiasi halisi cha mazao kitakachopatikana, na hivyo
chakula hiki kitapelekwa kwenye maeneo yenye upungufu mkubwa,” alieleza waziri.
Post a Comment