Baadhi ya watoto wa shule ya msingi Shingida wilayani Shinyanga wakijiandaa kurejea nyumbani baada ya kukamilisha masomo yao ya siku |
WITO
umetolewa kwa wakazi wa mkoa wa Shinyanga kujitolea kwa hali na mali kusaidia
ujenzi wa vyumba maalumu kwenye shule za msingi na sekondari vitakavyotumika kwa
ajili ya kujihifadhi watoto wa kike wanaoingia kwenye hedhi.
Ukosefu
wa vyumba hivyo umetajwa kuwa moja ya changamoto inayowakabili watoto wengi wa
kike katika shule za msingi na sekondari hali inayochangia wapoteze vipindi
vingi vya masomo kila mwaka kutokana na kushindwa kuhudhuria masomo.
Wito
huo umetolewa na mkurungenzi wa Shirika la Agape Aids Control Programme mkoani
Shinyanga, John Myola kwenye kikao cha uzinduzi wa mradi wa utoaji elimu ya
afya ya uzazi na haki ya mtoto utakaotekelezwa katika kata ya Usanda wilayani
Shinyanga chini ya ufadhili wa Shirika la Save the Children.
Akichangia
hoja iliyowasilishwa na washiriki waliohudhuria uzinduzi wa mradi huo, Myola
alisema imefika wakati jamii yenyewe ikabiliane na changamoto ya ukosefu wa
vyumba hivyo na ijitolee kuvijenga kwa ushirikiano na serikali ili kuwanusuru
watoto wa kike badala ya kusubiri misaada ya wafadhili au serikali kuu.
Akizungumzia
changamoto hiyo, Myola alisema jamii inapaswa kubadilika kwa kuanza kuchukua
hatua za kukabiliana na changamoto ambazo wana uwezo wa kukabiliana nazo mfano
wa ujenzi wa vyumba hivyo ambavyo gharama zake siyo kubwa.
Kutokana
na hali hiyo yeye binafsi aliahidi kuchangia bati 10 kwa shule yoyote katika
kata ya Usanda itakayokuwa ya kwanza kuanzisha ujenzi wa chumba maalumu ambapo
pia alisema atajitolea kutoa kilo 40 za unga na dagaa kwa watu watakaojitolea
kujenga na yeye mwenyewe atashiriki kwenye ujenzi huo.
“Ukosefu
wa vyumba hivi unawaathiri watoto wetu sisi wenyewe, hivyo tusibweteke kusubiri
wengine kutuondolea tatizo hili, lazima tuamue, wenyewe tuanze sasa, kata ya
Usanda ioneshe mfano kwamba jamii ikiamua inaweza, vyumba hivi havihitaji
gharama kubwa, mbali ya watoto kujihifadhi pia vitatumika kutolea huduma ya
kwanza kwa watakaopatwa tatizo lolote,”
“Mimi
binafsi naahidi kuchangia bati 10 kwa watakaokuwa wa kwanza kuanzisha ujenzi,
na nitatoa kilo 40 za unga na dagaa kwa ajili ya chakula cha watakaojitolea
kujenga chumba hicho, ndugu zangu tutumie njia ya nguvu kazi, tusaidiane na
serikali yetu ili kuwaondolea watoto wetu ukosefu wa eneo la kujihifadhi,”
alieleza Myola.
Kwa
upande wake mmoja wa washiriki wa kikao hicho, Kennedy Malesa alisema ukosefu
wa vyumba maalumu kwa ajili ya kujihifadhi watoto wa kike ni changamoto iliyopo
katika shule nyingi za msingi na sekondari maeneo mengi nchini hali
inayosababisha washindwe kwenda shule wanapokuwa katika hedhi.
Awali
wakichangia mada juu ya uendeshaji wa mradi wa elimu ya afya ya uzazi na haki
ya mtoto, washiriki wa kikao hicho walisema iwapo elimu hiyo itawekewa mkazo
itapunguza kwa kiasi kikubwa matukio ya mimba za utotoni ikiwemo maambukizi ya
virusi vya UKIMWI.
“Tunawashukuru
wenzetu wa Agape na Save the Children kwa kutuletea mradi huu, tunaani
ukitekelezwa kikamilifu utapunguza tatizo la watoto wa kike kubeba mimba wakiwa
na umri mdogo, wengi wanabebeshwa mimba kutokana na kutojitambua juu ya makuzi
yao na wengine kuambukizwa virusi vya UKIMWI na magonjwa ya zinaa,”
Ofisa Mradi kutoka Shirika la Save the Children CIS, John Maliyapambe akitoa maelezo kuhusiana na mradi wa utoaji elimu ya afya ya uzazi na haki ya mtoto katika kata ya Usanda wilaya ya Shinyanga. |
“Lakini
ni vizuri elimu hii ikawafikia pia wazazi ili iwasaidie kubadilika, wapo baadhi
yao hushindwa kusikiliza ushauri wa wazazi wenzao wanaposhauriwa kuhusiana tabia mbaya za watoto
wao wanaojiingiza katika nyendo zisizofaa ikiwemo kujihusisha na mambo ya
mapenzi wakiwa na umri mdogo,” alieleza Chande Musa katibu wa msikiti wa
Usanda.
Post a Comment