Nape Nnauye akiwahutubia waandishi wa habari akiwa amesimama juu ya gari lake baada ya kikao chake cha ndani kupigwa "STOOOP" na Polisi. |
Khamis Mgeja katika moja ya mikutano ya chama chake cha CHADEMA. |
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. |
Mgeja ambaye kwa hivi sasa ni miongoni mwa makada wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) alitoa kauli ya kulaani kitendo
hicho alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mkoani Kigoma ambapo
amemuomba waziri mkuu, Kassim Majaliwa asimame hadharani kuwaomba radhi
watanzania kwa niaba ya serikali.
Akifafanua Mgeja aliyewahi kuwa kiongozi wa ngazi ya
juu ya kimkoa ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) alisema tukio la Nape
kutishiwa silaha ni moja ya matukio ya ukandamizaji wa haki za kibinadamu
yanayoendelea kushamiri hapa nchini chini ya serikali ya awamu ya tano
inayoongozwa na CCM.
Nape Moses Nnauye |
“Kwa kweli mimi binafsi pamoja na taasisi yangu ya
Tanzania Mzalendo Foundation tunalaani vikali kitendo kilichotendwa hadharani
na mmoja wa walinzi wa raia kutumia kumtisha raia kwa silaha ya moto kwa lengo
tu la kumzuia asizungumze na wanahabari, tukio hili limetushitua na
kutusikitisha,”
“Matukio haya ni ishara ya wazi ya ukandamizaji wa
demokrasia na ni matumizi mabaya ya madaraka ambayo yameanza kushika kasi
miongoni mwa viongozi wa serikali, wananchi wengi hivi sasa hawatendewi haki,
angalieni yanayotokea kwa wafugaji, hivi karibuni vijana wawili wa wafugaji
kule Bagamoyo walipigwa risasi na kufa,” alieleza Mgeja.
Aliendelea kueleza kuwa wananchi wanyonge hivi sasa
wanajiuliza iwapo mtu aliyekuwa waziri wa serikali, kada maarufu ndani ya chama
tawala na aliyekipigania kiweze kupata ushindi japokuwa kwa goli la mkono leo
anafanyiwa hivyo na vyombo vya dola na kudhalilishwa mbele ya kadamnasi kwa
wananchi wanyonge hali ingekuwaje.
“Tunashauri sasa waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Kassim Majaliwa ambaye ni kiongozi na msimamizi mkuu wa shughuli za
serikali za kila siku, asimame hadharani kwa niaba ya serikali yake ya CCM
awaombe radhi watanzania kwa matukio haya ya uvunjaji wa haki za kibinadamu na
demokrasia ikiwemo ukandamizaji wa haki kibinadamu na utawala bora hapa nchini,”
alieleza Mgeja.
Mwenyekiti huyo ameiomba na kuishauri serikali iache
kushughulikia watu kwa vitisho bali ielekeze nguvu zake katika kuboresha maisha
ya watanzania ili yawe bora na kwamba kwa sasa hali ya maisha kwa watanzania
wengi imekuwa ngumu huku mfumko wa bei za bidhaa mbalimbali ukipaa kila siku.
Hata hivyo kwa upande mwingine Mgeja alimpongeza Nape
kwa ujasiri aliouonesha japokuwa anapingana naye kiitikadi na kimtizamo kwa
muda mrefu na kwamba kitendo alichokifanya kimeonesha uzalendo wake hasa pale
alipowahamasisha vijana na watanzania kutokuwa waoga na kuwataka wasimame imara
kudai haki zao.
“Haya yanayojitokeza sasa nchini tumekuwa tukiyaona nchi
za wenzetu kule Zimbabwe, Congo, Rwanda, Burundi na hata jirani zetu pale
Uganda, hivyo tusidanganyane kwamba hii ni Tanzania mpya tunayoitaka
watanzania, tuwaombe viongozi wetu wa dini na wastaafu waisaidie nchi kuliko
kukaa kimya, maana hili ni janga jipya kwa taifa letu,” alieleza.
Post a Comment