SEREKALI imeombwa
kutunga sheria itakayotoa adhabu kali kwa wazazi wenye tabia ya kukatisha
masomo na kuwaozesha kwa lazima watoto wao wa kike bila kujali madhara
wanayoyapata kutokana na kuolewa wakiwa na umri mdogo.
Ombi hilo limetolewa na
watoto walioshiriki katika Kongamano la Siku ya Kimataifa ya mtoto wa kike
duniani lililofanyika mjini Shinyanga ikiwa ni maandalizi ya kilele cha
maadhimisho hayo yatakayofanyika kitaifa Oktoba 11, mwaka huu mkoani Shinyanga.
Watoto hao walisema
wazazi wengi wamekuwa wakikimbilia kuwaozesha watoto wao wa kike bila kujali
athari wanazopata ikiwemo mimba katika umri mdogo zinazoweza kusababisha kifo
na kwamba tabia hiyo inaelekea kuwa sugu miongoni mwa wakazi wa mkoa wa
Shinyanga kutokana na kutokuwepo kwa sheria kali inayozuia watoto wadogo
kuozeshwa.
Sehemu ya watoto wa kike walioshiriki kongamano wakimsikiliza mgeni rasmi kutoka wizarani, Bi. Margareth Mussai |
Mwakilishi kutoka Shirika la ICS SP, Shadia Naka akitoa neno kwa washiriki wa Kongamano. |
Wakitoa ushahidi juu ya
madhara wanayopata kutokana na kuolewa wakiwa na umri mdogo baadhi ya watoto
walisema wengi wao wamekuwa wakiathirika kiafya na kisaikolojia ikiwemo kukosa
elimu baada ya kukatishwa ndoto zao za kusoma kwa kadri ya uwezo walionao kama
wenzao wa kiume wanavyopatiwa fursa hiyo.
Miongoni mwa watoto
waliokatishwa masomo na kuozeshwa kwa nguvu ambao hivi sasa wanatunzwa na
Shirika la Agape Aids Control Programme (AACP) la mjini Shinyanga walipata
nafasi ya kutoa ushuhuda juu ya madhara waliyoyapata baada ya kufungishwa ndoa
kwa lazima na wazazi wao bila ya ridhaa yao.
Moja ya madhara
waliyotaja ni vipigo kutoka kwa wanaume waliozeshwa ambao hawakuwa na mapenzi
nao ya dhati kwa vile hawakuridhia kuolewa ikiwemo suala la kupata matatizo
wakati wa kujifungua kutokana maumbile yao hasa ikizingatiwa umri mdogo
waliokuwa nao huku wanaume wengine wakizikataa mimba wakidai si za kwao.
Sehemu ya watoto wa kike ambao ni wahanga wa mimba na ndoa za utotoni wanaotunzwa na kupatiwa elimu ya kujiendeleza na Shirika la Agape Shinyanga. |
“Mimi niliolewa nikiwa
na umri wa miaka 13, pamoja na kuchaguliwa kujiunga na masomo ya sekondari
mwaka 2013, lakini wazazi wangu walikataa nisiende shule na badala yake
walinitafutia mwanamume ili anioe, huyo alikuwa na miaka 36, nilisikia machungu
makubwa hasa nilipoona wenzangu niliofaulu nao wanaendelea na masomo,”
“Wazazi wangu walipokea
mahari ya ng’ombe 11 na nikaozeshwa kwa nguvu, hata hivyo kipindi kifupi tangu
niolewe, mwanamume yule alikuwa akinipiga kila siku, na hata pale nilipopata
ujauzito alikataa na kudai mimba ile si yaka, na kunitaka nirudi kwetu, kweli
niliumia na kujuta sana,” alieleza mmoja wa wahanga wa ndoa za utotoni.
Aliendelea kueleza
baada ya muda maisha kati yake na mume wake yalikuwa magumu zaidi, pamoja na
usuluhishi wa mara kwa mara uliokuwa ukifanywa na ndugu za upande wa mume,
lakini tabia ya mume wake ya kumpiga na kumuumiza vibaya iliendelea na hivyo
aliamua kuondoka kwa na kurudi kwa wazazi wake.
Hata hivyo alisema
akiwa nyumbani kwao watu wa Shirika la Agape walikwenda kijijini kwao kuonesha
sinema juu ya madhara ya ndoa na mimba za utotoni ambapo alikutana na
mkurugenzi wa shirika hilo na kumuomba ajiunge ili aweze kupata nafasi ya
kujiendeleza kimasomo na hivi sasa anasoma kidato cha pili.
Kwa upande wake katibu
wa Baraza la watoto mkoani Shinyanga, Christina Bakari alisema ili kukabiliana
na wimbi la ndoa na mimba za utotoni ni muhimu serikali na wadau mbalimbali wa
asasi za kiraia wakashirikiana kwa pamoja kukomesha tabia hiyo inayochangiwa na
tamaa ya mali kwa baadhi ya wazazi.
“Matukio ya ndoa za
utotoni bado ni janga kubwa kwa sisi watoto wa kike hasa katika mkoa wetu wa
Shinyanga, tunaiomba serikali iweke mkazo katika kupiga vita vitendo hivi,
itunge sheria kali itakayowabana wazazi na wale wote wenye kupenda kuoa watoto
wadogo badala ya kuwaacha wasome,”
“Kutokuwepo kwa sheria
inayotoa adhabu kali kwa wazazi wanaowakatisha masomo ya watoto wa kike kwa
lengo la kuwaozesha ni janga kubwa kwetu sisi watoto, maana hali ya umaskini
ndani ya familia imesababisha tugeuzwe kuwa vitega uchumi kwa kuozeshwa tukiwa
na umri mdogo badala ya kupewa haki yetu ya kupata elimu,” alieleza Christina.
Akizungumza katika
kongamano hilo mwakilishi kutoka Shirika la ICS SP Kanda ya Tanzania, Shadia Naka alisema serikali
inapaswa kuongeza mkazo katika suala zima la ulinzi wa mtoto wa kike kwa
kuhakikisha kila mtoto aliyekuwa shuleni hivi sasa anamaliza masomo yake bila
ya kukatishwa kwa sababu zisizokuwa na msingi.
Hata hivyo alisema pana
umuhimu pia wa serikali kujenga mazingira bora yatakayowezesha upatikanaji wa
elimu bora badala ya bora elimu kwa kuboresha mazingira ya kujifunzia na
kufundishia katika shule zote zilizopo hapa nchini ikiwemo kuweka mkazo kwenye
ujenzi wa mabweni katika shule za sekondari.
“Ni muhimu kwa serikali
hivi sasa ikahakikisha inatoa kipaumbele katika suala zima la uboreshaji wa
elimu hapa nchini, elimu inayotolewa iwe ni elimu bora na siyo bora elimu,
isaidie kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia, lakini pia mkazo
uwekwe kwenye ujenzi wa mabweni ili kuwaokoa watoto wa kike wanaoishi mbali ya
shule,” alieleza Naka.
Naye Kaimu mkurugenzi wa watoto kutoka wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, wazee na watoto, Margareth Mussai aliwaomba watoto wa kike
walioko mashuleni kutokubali kurubuniwa na vishawishi vya wanaume na badala
yake wajikite katika masomo ili wapate elimu itakayowasaidia katika maisha yao
ya baadae.
Kaimu Mkurugenzi wa watoto kutoka wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na watoto, Margareth Mussai akiwahutubia wakazi wa kijiji cha Nhelegani, kata ya Kizumbi Manispaa ya Shinyanga. |
Mkazi wa kijiji cha Nhelegani, Kata ya Kizumbi akichangia hoja kuhusiana na suala la jukumu la malezi ya watoto wa kike ambapo alisema ni jukumu la wazazi wawili, baba na mama. |
Kaimu Mkurugenzi wa watoto, Margareth Mussai (aliyebeba mtoto) akiwa katika picha ya pamoja na watoto wa kijiji cha Nhelegani, kata ya Kizumbi, Manispaa ya Shinyanga. |
Alisema
kutokana na ongezeko la ndoa za utotoni katika mkoa wa Shinyanga ambao unaoongoza
kwa asilimia 59, wizara yake imeamua maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya mtoto
wa kike yafanyikie mkoani humo ili kuweza kutoa elimu kwa wakazi wake waweze
kuachana na tabia ya kuozesha watoto wenye umri mdogo ambayo ina athari kubwa
kwa mtoto wa kike.
“Tunaamini
elimu tutakayoitoa katika kipindi cha maadhimisho haya ambayo kilele chake ni
Oktoba 11, mwaka huu tutaweza kufikisha ujumbe kwa wazazi, walezi, watoto na
jamii nzima kwa ujumla ili waone tatizo, na wazazi waone umuhimu wa mtoto wa
kike katika kuleta maendeleo ndani ya familia,” alieleza Mussai.
End.
Post a Comment