Moja ya mabango yaliyooneshwa na wanafunzi wa kike kwenye  Bonanza la kupiga vita mimba za utotoni Shinyanga.

TABIA ya wanaume kuwarubuni kwa zawadi ndogondogo wanafunzi wa kike imetajwa kuchangia kuendelea kwa matukio ya mimba katika umri mdogo mkoani Shinyanga hali inayochangia wengi wao kushindwa kumaliza masomo yao.


Hali hiyo imeelezwa na wanafunzi wa shule za msingi Mwenge, Uhuru na Jomu manispaa ya Shinyanga katika Bonanza la michezo lililoandaliwa kwa ajili ya kufikisha elimu ya kupiga vita na kuzuia mimba na ndoa za utotoni kwa wanafunzi wa kike mkoani Shinyanga.


Maandamano kabla ya Bonanza kuanza, hapa ni kwenye uwanja wa michezo wa Kambarage manispaa ya Shinyanga.
Mradi wa kupiga vita na kuzuia mimba za utotoni kwa wanafunzi wa kike  unaendeshwa na Shirika la Shirika la Young Women Christian Association (YWCA) la mkoani Shinyanga katika kata tatu za manispaa ya Shinyanga ambazo ni Kambarage, Ibadakuli na Mjini.

Wakichangia hoja baadhi ya wanafunzi walioshiriki katika bonanza hilo walisema wengi wao hujikuta wakijiingiza katika vitendo vya kimapenzi na vijana wa mitaani baada ya kurubuniwa na zawadi ndogo ndogo wanazopewa ikiwemo chipsi na lifti za pikipiki.

“Moja ya changamoto tunayokumbana nayo sisi watoto wa kike tunapokwenda au kutoka shuleni ni vishawishi vya wanaume wenye tabia ya kutupatia zawadi ndogo ndogo mfano wa chipsi na wengine tunaokaa mbali kupewa lifti za pikipiki, hii huchangia tuwakubalie kufanya nao mapenzi bila kujua madhara yake,” alieleza mmoja wa wanafunzi hao.

Sikiliza hapo ujumbe wa wanafunzi kidogo.

Kwa upande wake mwakilishi kutoka Jeshi la Polisi kitengo cha dawati la jinsia, Cecilia Kiiza aliwaasa wanafunzi wote wa kike kuacha tabia ya kukubali kurubuniwa kwa vitu vidogo vidogo na badala yake wazingatie masomo yao na kwamba kujiingiza katika mambo ya mapenzi wakiwa na umri mdogo madhara yake ni makubwa.




Hao ni baadhi ya viongozi wa YWCA mwenyekiti na katibu wake katika Bonanza hilo la wanafunzi.

Naye makamu mwenyekiti wa YWCA, Specioza Ikombe aliwataka wanafunzi hao wajiepushe na vitendo vya kukubali kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanaume wadanganyifu katika umri mdogo kabla ya kufikisha umri wa kuolewa na baada ya kuhitimu masomo yao.

“Wanangu nawaomba sana, zingatieni masomo, maisha ya anasa yana wakati wake, tahadharini na vishawishi vya wanaume wanaotaka mfanye nao mapenzi wanaowadanganya kwa vizawadi vidogo vidogo mfano wa chipsi, zawadi hizi zina madhara makubwa ikiwemo kuambukizwa virusi vya UKIMWI,” alieleza Ikombe.

Awali katika taarifa yake katibu wa YWCA, Mericiana Makundi alisema mradi huo unaofadhiliwa na Shirika la Agape utatekelezwa katika kipindi cha miezi 21 katika kata tatu za manispaa ya Shinyanga na pia shirika lake linashughulikia suala la ulinzi na usalama wa mtoto ikiwemo kuhakikisha anapata haki yake ya kupata elimu.

Kwa upande wao wanafunzi kutoka shule za msingi Jomu, Uhuru na Mwenge walishindana katika michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, kukimbia ndani ya gunia na kujaza maji ndani ya ndoo kwa kutumia mikono, ambapo zawadi mbalimbali zilitolewa kwa washindi, huku Shule ya msingi Uhuru wakiwa washindi wa jumla.

Kujaza maji kwenye ndoo kwa kutumia mikono.

Viongozi wanakagua timu za mpira wa miguu.


Kukimbia ndani ya gunia.

Kuvuta kamba

Furaha ya Ushindi kwa timu ya Uhuru shule ya msingi.
 


Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top