Naibu waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina akishiriki kufanya usafi mjini Shinyanga |
Naibu
waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina
ametishia kuanza kuwachukulia hatua za kinidhamu viongozi na watendaji wa
serikali watakaoshindwa kusimamia kikamilifu kazi ya upandaji miti na utunzaji
wa mazingira katika maeneo yao.
Mpina ametoa kauli hiyo aliposhiriki katika zoezi la kufanya usafi eneo la kata ya Ibinzamata Manispaa ya Shinyanga ikiwa ni kutekeleza agizo la Rais Dkt. John Magufuli la kuwataka watanzania kufanya usafi kila siku ya jumamosi ya mwisho wa mwezi.
Zoezi
hilo ambalo kitaifa kwa mwezi huu wa Oktoba limefanyika mkoani Shinyanga ambapo
viongozi mbalimbali ngazi ya mitaa, manispaa, wilaya na mkoa walishirikiana na
Naibu waziri Mpina walishiriki katika kufanya usafi kwenye maeneo mbalimbali ya
mitaa ya manispaa ya Shinyanga.
Mbali
ya kufanya usafi pia Naibu waziri Mpina alizindua kampeni ya upandaji miti
katika manispaa ya Shinyanga kwa kupanda miti kwenye shule ya msingi Ibinzamata
ambapo alitoa wito kwa wakazi wa manispaa hiyo kuhakikisha wanapanda miti mingi
ili kukabiliana na kasi ya uharibifu wa mazingira.
Alisema
ili kuhakikisha suala utunzaji wa mazingira linapewa kipaumbele ofisi yake itaanza
kufuatilia kila wilaya kuangaliaa uwajibikaji wa viongozi na watendaji wa
serikali katika suala la upandaji miti katika maeneo yao na kwa watakaobainika
kushindwa kuwajibika kikamilifu ataagiza wachukuliwe hatua za kinidhamu.
“Suala
la utunzaji wa mazingira siyo la hiari, ni amri na ni sheria, hivyo ye yote
anayekiuka anastahili kuchukuliwa hatua, na mimi nawaagiza viongozi na
watendaji wote wa serikali wasimamie kikamilifu zoezi la upandaji miti katika
maeneo yao, ni jukumu lao,”
“Tumepanga
kila kitaifa kila mwaka tupande miti ipatayo milioni 280 hii itapandwa katika
hekta 185,000, na kwa ngazi ya wilaya wapande miti milioni mbili, na ofisi
yangu itakwenda kila wilaya kukagua kuona miti iliyopandwa, maana kuna
watendaji huwa wanatuletea takwimu hewa,” alieleza Mpina.
Naibu waziri Mpina akizindua kampeni ya upandaji miti katika manispaa ya Shinyanga, hapa ni eneo la shule ya msingi Ibinzamata. |
Alisema
wilaya yo yote itakayoshindwa kutimiza lengo la kupanda miti milioni mbili kwa
mwaka watendaji wake wa serikali watachukuliwa hatua za kinidhamu na kwamba
dhamira ya Rais Magufuli ya Hapa Kazi Tu, haikuwa nguvu ya soda hivyo lazima
watu wahakikishe wanaitekeleza kwa vitendo.
Akiwahutubia
wananchi mara baada ya kumaliza kazi ya upandaji miti na kufanya usafi eneo la
kata ya Ibinzamata, Mpina aliwapongeza wakazi wa manispaa ya Shinyanga kwa jinsi
wanavyotekeleza vizuri suala la kufanya usafi na kuelezea kushangazwa na jinsi walivyojitokeza
kwa wingi katika kazi hiyo.
“Nichukue
fursa hii kukupongezeni kwa kazi nzuri, kwa mara ya kwanza nimejikuta nakosa
cha kufanya baada ya kila mtaa niliokwenda na ufagio wangu kukuta ukiwa msafi
kutokana na kukuta wananchi tayari wamemaliza kazi hiyo, hii ni tofauti na
mikoa mingine niliyowahi kutembelea,”
“Hapa
mmeonesha wazi jinsi gani mnaunga mkono agizo la Rais wetu, Dkt. Magufuli la
kufanya usafi kila jumamosi ya mwisho wa mwezi, hongereni sana na endeleeni na
moyo huu, maana suala la usafi ni jukumu lenu ninyi wenyewe na inasaidia
kuepukana na magonjwa ya mlipuko,” alieleza Mpina.
Akizungumzia
suala upandaji miti na utunzaji wa mazingira alisema maeneo mengi ya Tanzania
yanakabiliwa na kasi ya uharibifu wa mazingira kutokana na ongezeko kubwa la
shughuli za kibinadamu hali inayosababisha ongezeko mabadiliko ya tabia nchi.
Alisema
ili kukabiliana na hali hiyo ni jukumu la watanzania wenyewe kwa ushirikiano na
viongozi na watendaji wao wa serikali kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika
suala zima la utunzaji wa mazingira na upandaji miti kwa wingi kwenye maeneo
yote ili kurejesha hali ya uoto wa asili uliopotea maeneo mengi nchini.
Katika
hatua nyingine waziri Mpina amesema ofisi yake inajipanga kuupatia mkoa wa
Shinyanga mtambo wa kisasa wa kutengeneza mkaa unaotokana na mabaki ya takataka
na maganda ya miti ili kupunguza kasi ya matumizi ya nishati ya mkaa.
Alisema
tayari maombi ya kupatiwa kwa mtambo huo yaliyowasilishwa ofisini kwake na
viongozi wa wilaya ya Shinyanga yameanza kufanyiwa kazi na unatarajiwa
kupatikana mapema mwaka ujao na ikiwezekana utazinduliwa kipindi cha mbio za
mwenge utakapokuwa mkoani Shinyanga.
Awali
katika hotuba yake fupi mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro alisema
pamoja na wakazi wa wilaya yake kujitahidi katika suala la utunzaji wa
mazingira bado wanakabiliwa na changamoto ya ukatwaji miti kutokana na shughuli
ya uchomaji mkaa, na kwamba suluhisho lake ni kupata mtambo wa kutengeneza mkaa
mbadala.
Post a Comment