SERIKALI ya Kijiji cha Sanya Hoye, Wilaya ya Siha, mkoani Kilimanjaro imetangaza
adhabu ya kuchapwa viboko 15 na kulipa faini ya Sh. 50,000 kwa mkazi yeyote
atayekutwa baa nyakati za usiku, akiwa ameambatana na mtoto mwenye umri chini ya
miaka 18.
Uamuzi huo umefikiwa juzi na wakazi wa kijiji hicho, katika mkutano
uliofanyika Wilayani hapa.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Sanya Hoye, Mosses Munuo, alisema wapitisha azimio
la kutoa adhabu ya viboko na faini kwa kuwa ni malezi mabaya ya wazazi au
walezi, baada ya wanafunzi kutoka shule.
“Kwenda baa na watoto nyakati za jioni au wakati wa kazi, huo ni ukatili na
ni kinyume kabisa cha haki za watoto,” alisema Munuo.
“Kimsingi, jambo hili la baadhi ya wazazi au walezi kwenda baa na watoto na
kukaa nao wakati mwingine hadi saa 3 mpaka saa 5 usiku halikubaliki.
Ndio maana wananchi wamesema watakaokutwa hatua zichukuliwe,” alisema.
Munuo alisema hali hiyo kwa sasa ni tatizo sugu kwa baadhi ya wakazi wa
kijiji hicho, hivyo kusababisha ongezeko la watoto wanaoishi katika mazingira
hatarishi na magumu.
Ulevi, pia, umesababisha watoto wengine kuachwa nyumbani bila ya uangalizi
wowote, alisema Mwenyekiti huyo.
“Wakati wa jioni watoto wanastahili kuoga, kupumzika na baadaye kurejea yale waliyofundishwa darasani,” alisema Munuo na kuongeza:
“Sasa hawa wanaobeba watoto mgongoni na kwenda nao baa, wananchi wangu na
hata mimi mwenyewe hatuliafiki. Na ndio maana wakataka tuanze kuchukua
hatua.”
Serikali ya kijiji hicho pia imepiga marufuku uuzwaji pombe nyakati za kazi,
na kutoa amri kwa baa zote kuanza biashara saa 9:00 alasiri kila siku na
kuzifunga ifikapo saa 5:00 usiku.
Mei 12, mwaka huu wakazi zaidi ya 200 wa Kata ya Karansi wilayani humo,
wakiwa katika mkutano ulioandaliwa na wazee wa mila wa kabila la Wameru, nao
walipitisha uamuzi wa kuacharazwa viboko 60 hadi 70, wanaume watakaovaa suruali
chini ya kiuno na wanawake watakaokutwa wamevaa sketi fupi.
Source: Nipashe Newspapers.
Post a Comment