Bango lenye salaam za kuwakaribisha wageni eneo la mkutano katika msikiti wa Latif uliopo katika kijiji cha Nsalala kata ya Tinde wilayani Shinyanga. |
Kiongozi mkuu wa Jumuiya ya Waislamu Waahmadiyya Tanzania, Maulana, Sheikh Tahir Mahamood Chaudhry akitoa tamko la kulaani mauaji yaliyotokea katika nyumba ya Ibada jijini Mwanza. |
JUMUIYA
ya Waislamu Waahmadiyya nchini imelaani vikali tukio la mauaji yaliyotokea
katika msikiti wa Ibanda kata ya Mkolani wilayani Nyamagana mkoani Mwanza na
kuiomba serikali ihakikishe inawasaka na kuwakamata watu wote waliohusika na
mauaji hayo ya kinyama.
Tamko
hilo limetolewa na Kiongozi mkuu wa Jumuiya ya Ahmadiyya nchini, Maulana
Sheikh Tahir Mahamood Chaudhry alipokuwa akifunga mkutano wa mwaka uliofanyika
katika kijiji cha Nsalala kata ya Tinde wilayani Shinyanga mkoani humo.
Masjid Latif Ahmadiyya Muslim Jamaat Msalala. |
Sehemu ya waumini kutoka maeneo mbalimbali mkoani Shinyanga na mikoa jirani wakisikiliza hotuba za viongozi katika mkutano huo. |
Mkutano
huo uliowashirikisha pia viongozi wakuu wa kiserikali mkoani Shinyanga ulijadili
mambo mbalimbali ikiwemo umuhimu wa waumini wa kiislamu kudumisha hali ya amani
na utulivu nchini kwa kuzingatia mafundisho ya kitabu chao Qur – ani na mafundisho ya
Mtume Muhammad (S.A.W).
Akizungumzia
mauaji yaliyotokea msikitini hivi karibuni alisema, kitendo kilichofanyika
kinastahili kulaaniwa na kila binadamu mpenda amani na kwamba waliotekeleza
mauaji hayo si waumini wa kweli wa kiislamu kwa vile daima dini ya kiislamu
huhimiza suala la amani, salama na upendo miongoni mwa binadamu wote.
Mmoja wa viongozi wa Jumuiya ya Waahmadiyya, ambaye ni Sheikh wa mkoa wa Morogoro, Sheikh Asif Mahmood Butt akitoa nasaha zake katika mkutano huo wa mwaka. |
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Nsalala, Sandeko Machongo akitoa nasaha zake wa washiriki wa mkutano huo. |
“Jumuiya
ya Waislamu Waahmadiyya hapa nchini tunaungana na watanzania wengine kulaani
vikali mauaji yaliyotokea katika nyumba ya ibada kule jijini Mwanza, na tunaiomba
serikali iwatafute wale wote waliohusika na mauaji hayo ili waweze kukamatwa na kuchukuliwa
hatua kali za kisheria,”
“Daima
uislamu haukubaliani na vitendo vya kigaidi vinavyotekelezwa kwa kivuli cha dini
yetu, maana ya neno uislamu ni amani na salama, hivyo ni kosa kubwa kwa
binadamu ye yote kumwaga damu ya mwingine kwa kisingizio eti cha Jihad, jihad
siyo kuua watu, ni kufikisha neno la amani kwa walimwengu wote,” alieleza
Sheikh Chaudhry.
Akifafanua
alisema mafundisho ya uislamu yaliyomo ndani ya kitabu kitukufu cha Qur - ani
yanahimiza suala la binadamu kuheshimiana, lakini pia inakatazwa kuwalazimisha kwa
nguvu watu wengine kuingia katika uislamu bila ya hiari yao na kwamba mwenyezi
mungu anamchukia sana mtu anayetoa roho ya binadamu mwenzake pasipo sababu.
Kwa
upande mwingine kiongozi huyo alitoa wito kwa wakazi wa mkoa wa Shinyanga kujiunga
na Jumuiya hiyo na kwamba lengo kuu la uwepo wake hapa nchini ni kuendeleza mafundisho yote
yaliyokuwa yakifundishwa na mtume Muhammad (S.A.W) kwa kufuata kitabu kitukufu cha Qur-ani.
“Lengo
la
Jumuiya ya Ahmadiyya ni kuhakikisha watu wote wanafikishiwa ujumbe wa
neno
la mungu, na kuhimiza suala la kudumisha hali ya amani na utulivu,
popote
pasipokuwa na amani na utulivu hakuna maendeleo yatakayofanyika, lakini
pia tumekuwa tukisaidia misaada mbalimbali ya kijamii ikiwemo
uchimbaji wa visima vya maji,” alieleza.
Wawakilishi kutoka Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi. |
Kiongozi Mkuu wa Jumuiya ya Waislamu Waahmadiyya, Maulana Sheikh Tahir Mahamood Chaudhry akiwa pamoja na mgeni rasmi, mwakilishi wa mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Mohamed Mchiya. |
Mmoja wa viongozi wa Jumuiya ya Waislamu Waahamadiyya nchini, Sheikh Abdulrahman Ame akitoa ujumbe kwa waumuni waliohudhuria mkutano mkuu wa mwaka. |
Awali
katika hotuba yake ya ufunguzi mgeni rasmi katika mkutano huo, Mohamed Mchiya
aliyemwakilisha kaimu mkuu wa mkoa wa Shinyanga, John Mongella alisema serikali
nchini inatambua michango mbalimbali ya kijamii inayotolewa na madhehebu ya kidini
hapa nchini ambayo imechangia kupunguza matatizo miongoni mwa jamii.
Hata
hivyo alisema pamoja na hali hiyo serikali daima inawahimiza waumini wa
madhehebu yote yaliyopo nchini kuishi kwa kuvumiliana ili kuweza kudumisha hali
ya amani na utulivu iliyopo na kwamba kila kiongozi wa kidini ahakikishe dini
yake haitumiki katika masuala ya kisiasa kitendo ambacho ni kinyume na sheria za
nchi.
“Nyote mnafahamu ya kuwa Serikali ya Tanzania
haina dini, bali Watanzania ndio wenye imani mbalimbali za dini. Serikali ina wajibu wa kuziheshimu dini hizo
kwa mujibu wa katiba ya nchi, na tunaamini kwamba jambo hili la kutoa uhuru wa kuabudu
limechangia sana katika amani ya nchi yetu,”
“Ninakuhakikishieni kwamba Serikali yenu ya
Tanzania itabaki na msimamo huu daima wa kuhakikisha kila mtanzania yuko huru katika
kuamini na kuabudu jinsi apendavyo maadamu tu havunji sheria za nchi zilizopo wala
kusababisha shida kwa watu wengine na kila mtu ajiepushe na vitendo vya kigaidi
kwa lengo la kuihami dini yake,” alieleza Mchiya.
Aidha aliipongeza Jumuiya hiyo kwa mchango wake
wa huduma za kijamii inaoutoa ikiwemo utekelezaji wa mradi wake wa “Water for
Life” unaoshughulikia suala la uchimbaji na ukarabati wa visima vya maji safi
na salama katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na Dodoma ambapo kwa
mkoa wa Shinyanga watachimba visima 30.
Rais wa Tawi la Jumuiya ya Waahmadiyya - Tawi la Nhumbili, Shabani Mgeja. |
Rais wa Tawi la Jumuiya ya Waahmadiyya - Tawi la Butigu, Rashidi Peter akitoa nasaha zake. |
Rais wa Tawi la Jumuiya ya Ahmadiyya - Kata ya Kijiji cha Kasomela, Kinamapula - Kahama, Iddy Paulo. |
Kwa
upande wao marais wa matawi ya Jumuiya ya Ahmadiyya kutoka mkoani Shinyanga,
Rashid Peter (Tawi la kijiji cha Butwigu), Iddy Paulo (Kasomela) na Shabani
Mgeja (Nhumbili) waliishukuru Jumuiya hiyo kwa mchango wanaoutoa ikiwemo elimu
ya dini inayosaidia vijana wengi kushiriki ibada kikamilifu.
Post a Comment