Mbunge wa
Kahama aliyemaliza muda wake, James Lembeli amekataa kubadili msimamo wake wa
kutogombea ubunge kupitia CCM akisema atagombea nafasi hiyo kupitia chama
kingine.
Akizungumza
mjini hapa jana, Lembeli alisema hawezi kubadili msimamo wake wa kuondoka CCM,
kutokana na masharti mazito ya kimila aliyopewa kabla ya kutangaza kuondoka
katika chama hicho.
Baada ya uamuzi
wake, watu mbalimbali, wakiwamo maofisa wa Serikali na wafanyabiashara
waliahidi kumsaidia hata nguvu ya kifedha, wakimtaka atengue uamuzi wake
achukue fomu katika Jimbo la Kahama Mjini.
Alisema hawezi
kukiuka masharti ya kimila kwa kuwa yeye ni mtoto wa chifu. Mtoto huyo wa Chifu
Daud Lembeli alisema kabla ya kutoa uamuzi huo alikaa na mama yake mzazi, Maria
Kalembo kuanzia saa 10 jioni hadi saa nane usiku akizungumzia suala hilo hadi
walipokubaliana.
Alisema baada
ya mama yake kukubali na kutoa baraka za kuhama CCM, alipigiwa ngoma za kimila
za Waswezi, ambazo hutumika kutoa baraka katika imani za kichifu akisema ndizo
zilizohitimisha fursa za kugombea kwake ubunge kupitia chama hicho.
“Najisikia
amani kubwa kuondoka CCM, kabla sijachukua uamuzi huu nilikuwa nikiishi kwa
presha, hivi sasa nipo huru, niacheni tu kama ni ubunge sikuzaliwa nao na
unaweza kuishi bila ubunge na maisha yakawa mazuri,” alisema Lembeli.
Ilivyokuwa
Juzi, Lembeli
alifika katika Ofisi ya CCM Wilaya ya Kahama na kutangaza kuwa hawezi kugombea kupitia
chama hicho kwa kuwa kimejaa rushwa na matukio ya wagombea kugawa kadi kwa
wanachama ili wachaguliwe.
Mwenyekiti wa
CCM Wilaya ya Kahama, Mabala Mlolwa alielezea kusikitishwa na uamuzi huo wa
Lembeli kuamua kuhama bila kushauriana na uongozi wa wilaya.
Alisema CCM
inatambua mchango mkubwa aliotoa katika miaka 10 ya uongozi wake na
imeshangazwa na tukio hilo.
Mwenyekiti wa
CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja alisema pamoja na kulisikia suala hilo,
hivi sasa yupo mapumzikoni kisiasa kutokana na dhoruba kubwa ya kitaifa
waliyoipata katika mchakato wa uteuzi wa mgombea urais.
“Niacheni
kwanza nipumzike suala hilo nalisikia lakini muda mwingi sikuwapo. Najua suala
la Lembeli kuhama litaibomoa CCM Kahama, ataondoka na wengi lakini mimi
sizungumzi lolote juu ya hilo,” alisema Mgeja.
Chanzo:
Mwananchi News
Post a Comment