Kamanda wa TAKUKURU mkoani Shinyanga, Gasto Mkono akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Shinyanga imewakamata na kuwafikisha mahakamani watumishi watatu wa Hospitali binafsi inayomilikiwa na Kanisa la AIC Shinyanga wakituhumiwa kwa kosa la kuisababishia hasara serikali kiasi cha shilingi milioni 63.4.


Watumishi waliofikishwa mahakamani ni pamoja na aliyekuwa mganga mkuu wa hospitali hiyo, Dkt. Elimeleki Katani, wakuu wa idara ya uhasibu, Hamisi Batano na Samson Maselle.

Watumishi hao wote kwa pamoja mbali ya mashitaka ya kuisababishia hasara serikali pia wanashitakiwa kwa makosa ya matumizi mabaya ya madaraka yao ikiwemo matumizi mabaya ya fedha ya ruzuku inayotolewa na serikali.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari na OfisaUhusiano na habari wa TAKUKURU makao makuu Mussa Misalaba, watumishi hao wanashitakiwa kwa makosa manne ikiwemo kulipa mishahara hewa na kuwasilisha michango hewa NSSF kwa mstaafu aliyetajwa kwa jina la Dkt. Emmanuel Mwandu.



Waandishi wa habari wakipokea taarifa ya utendaji kazi za TAKUKURU Shinyanga kati ya Julai, 2016 na Machi, 2017.

Baadhi ya waandishi wa habari mjini Shinyanga wakitoka katika ofisi za TAKUKURU Shinyanga.
Misalaba alisema katika shitaka la kwanza washitakiwa hao wanadaiwa kati ya Juni 10,  2011 na Januari 1, 2016 walitumia madaraka yao vibaya kwa kushindwa kurejesha kwa mlipaji mkuu wa serikali mshahara wa mstaafu, Dkt. Emmanuel Mwandu kiasi cha shilingi 63,479,800.

Shitaka la pili inadaiwa washitakiwa hao kati ya Septemba 18, 2013 na Agosti 21, 2014 waliandaa na kupeleka katika Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kiasi cha shilingi 14,361,124 ikiwa ni michango ya mstaafu, Dkt. Emmanuel Mwandu.

Shitaka la tatu linamuhusu mshitakiwa Batano anayedaiwa kati ya Mei 30, 2011 na Januari 6, 2014 alitumia madaraka yake vibaya na kuandaa orodha ya malipo kama mshahara wa mstaafu Dkt. Emmanuel Mwandu kiasi cha shilingi 14,361,124 huku shitaka la nne la kuisababishia hasara serikali kiasi cha shilingi 63,479,800 likiwahusu washitakiwa wote.

Tayari washitakiwa wote wamesomewa mashitaka yao na mwendesha mashitaka wa TAKUKURU, Carson Nkya mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi, Rahimu Mushi na wamekana mashitaka yote ambapo kesi hiyo imeahirishwa mpaka Mei 3, mwaka huu itakapotajwa tena mahakamani hapo.  Washitakiwa wote wako nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana.

Wakati huo huo ofisi ya TAKUKURU mkoani Shinyanga imepokea jumla ya taarifa 36 za matukio ya rushwa yaliyoripotiwa ndani ya kipindi cha miezi tisa iliyopita (Julai 2016 hadi Machi 31, 2017) zikihusisha idara ya mahakama, polisi, ardhi, afya, elimu, taasisi binafsi, madini, biashara, michezo na siasa.

Akitoa taarifa ya utendaji kazi ya taasisi yake, Kamanda wa TAKUKURU mkoani Shinyanga, Gasto Mkono alisema tayari wanaendelea na uchunguzi wa kina juu ya taarifa zilizopokelewa kwa kufungua majalada ya uchunguzi kwa ajili ya kuchunguza taarifa zote zilizopokelewa.

Mbali ya kupokea taarifa za matukio ya rushwa pia TAKUKURU mkoani humo katika kipindi hicho cha miezi tisa imefanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi 114,479,838.28 kutoka idara za Afya, Elimu na kilimo zilizokuwa zitumike kinyume cha utaratibu ikiwemo ulipaji mishahara hewa.

“Katika kipindi cha miezi tisa iliyopita tumepokea taarifa 36 zinazohusiana na masuala ya rushwa na tayari tumefungua majalada 23 ya uchunguzi kuhusiana na taarifa hizo, taarifa hizi zinahusu upande wa idara za elimu, michezo, biashara na siasa, na tayari kesi tatu zimefikishwa mahakamani,”

“Lakini pia zipo kesi tisa zinazoendelea mahakamani zikihusisha idara za fedha katika halmashauri, afya, elimu na Jeshi la Polisi ambapo katika kipindi hiki tumeshinda kesi tatu huku tukishindwa kesi nne na kesi tisa bado zinaendelea kusikilizwa,” alieleza Mkono.

Aliendelea kueleza ofisi yake inaendelea na utafiti na udhibiti ya mianya ya rushwa katika idara mbalimbali za serikali na taasisi binafsi ikiwemo pia kufuatilia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri za manispaa na wilaya ili kubaini iwapo inatekelezwa kwa kiwango kinacholingana na fedha zilizotolewa.


Ofisi za TAKUKURU Shinyanga.

Aidha Kamanda huyo wa TAKUKURU aliwapongeza wakazi wa mkoa wa Shinyanga ikiwemo vyombo vya habari kwa msaada mkubwa wanaoutoa na kuweza kufanikisha kukabiliana na matukio ya rushwa katika idara mbalimbali za umma na hivyo kudhibiti upotevu wa fedha za serikali kwa njia ya ulipaji mishahara hewa.

“Tunawashukuru wakazi wa mkoa wa Shinyanga ikiwemo wana habari kwa msaada mkubwa wanaotupatia katika mapambano haya dhidi ya vitendo vya rushwa katika mkoa wetu, na tunawaomba wasichoke waendelee kutupatia taarifa mbalimbali zitakazosaidia kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wote,” alieleza Mkono.
Share this PostPin ThisShare on TumblrShare on Google PlusEmail This

Asante kwa kutembelea mtandao huu

Post a Comment

 
Top