Haya ni majeraha yanayotokana na shambulizi alilopokea mwananchi huyu kutoka kwa askari Magereza wa Gereza la Shinyanga. |
KATIKA hali
isiyokuwa ya kawaida mkazi wa kijiji cha Nhelegani manispaa ya Shinyanga
ameshambuliwa kwa kipigo na askari wa Jeshi la Magereza na kujeruhiwa vibaya
sehemu mbalimbali za mwili wake baada ya kugoma kuwapa askari hao soda na
biskuti.
Tukio hilo
la aina yake limetokea katika Gereza la wilaya ya
Shinyanga wakati mwananchi huyo aliyejitambulisha kwa jina la Lugenzi Maguta
(45) alipokwenda kumsalimia ndugu yake aliyeko mahabusu aliyemtaja kwa jina la
Mahushi Nangale.
Mbali ya
kushambuliwa kwa kipigo hadi kupasuka katika miguu yake yote miwili kutokana na
kupigwa virungu bado askari magereza hao wanadaiwa kumgeuzia kibao kwa
kumfungulia shitaka la kufanya fujo gerezani tuhuma ambazo alidai ni za uongo
kwa vile hakuna fujo yoyote iliyotokea.
Akizungumza
na waandishi wa habari wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya serikali,
Maguta alisema askari waliomshambulia waliokuwa wamevaa kiraia hawakuwa zamu
bali walikuwa nje ya gereza waliamua kumshambulia kwa madai walichukizwa na
kitendo chake cha kukataa kuacha soda na biskuti alizokuwa nazo.
“Baadaye
wale askari waliomba tusameheane lakini walielekezwa twende nao pamoja kituo
cha polisi na kama ni kusameheana tukaelewane huko huko, maana yule kiongozi
wao alisema tukielewana kienyeji mimi baadae naweza kuwageuka, tulikwenda hadi
kituoni na sote tukatoa maelezo yetu, na kisha nilipewa PF 3 kwenda kutibiwa,”
alieleza Magucha.
Alisema
baada ya kupewa fomu namba tatu aliongozana kwenda hospitali na askari wote
wanne wawili waliokuwa zamu na waliomshambulia kwa kipigo ambako baada ya
kupimwa fomu ilijazwa na kurudishwa polisi hata hivyo wakiwa wanarejea kituoni
askari wale walimlazimisha akaeleze kuwa hakuumia sana.
Kwa upande
wake msemaji wa Jeshi la Magereza mkoani Shinyanga, ACP Grace Massawe
alikanusha kuwepo kwa tukio lolote la kutokea fujo gerezani wala kushambuliwa
kwa mwananchi ye yote aliyekuwa amekwenda kumsalimia ndugu yake.
“Ndugu zangu
hapa ofisini hatuna taarifa zozote za kushambuliwa kwa raia gerezani au kutokea
fujo, taarifa hizi ndiyo kwanza nazisikia kutoka kwenu waandishi, nakushukuruni
sana tutalifanyia kazi suala hili mara moja, maana haturuhusu watu kupigwa
ovyo, achilia mbali raia wa kawaida awe mahabusu au mfungwa hawaruhusiwi
kupigwa,” alieleza Massawe.
Naye Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha hakuwa na taarifa zozote
kuhusiana na tukio hilo ambapo alisema atawasiliana na mkuu wa kituo cha polisi
wilaya (OCD) ili apate taarifa kamili na kama kweli limetokea ofisi yake
itafanya uchunguzi wa kina ili kubaini ukweli wake na sheria ichukue mkondo
wake kwa watakaobainika.
Post a Comment