VIONGOZI, watendaji na wanachama wa Chama cha
Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga wameaswa kutotegemea kushinda katika chaguzi zijazo
za serikali nchini kwa mbwembwe nyingi na hotuba za majukwaani bali ni kwa
kutekeleza kikamilifu kwa Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2010 – 2015.
Ushauri huo umetolewa juzi na mwenyekiti wa CCM
mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja wakati wa hafla fupi ya kukabidhi misaada kwa
ajili ya ujenzi wa kituo cha polisi katika kata ya Didia kinachojengwa kwa
nguvu ya wananchi ambapo viongozi mbalimbali wa CCM wakiwemo wa kitaifa
walichangia zaidi ya mifuko 120 na fedha taslimu shilingi milioni moja.
Mgeja alisema watanzania hawawezi kukubali
kuendelea kukichagua chama hicho iwapo hakitatekeleza kikamilifu ilani yake na
kwamba ufanisi wa utekelezaji wa ilani hiyo ni wana CCM sasa kuhakikisha
wanakisemea chama na kuwaondolea wananchi kero mbalimbali zinazowakabili.
“Wanachohitaji wananchi ni vitendo siyo maneno
au kupiga kelele, watanzania walitukabidhi kazi ya kuwaondolea kero mbalimbali
zilizopo katika maeneo yao, na wenzetu wapinzani walipewa kazi ya kupiga
kelele, ni muhimu sasa tuhakikishe tunautumia vizuri muda uliosalia kuelekea
uchaguzi mkuu wa serikali za mitaa kwa kufanya kazi kwa bidii,”
Mgeja alisema wakati huu uliosalia lazima tuwe
makini, wapo baadhi yetu kazi yao ni kupigana madongo wenyewe kwa wenyewe
badala ya kuwatumikia wananchi, na kutoa mfano wa baadhi ya wana CCM ambao kazi
yao ni kuwatungia uongo wenzao huku wakichonga viongozi watakaosimama katika
chaguzi zijazo.
“Tukumbuke kwamba wakati wa kampeni zijazo
wananchi watatupima kwa kazi tulizowafanyia na siyo kwa uhodari wa kupanga
maneno majukwaani, watanzania wanachohitaji ni maendeleo siyo hotuba tamutamu,
tufanye kazi kwa kuonesha vitendo kama walivyofanya wenzetu hawa katika ujenzi
wa kituo hiki cha polisi,”
“Muda huu sasa si wa kuendeleza makambi ya
uchaguzi, hapana ni muda adimu sana kwetu, tuna ahadi nyingi tulizowaahidi
wananchi wetu, lazima tuwe na majibu tujitahidi kukisemea chama chetu maana
hakina mjomba wala shangazi wa kukisemea, tukikaa kimya tutawapa nafasi wapinzani
wetu ya kuturushia makombora,”
“Bado kuna kero nyingi hasa maeneo ya vijijini,
muda bado unatosha, sasa tuhakikishe tunakwenda kwa wananchi, tuwasikilize na
tuchukue hatua pale panapostahili, tuache tabia ya kulalamika pale wananchi wanapotulalamikia
badala ya kushughulikia kero zao tunakimbilia kuwapakazia kuwa ni wapinzani,”
alieleza Mgeja.
Aliwaomba wana CCM wazingatie suala la ushindi
na maslahi na katika chaguzi zijazo kwa kuhakikisha wanajenga umoja miongoni
mwao wenyewe na kuwa na mshikamano wa dhati, badala ya kushughulikiana wenyewe
kwa wenyewe, watumie nguvu kubwa katika kutatua kero zilizoko kwa wananchi.
Katika hatua nyingine mwenyekiti huyo
aliupongeza uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga kwa jinsi
unavyotekeleza kwa ufanisi mkubwa ilani ya uchaguzi ya CCM ambapo imeweza
kuchangia kiasi cha shilingi milioni 15 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha polisi
na kituo cha afya, milioni tano zikiwa za kituo cha polisi.
Mwisho.
Post a Comment