Mamia ya wapiga kura wa Jimbo la Kisesa wakisalimiana na mbunge wao, Luhaga Mpina muda mfupi baada ya kukabidhiwa vifaa mbalimbali kwa ajili ya shughuli za uzalishaji mali. Hapa ni Kata ya Lubiga |
MBUNGE anayemaliza muda wake katika Jimbo la Kisesa wilaya ya Meatu mkoani
Simiyu, Luhaga Mpina (CCM) amepongezwa na wapiga kura wake kwa kitendo chake
cha kutekeleza ahadi zake alizozitoa mwaka 2010 baada ya kugawa vifaa
mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni 200.
Pongezi za wananchi hao wa Kisesa zimetolewa kwa nyakati tofauti katika
kata za Lubiga, Mwakisandu, Mwabusalu, Mwasengela, Sakasaka, Sanga Itenje,
Isengwa na Lingeka ambapo Mpina alikabidhi vifaa kwa vikundi vya wajasiliamali
wadogo na vile vya kilimo cha umwagiliaji.
Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na pampu 20 kwa ajili ya visima vifupi vya
maji, pampu 31 za kilimo cha umwagiliaji, mashine moja ya kuoshea magari kwa
kikundi cha vijana wanaoosha magari katika kata ya Mwandoya na pikipiki 30 kwa
vijana waendesha bodaboda.
Diwani wa Kata ya Lubiga, Juma Mpina (Kulia) akipokea vifaa kutoka kwa mbunge wa Jimbo la Kisesa, Luhaga Mpina (mwenye miwani) kwa ajili ya wajasiliamali wa kata yake. |
Vifaa vingine vilivyotolewa ni mashine mbili za kusindika mafuta ya
alizeti, mashine tano za kuchakata katani, baiskeli mbili za walemavu wa
viungo, vyerehani 50 kwa vikundi vya ushonaji, pikipiki tano kwa shule tano za
sekondari, vitanda sita vya kujifungulia wajawazito na kompyuta 10 na printa
nne kwa shule za sekondari.
Pia alikabidhi madawati 250 kwa ajili ya shule za sekondari zilizopo katika
jimbo la Kisesa ambapo alisema vifaa vyote alivyovitoa ni katika kukamilisha
ahadi zake alizowaahidi wapiga kura mwaka 2010 na kufafanua kuwa vifaa hivyo
havitokani na mfuko wa jimbo bali amevikusanya kutoka kwa marafiki zake na
sehemu ya mshahara wake.
“Nitahadharishe kitu kimoja, vifaa hivi sivitoi kama rushwa, bali ni ahadi
nilizozitoa kwenu, huko nyuma tumekabidhi vitu mbalimbali na hivi vya leo ni
katika kukakamilisha ahadi zangu kwenu, sehemu kubwa nimechangiwa na rafiki
zangu ikiwemo watu SIDO waliotoa mashine za katani na hizi za kusindika mafuta
ya alizeti,” alieleza Mpina.
Wakati huo huo mbunge huyo amewashukuru wanachama wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) katika Jimbo la Kisesa kwa kitendo chao cha kumpitisha bila kupingwa
katika mchakato wa kura za maoni ambapo hakuna mwana CCM ye yote aliyejitokeza
kumpinga.
Mpina alitoa shukrani hizo juzi katika mikutano ya hadhara iliyofanyika kwa
nyakati tofauti kwenye kata mbalimbali jimboni Kisesa iliyoambatana na shughuli
ya kukabidhi vifaa hivyo kwa vikundi vya wajasiliamali na vile ya kilimo cha
umwagiliaji na vya watumiaji maji.
Mpina alisema hatua ya wana CCM kutokuchukua fomu kuwania kiti cha ubunge
katika jimbo hilo imeonesha wazi bado wana imani naye hali iliyoonesha wazi
wanathamini kazi kubwa alizowafanyia katika kipindi cha miaka 10 ya ubunge wake
ambapo jimbo la Kisesa limepiga hatua kubwa katika suala zima la maendeleo.
“Nichukue fursa hii kuwashukuru sana wanachama wenzangu wa CCM kwa imani
yenu kubwa mliyonionesha, kwa kweli nimeona jinsi gani mnavyothamini mchango
wangu katika kuwatumikieni, na mimi naomba nitoe ahadi kwenu kwamba tarajieni
mambo makubwa zaidi katika kipindi kijacho iwapo nitashinda hapo Oktoba 25,
mwaka huu,”
“Jambo kubwa ninalowaomba jitokezeni kwa wingi siku ya upigaji kura Oktoba
25, mwaka huu ili muudhihirishie umma kwamba jimbo la Kisesa daima litaendelea
kuongozwa na wabunge wa CCM, binafsi sioni mpinzani kutoka kwa wenzetu wa vyama
upinzani, aliyeteuliwa na CHADEMA nimekuwa nikimwangusha tangu 2005, sina hofu
naye,” alieleza Mpina.
PICHA ZAIDI ZA MAKABIDHIANO YA VIFAA MBALIMBALI KWA VIKUNDI VYA WAJASILIAMALI JIMBO LA KISESA.
Mama huyu anaonesha jinsi gani alivyofurahishwa na kitendo cha mbunge wake kumkomboa kwa kumpatia vitendea kazi, kikundi chake kilikabidhiwa cherehani ya kushonea. |
Wakazi wa kata ya Lingeka pia hawakusahaulika. |
Post a Comment