Chama cha ACT-Wazalendo kimesema kila
mwanachama anapaswa kuwaunga mkono wagombea watakaopitishwa na chama hicho
katika nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu ujao, kwani kinyume chake ni
kukisaliti na adhabu yake ni kufukuzwa.
Mwenyekiti wa chama hicho, Anna Mghwira alisema
mwishoni mwa juma kuwa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu,
chama hicho kinahitaji nguvu za pamoja.
“Sisi bado hatujajiunga na Ukawa, hivyo
wanachama wetu wanapaswa kulitambua hilo na kuepuka kushiriki kwenye ushawishi
wa kufanya kampeni za wagombea wa vyama vingine.
Hata kwenye katiba yetu tunasema sasa tunalenga
zaidi katika kujiimarisha ili kutoa ushindani mzuri wa kisiasa katika uchaguzi
huu,” alisema.
Katiba ya ACT, imeeleza wazi kuwa pamoja na
sababu nyingine na kwa mujibu wa kanuni zitakazotungwa na Halmashauri Kuu,
mwanachama yeyote ambaye atasaidia kushawishi, kujiunga, kutoa tamko la kuunga
mkono chama kingine au mgombea wakati chama kimeweka mgombea wake kwa mujibu wa
sheria za nchi, atakuwa amepoteza uanachama wake.
ACT- Wazalendo tayari imetoa ilani yake ya
uchaguzi ikionyesha kwamba iwapo itaingia madarakani, itawajibika kwa wananchi
kwa kuweka kipaumbele katika maeneo manne ambayo ni hifadhi ya jamii, uchumi
shirikishi wenye kuzalisha ajira nyingi na bora, afya na elimu.
Kauli hiyo ya ACT linakuja huku kambi ya vyama
kadhaa vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ikiwa
kwenye mchakato wa kuunganisha nguvu ili kusimamisha mgombea mmoja wa urais na
kuachiana majimbo katika baadhi ya maeneo.
Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia
amewahi kunukuliwa akisema kuwa umoja huo unaoundwa na Chadema, CUF,
NCCR-Mageuzi na NLD umehamishia nguvu zake kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Mbatia alisema tayari umoja huo umeunda kamati
maalumu kutafuta namna ya kumsimamisha mgombea mmoja wa urais na kuachiana
majimbo.
Mbatia alisema tayari umoja huo umeunda kamati
maalumu kutafuta namna ya kumsimamisha mgombea mmoja wa urais na kuachiana
majimbo.
Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa
NCCR-Mageuzi, alisema tayari kamati zimeundwa na zinaendelea na kazi ya
kuratibu mpango huo mahsusi, unaolenga kuiondoa CCM madarakani.
“Lengo letu ni kuhakikisha Ukawa ina nguvu ya
kushika dola katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 na katika mpango huo, vyama
vitaachiana majimbo na viti vya udiwani kulingana na nguvu ya chama katika
sehemu husika,” alisema.
Mkakati huo uliopangwa na Ukawa, unaelezwa na
wachambuzi wa masuala ya kisiasa kuwa ni kombora kwa CCM, kwani endapo
utafanikiwa, utakiweka chama hicho tawala katika wakati mgumu katika Uchaguzi
Mkuu uliopangawa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Source: Mwananchi
Post a Comment