WAZIRI
MKUU Mizengo Pinda amekataa ombi la wananchi wa jimbo lake la uchaguzi la
Katavi la kumtaka agombee tena ubunge katika jimbo hilo ili kuendeleza mipango mbalimbali ya maendeleo aliyoianzisha.
Akizungumza
baada ya Ibada ya Jumapili katika kigango cha Kanisa Katoliki cha Kibaoni
wilayani Mlele (Jumapili, Julai 19, 2015), Waziri Mkuu Pinda amesema
anamshukuru Mungu kwa nafasi aliyopewa ya kulitumikia Taifa akiwa Waziri Mkuu
kwa miaka minane na anaamini wakati umefika wa yeye kuwaachia wengine nafasi ya
ubunge wa jimbo la Katavi.
Amesema
yeye ataendelea kuwa karibu na wananchi wa Katavi wakati wote na kwa vile
atakuwa na muda wa kutosha atashiriki kikamilifu katika mikakati mbalimbali ya
kuwaletea maendeleo wananchi ili waweze kujikwamua kutoka kwenye umaskini.
Mheshimiwa Pinda aliwaasa wananchi wa jimbo la Katavi wawe makini katika kuchagua mbunge na madiwani na kamwe watoa rushwa na wabadhirifu wasipewe nafasi katika uchaguzi ujao.
Akimshukuru
Mheshimiwa Waziri Mkuu, Paroko wa Parokia ya Usevya wilayani Mlele, Padri
Aloyce Nchimbi aliwaasa wananchi wa Wilaya ya Mlele kumuenzi Mheshimiwa Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda hata atakapokuwa amestaafu kwani bado watahitaji busara na
uzoefu wake katika kujiletea maendeleo.
Waziri
Mkuu yuko kijijini kwake Kibaoni, wilayani Mlele kwa ajili ya mapumziko mafupi.
Leo
saa 10 jioni ndiyo mwisho wa kurejesha fomu za ubunge ndani ya Chama cha
Mapinduzi (CCM).
IMETOLEWA
NA
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JULAI 19, 2015.
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JULAI 19, 2015.
Post a Comment