Naibu waziri akitoa pongezi kwa watendaji wa KASHWASA eneo la mradi wa kupeleka maji kutoka Ziwa Victoria kwenda wilayani Kishapu mkoani Shinyanga. |
Mheshimiwa Naibu waziri kazi ya kupeleka maji wilaya ya Kishapu ndivyo inavyoendelea hivi. Anaeleza Mhandisi Laurence Wasala (kushoto) anayesikiliza ni Naibu waziri wa Maji, Amos Makala. |
Naibu waziri wa Maji, Amos Makala (mwenye suti nyeusi) na mkuu wa wilaya ya Kishapu, Wilson Nkhambaku (mwenye shati la draft) wakijionea jinsi kazi inavyoendelea. |
HATIMAYE
serikali imeanza kutekeleza ahadi iliyotolewa na waziri wa Maji nchini, Profesa
Jumanne Maghembe ya kuwapatia wakazi wa wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga maji
kutoka mradi mkubwa wa maji ya Ziwa Victoria baada ya kazi ya utandazaji wa
bomba za maji kwenda wilayani humo kuanza hivi karibuni.
Mradi huo
ambao ni miongoni mwa miradi mikubwa nchini unaotekelezwa kwa fedha za ndani
unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 13.5 utakapokamilika na
unatekelezwa kwa kuwatumia watumishi wa Mamlaka ya Kusambaza Maji katika miji
ya Kahama na Shinyanga (KASHWASA).
Kwa mujibu
wa taarifa iliyotolewa kwa Naibu waziri
wa Maji, Amos Makala aliyekuwa katika ziara ya siku moja mkoani Shinyanga,
utekelezwaji wa mradi huo unatokana na ahadi iliyotolewa na waziri maji nchini,
Profesa Jumanne kwa wananchi wa wilaya ya Kishapu alipotembelea wilaya hiyo
mnamo mwezi Machi, 2014.
Waziri
Maghembe akiwa mkoani Shinyanga alipokea taarifa za kiufundi zilizoonesha
kuwepo kwa uwezekano mkubwa wa kupanua mradi mkubwa wa maji wa Ziwa Victoria
kuanzia eneo la Old Shinyanga kwenye wilayani Kishapu ambapo pia kwa kuanzia
vijiji 12 kando ya mtandao wa bomba hilo vitanufaika.
Akisoma
taarifa yake kwa Naibu waziri, Kaimu mkurugenzi wa KASHWASA, Mhandisi Laurence
Wasala ilisema mapitio ya usanifu wa mradi huo ulifanywa na Mhandisi mshauri
GIBB East Africa mnamo mwaka 2008 ili kuona uwezekano wa kuunganishwa wilaya
hiyo kwa gharama ndogo na kutumia watumishi wa ndani.
“Mheshimiwa
Naibu waziri, kazi za upimaji na usanifu ilianza mwezi Mei 2014 na kukamilika
mwezi Agosti 2014, ujenzi wa mradi ulianza rasmi mwanzoni mwa mwezi Februari,
2015 baada ya kukamilika kwa mchakato wa ununuzi wa mabomba, viungio na baadhi
ya vitendea kazi,”
“Kwa ujumla
ujenzi wa mradi huu umefikia kiasi cha asilimia 30 na inatarajiwa ifikapo
mwishoni mwa mwezi Septemba, 2015 utakuwa umekamilika kwa upande wa eneo la Old
Shinyanga na Mgodi wa Almasi wa Mwadui, kazi zote zinatekelezwa na watumishi wa
ndani wa KASHWASA na kutoka kwa mzabuni wa bomba,” alieleza Mhandisi Wasala.
Akifafanua
Wasala alitaja hatua iliyokwisha fikiwa katika ujenzi wa mradi huo mpaka hivi
sasa ikiwemo usafishaji wa njia ya bomba yenye urefu wa mita 20,000 kati ya
mita 22,800 ambayo imekamilika.
Pia
uchimbaji wa mtaro wa kulaza bomba wenye urefu wa mita 21,000 kati ya mita
22,800 hadi Williamson Diamonds Ltd Mwadui, na mita 63,000 hadi mji wa Kishapu
pia umekamilika.
Ulazaji na
ufungaji wa bomba umekamilika urefu wa mita 12,966 kati ya mita 21,000
zilizochimbwa, ulipuaji wa miamba katika eneo la Ikonongo umekamilika na kwa
sasa unaendelea katika maeneo mengine.
Aidha jumla
ya valvu tano za kuondolea hewa kwenye bomba (air valves) zimefungwa kati ya 12, valvu moja ya kuondolea uchafu
kwenye bomba (washout valves) kati ya
sita imefungwa na bends tatu kati ya
19 zimekamilika kufungwa.
Kwa upande
wake Naibu waziri Makala aliwapongeza watumishi wa KASHWASA kwa juhudi na kazi
kubwa wanazozifanya kuhakikisha mradi huo unakamilika katika muda na wakati
uliopangwa ambapo aliahidi kufanyia kazi changamoto za hapa na pale
zinazojitokeza ikiwemo upatikanaji wa kibali cha kupitisha bomba eneo la jeshi
na reli.
“Binafsi
nipongeze juhudi kubwa zinazofanywa na wizara pamoja na wenzetu wa KASHWASA,
niseme tu kwa kazi kubwa hii inayofanywa na serikali wananchi waendelee
kuwa na imani na serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kama jinsi alivyoahidi
waziri Maghembe, ni wazi maji haya yatafika Kishapu kwa wakati,” alieleza
Makala.
Kwa upande
wake mkuu wa wilaya ya Kishapu, Wilson Nkhambaku alisema mara baada ya maji
kufika katika makao makuu ya wilaya, serikali ya wilaya itashirikiana na
halmashauri yake ya Kishapu kusambaza huduma ya maji katika vijiji vyote jirani
ya maeneo ya mtandao wa bomba kutokea Old Shinyanga.
Post a Comment