BALOZI SEIF ALI IDDI |
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif
Ali Iddi amesema atakuwa bega kwa bega na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Bernard Membe katika mbio zake za kuwania urais.
Membe, ambaye amekuwa akizungumzia kutangaza
nia kuwania urais kama “kusubiri kuoteshwa”, ameshasema siku ikifika atachukua
fomu lakini anatarajia kutangaza rasmi mpango wake jimboni kwake Mtama, sasa
anaungwa mkono na mmoja kati ya viongozi wa juu wa Serikali na CCM kutoka
Zanzibar ambayo ina nafasi ya pekee katika kuamua mgombea urais wa chama hicho.
Balozi Iddi ambaye amewahi kuwa Naibu Waziri wa
Mambo ya Nje tangu mwaka 2006, alitoa msimamo huo wa kwanza kwa kiongozi wa juu
wa Serikali jana jijini Dar es Salaam wakati akifunga mkutano wa siku tatu wa
mabalozi wa Tanzania katika nchi mbalimbali, akimwakilisha Rais wa Zanzibar, Dk
Ali Mohamed Shein aliyeshindwa kuhudhuria kutokana na msiba wa dada yake.
“Namtakia Membe safari njema na ninamuahidi
kuwa tutakuwa naye bega kwa bega katika safari hii ngumu kwake,” alisema Balozi
Idi bila ya kutaja neno urais.
Kauli ya makamu huyo wa Rais ilikuja baada ya
Membe, ambaye amesema wakati ukifika atachukua fomu za kugombea urais, kuwaaga
mabaozi hao kabla ya kumkaribisha mgeni huyo rasmi.
Katika hotuba yake ya mwisho kwa mabalozi hao,
Membe aliweka wazi kuwa hatarudi tena bungeni akiwa waziri baada ya kuongoza
wizara hiyo kwa takriban miaka minane.
Alirejea kauli yake ambayo amekuwa akiitoa mara
kwa mara kuwa ameamua kuondoka wizarani hapo ili kujaribu nafasi kubwa zaidi
katika siasa na kuwakaribisha bungeni mjini Dodoma ili wasikilize hotuba ya
bajeti yake ya mwisho.
“Njooni msikilize bajeti yangu ya mwisho kama
waziri kwani sitarajii tena kuingia bungeni kama waziri labda kwa nafasi
nyingine ambayo ni ngumu sana,” alisema Membe akiwaaga mabalozi 36.
Waziri huyo pia alitumia nafasi hiyo kuwaomba
mabalozi hao kuitangaza Tanzania nje, huku akitahadharisha kuhusu mabadiliko ya
kisiasa yanayoendelea kutokea katika baadhi ya mataifa barani Afrika.
Alisema nchini Madagascar, Bunge limepiga kura
ya kutokuwa na imani na rais na kuilazimu Mahakama ya Katiba kufanya uamuzi
kuhusu suala hilo.
“Rais (Hery) Rajaonarimampianina amepigiwa kura
121 kati ya 125. Sitarajii kama kama Mahakama itaamua tofauti na matakwa ya
Bunge.
Hukumu inatarajiwa kutolewa leo (jana) baada ya
kura hizo kupigwa jana (juzi),” alisema Waziri Membe.
Pamoja na kumuunga mkono Membe, Balozi Iddi
aliwataka mabalozi hao kutumia vyema nafasi walizonazo katika kuitangaza
Tanzania ili nchi inufaike na fursa za kiuchumi zilizopo huko walipo.
Chanzo: Mwananchi News Paper
Post a Comment