Ndani ya jumba hili la bunge, Wajumbe wa bunge maalum la Katiba (BMK) walipinga vikali muundo wa serikali tatu kwa madai utakuwa na gharama kubwa. |
Kipindi
kama hiki, mwaka jana kulikuwa na mnyukano mkubwa wa maoni kuhusiana na
pendekezo la Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwamba muundo wa Muungano wa Tanzania
Bara na Zanzibar uwe wa Serikali tatu.
NDANI YA RASIMU HII ILIPENDEKEZWA MUUNDO WA SERIKALI TATU ILI KUPUNGUZA GHARAMA KUBWA ZA UENDESHAJI WA SERIKALI |
Katika
Bunge Maalumu la Katiba, wajumbe wengi hasa kutoka CCM, walipinga pendekezo
hilo kwa maelezo kwamba ni gharama kuendesha serikali tatu katika nchi maskini
kama Tanzania na kwamba pendekezo hilo lililenga kugawana vyeo tu na si
kuimarisha utendaji.
Lakini
safari hii, madiwani na wabunge wengi wa CCM wako mstari wa mbele kuridhia
pendekezo la Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), la kuongeza gharama za uendeshaji
wa Bunge kwa kuongeza majimbo 42.
Nyongeza
hiyo ina maana kwamba wabunge wataongezeka pamoja na mishahara yao, posho,
fedha za mfuko wa jimbo na hata kiinua mgongo. Kiasi cha jumla ya Sh3.382
bilioni kitaongezeka kila mwaka kwa ajili ya kugharamia wabunge hiyo ikiwa ni
mbali ya mafao yao baada ya ubunge.
Mshahara
wa mbunge mmoja pamoja na matumizi mengine madogomadogo ni jumla ya Sh11
milioni. Hivyo, kwa miezi 12 mbunge mmoja atalipwa Sh132 milioni na kwa wabunge
42 itakuwa Sh554 milioni.
Kila
mbunge atakuwa akilipwa Sh80,000 ikiwa ni posho ya kujikimu anapokuwa nje jimbo
lake, posho ya kikao Sh200,000 na posho ya mafuta ya gari Sh50,000 jumla ni Sh330,000
kwa siku.
Posho
hizo akilipwa akiwa kwenye vikao vya Bunge; siku 56 za Bunge la Bajeti mjini
Dodoma; siku 14 kikao cha Februari; siku 14 za vikao vya Kamati za Bunge jijini
Dar es Salaam; siku 14 kikao cha Oktoba jumla ya siku 98, atalipwa Sh32,340,000.
Malipo kwa wabunge 42 yatakuwa Sh1.35 bilioni.
Aidha,
kila mbunge ana mfuko wa jimbo wa kati ya Sh35 milioni na Sh45milioni kulingana
na ukubwa wa jimbo, kwa ajili ya maendeleo ya jimbo lake.
Hivyo, ikiwa kila
mmoja atapewa wastani wa Sh35 milioni katika jimbo, kwa wabunge hao 42 itakuwa
Sh1.47 bilioni.
Kwa
hiyo, bila kuingiza posho za safari za ndani au nje akiwa na kamati ya Bunge,
misamaha ya kodi, mafao na posho za semina, kwa mwaka wabunge hao wapya
watatumia Sh3.38 bilioni.
JAJI MSTAAFU, DAMIAN LUBUVA |
Mwenyekiti
wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva alisema tume imezingatia vigezo vya idadi ya
watu, upatikanaji wa mawasiliano, hali ya kijiografia na vigezo vingine kwa
mujibu wa kanuni za uchaguzi wa rais na wabunge ya mwaka 2010.
Maoni
ya wadau
Katibu
Mkuu wa NCCR - Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema ongezeko la majimbo hayo
halitakuwa na tija yoyote na badala yake yataongeza mzigo kupitia uchangiaji wa
bajeti ambazo ni kodi za Watanzania.
Kada
mwingine wa chama hicho, Samwel Ruhuza alisema hali hiyo itafanya nchi ishindwe
kujiendesha... “Mpaka sasa tunao wabunge 357 lakini angalia ni wangapi
wanaochangia mada na kujenga hoja bungeni hata robo ya hao hawafiki.”
Mhadhiri
wa Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Alexander Makulilo
alionya kwamba wakati NEC inafikiria kuongeza majimbo, ni vyema ikazingatia
uchumi wa nchi na manufaa ya majimbo haya kwa mwananchi mmojammoja.
Mhadhiri
wa chuo hicho, Bashiru Ally alisema NEC imefanya uamuzi sahihi kwani imepewa
mamlaka ya kupitisha majimbo mapya kulingana na vigezo vilivyopo.
Mbunge
wa Viti Maalumu (CCM), Zarina Madabida alisema takwimu za idadi ya watu
zinapaswa kuangaliwa kabla ya kuipelekea NEC kugawanya majimbo.
Mbunge
wa Ubungo (Chadema), John Mnyika alieleza kushangazwa na watu waliokuwa
wanapinga serikali tatu katika Bunge la Katiba kwa kigezo cha gharama, kuwa leo
ndiyo wanaotaka majimbo yaongezeke bila kujali gharama.
Mfanyabiashara
Masoud Ally wa Dar es Salaam alisema: “Ugawaji wa majimbo utagharimu fedha
nyingi za Taifa wakati kuna mahitaji makubwa.
Kauli
ya NEC
Mkurugenzi
wa NEC, Julius Malaba alisema madai hayo hayana tija kwani siyo kila aliyeomba
jimbo atapata.
Malaba
alisema si sahihi kulalamikia mchakato huo wakati Tume haijapokea hata
mapendekezo ya majimbo.
“Watanzania
wanatakiwa kusubiri kwanza tupokee mapendekezo ya kuongeza majimbo, tugawanye
kwa vigezo vilivyopo halafu ndipo wapime hoja zao lakini siyo sahihi kuibua
umuhimu wa kuongeza majimbo kiuchumi au kuhofia upendeleo,” alisema Malaba.
Mgawanyo
wa Dar
Mkoa
wa Dar es Salaam umependekeza majimbo mapya matano ya Mbagala, Kijichi,
Kibamba, Bunju na Chanika yaliyopitishwa juzi katika kikao cha Kamati ya
Ushauri ya Mkoa (RCC) na kufanya jumla ya majimbo 13 kutoka manane ya sasa.
Mbeya
wagoma
RCC
ya Mbeya imetupilia mbali maombi matano ya mapendekezo ya kugawa majimbo
yaliyowasilishwa na halmashauri saba kutokana na kutokidhi kigezo cha idadi ya
watu. Majimbo ya uchaguzi yaliyopendekezwa katika kikao cha dharura cha RCC
kilichofanyika jana ni Halmashauri ya Mbeya, Momba, Mbozi, Kyela, Jiji la
Mbeya, Rungwe na Mbarali na yaliyokataliwa ni Rungwe, Mbarali, Kyela na Jiji la
Mbeya.
Rukwa
waridhia
Wadau
wa Maendeleo mkoani Rukwa, wameridhia kugawanywa majimbo ya mawili ya Kwela na
Kalambo.
Tanga
bado
Mapendekezo
ya kuongezwa majimbo ya Mkoa wa Tanga kutoka 11 hadi kufikia 17
yaliyowasilishwa RCC yamepitishwa kwa shaka baada ya baadhi ya wajumbe kudai ni
mengi mno. Maombi yaliyowasilishwa ni ya Handeni Mjini, Handeni Vijijini, Tanga
Kaskazini, Tanga Kusini Korogwe Mashariki na Korogwe Magharibi, Muheza Mjini na
Muheza Vijijini huku Mlalo ikitakiwa igawanywe kuwa Mtae na Umba.
Chanzo: Mwananchi News Paper
Post a Comment