Katika kile kinachoonekana kuendelea
kujiimarisha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, vyama vinavyounda Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa) vimegawana maeneo mbalimbali nchini vikifanya
mikutano ya hadhara na mafunzo kwa viongozi wake ikiwa ni utekelezaji wa
mkakati wa ushindi.
Ukawa unaundwa na vyama vya Chadema, NLD,
NCCR-Mageuzi na CUF.
Chadema kilianza ziara zake mikoani wiki
zilizopita baada ya kuzindua mkakati wake uitwao ‘Hakuna kulala, Hakuna kula,
Mpaka Kieleweke’ nchi nzima wakati timu ya NCCR-Mageuzi ikiweka kambi mkoani
Kigoma kwa kile ilichokiita kuimarisha majimbo ya kimkakati.
Sanjari na vyama hivyo, CUF tangu juzi
kiliingia katika moja ya ngome zake, mkoani Mtwara pamoja na mipango mengine ya
kiushindi, kinahamasisha wananchi kujitokeza kujiandikisha kupiga kura.
Jitihada za Ukawa kuzunguka mikoani zinakuja
ikiwa ni majuma kadhaa tangu Chama cha Mapinduzi (CCM) kikiongozwa na Katibu
Mkuu wake Abdulrahman Kinana kilipomaliza ziara ya kujiimarisha na kukagua
utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2010.
Pia, ziara hizo ziligongana na zile za Chama
cha ACT - Wazalendo zilizosababisha Chadema na chama hicho kipya kugongana
Butiama.
ACT - Wazalendo kinachoongozwa na Zitto Kabwe
kilihitimisha ziara yake ya kimkakati katika mikoa tisa inayoonekana kuwa ngome
ya CCM, wiki iliyopita wilayani Bariadi, Shinyanga na kuvuna wanachama zaidi
6,000 katika mikoa hiyo.
NCCR-Mageuzi ipo Kigoma
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema
jana kuwa Ukawa ina mikakati inayofanana ndani ya vyama vyao ya kuhakikisha
inajiimarisha kisiasa nchi nzima ili ishinde Uchaguzi Mkuu.
Alisema siku 10 zilizopita, timu ya NCCR
ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti - Zanzibar, Haji Hamis Hamad ilianza ziara
Kigoma kuhakikisha majimbo ya mkoa huo yanaendelea kuwa ngome yake.
“Kigoma nzima ina majimbo yetu ya kimkakati na
Ukawa wameshatukabidhi sasa kilichobaki ni kufanya ‘political management’
(usimamizi wa kisiasa) katika kiwango kinachotakiwa.
“Katika kikosi hicho, pia wamo Katibu Mwenezi,
David Kafulila, Katibu Mkuu Mstaafu, Samuel Ruhuza na Kamishna wa Kagera,
Peterson Mshenyela na wengineo,” alisema Nyambabe.
Source: Mwananchi News
Post a Comment