Wakati viongozi wajuu wa CCM wakiendelea
kulalamikia makada wanaowatuhumu kutumia fedha kujifagilia njia ya urais,
mkurugenzi wa Takukuru, Dk Edward Hoseah amesema taasisi yake inakusanya
taarifa zote za wanachama wa chama hicho tawala wanaotuhumiwa kutumia mlungula.
Mara kadhaa viongozi wa juu wa CCM wamekuwa
wakiwaonya wanachama wao dhidi ya makada wanaotumia fedha kujitengenezea
mazingira mazuri ya kupitishwa na chama hicho kugombea urais, lakini wameeleza
kuwa hawawajibiki kuwaripoti Takukuru kwa kuwa ni wajibu wa chombo hicho cha
kuzuia na kupambana na rushwa kufanyia kazi malalamiko hayo.
Jumatano, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa
Halmashauri Kuu ya CCM, Nape Nnauye alisema Takukuru hawahitaji kupata mwaliko
wa CCM ili kufanya uchunguzi wa kukamata wagombea wanaotumia rushwa ndani ya
chama hicho kwani rushwa inayoendelea kwa sasa iko wazi.
“Kazi ya kuwafuatilia imeshaanza muda mrefu,
tunazo taarifa zao za kutosha kwa kila mwanasiasa anayelalamikiwa,” alisema Dk
Hoseah wakati alipoongea na gazeti hili kuhusu sababu za taasisi yake kukaa
kimya wakati ikielezwa hadharani kuwa rushwa imezidi katika harakati za
uchaguzi ndani ya CCM.
Dk Hoseah alisema kwa muda mrefu Takukuru
imekuwa ikifuatilia mienendo ya wanasiasa wanaotaka uongozi kupitia chama hicho
na ambao wanatuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Alisema Takukuru kwa sasa inaendelea na kazi
yake ya uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo huku ikikusanya taarifa za kila
mwanasiasa anayeonekana kutuhumiwa na vitendo vya rushwa.
“Siyo kwamba Takukuru haijaona wala haisikii
malalamiko ya viongozi CCM. Tunajua wajibu wetu na kazi ya kuwafuatilia
imeshaanza,” alisema Dk Hoseah.
“Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010
imekataza wazi kwamba, ni makosa kutoa chochote kama zawadi kwa kundi la watu,
vinginevyo ni kukiuka sheria hiyo. Labda kama anaonekana kuwa na fedha nyingi
basi ajenge hata barabara kuliko kufanya hivyo.”
Dk Hoseah aliongeza kuwa sheria pia inazuia
kuanza kampeni kabla ya muda kupangwa rasmi na Tume ya Taifa (Nec), kwa hivyo
muda wa kampeni utakapoanza, itarahisisha kukusanya taarifa zake na kuchukua
hatua kwa wanasiasa hao.
“Kwanza ni kosa kufanya kampeni kabla ya muda,
lakini pia ni kosa kutoa zawadi kama maji ya kunywa kama unafahamu kuwa wewe ni
mwanasiasa utakayegombea. Sheria yetu ya Takukuru inaweka wazi pia kitendo
hicho ni kosa,” alisema Dk Hoseah.
Source: Mwananchi
News
Post a Comment